27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KASI YA WATANZANIA KUZALIANA YATISHIA MAENDELEO YA JAMII

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

HAIKUWA rahisi kwa Mariam Mussa, mkazi wa Temeke kumshawishi mumewe (jina tunalihifadhi) kuanza kutumia njia za uzazi wa mpango.

“Nilikutana na mume wangu huko Tandika mwaka 2010 wakati huo nilikuwa nikifanya biashara ndogondogo katika soko la Tandika, wote tulikuwa
wafanyabiashara sokoni hapo, tulipendana na kukubaliana kuishi,” anasema.

Anasema mwaka uliofuata alihisi kuwa ni mjamzito akaamua kwenda katika kituo cha afya ambapo alifanyiwa vipimo vilivyothibitisha kweli ni
mjamzito.

“Tulibahatika kupata mtoto wetu wa kwanza wa kiume, nilijifungua katika hospitali ya binafsi ambako huko walinishauri nianze kutumia njia za uzazi wa mpango,” anasema.

Anasema alirudi nyumbani kwake na kumjulisha mumewe taarifa hizo ambazo hata hivyo alionesha wazi kutokubaliana na suala hilo.

“Hakuonesha furaha yake niliyoizoea kuiona kila nilipomueleza jambo ambalo lilimpendeza, aliniangalia kwa hasira mno basi nikanyamaza na kuacha kabisa kulizungumzia suala hilo,” anasema.

Mariam anasema pamoja na kukaa kimya huko aliamua kufanya jambo hilo mwenyewe kwa siri pasipo kumshirikisha mumewe.

“Nilianza kutumia njia ya sindano ambapo haikuwa rahisi kwake kubaini kwani nilikuwa nikienda kuchoma kule hospitalini, nilipoona mwanangu
amefikia umri wa miaka miwili niliacha kuchoma nikabeba ujauzito wa pili,” anasema.

Anasema ilimlazimu kuacha matumizi ya uzazi wa mpango kila baada ya miaka miwili ili mumewe huyo asishitukie juu ya jambo hilo aliloamua kulifanya mwenyewe.

“Sasa hivi tuna watoto watatu, bado sijamueleza kwamba niliamua mwenyewe kutumia njia ya uzazi wa mpango kwani nina wasiwasi kwamba
huenda ataniacha jambo ambalo sipo tayari kuona likitokea,” anasema.

Si Mariam pekee anayekumbana na hali hiyo, jamii nyingi zilizopo katika Bara la Afrika hasa Tanzania zinaamini kwamba suala la kupanga uzazi ni la mwanamke pekee na wala halimuhusu kabisa mwanamume.

Frank Eugene (38) anasema haoni sababu ya mwanamume kupanga uzazi na wala si jukumu lao kabisa.

“Hakuna sababu ya kumlazimisha mwanamume atumie njia za uzazi wa mpango au kumshawishi mwanamke kutumia njia ya uzazi wa mpango,
wakati hata vitabu vya dini vinatueleza tuliletwa duniani ili tuzae tuijaze nchi,” anasema.

Msimamo huo wa Eugene ndiyo walio nao wanamume wengi ambao Ofisa Mawasiliano na Utetezi wa Chama cha Malezi Tanzania (Umati), Josephine
Mugishangwe anasema si mtazamo sahihi.

“Ni kweli Mwenyezi Mungu anasema tuzae lakini ni lazima kuangalia na kupanga idadi ya watoto ambao mtu anao uwezo wa kuwahudumia na kuwapa malezi bora na elimu bora itakayomsaidia katika maisha yake ya baadae,” anasema.

Hali halisi
Takwimu zinaonesha kwamba kasi ya kuzaliana nchini kwa sasa ni kubwa hali ambayo inasababisha kuwapo kwa  ongezeko kubwa la idadi ya watu
nchini.

Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 1967 idadi ya watu iliongezeka kutoka milioni tisa ilivyokuwa mwaka 1961 hadi kufikia watu milioni 12.3.

Aidha, katika sensa ya mwaka 2012 idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia watu milioni 45.

Inakadiriwa kila mwaka Watanzania milioni 1.5 wanazaliwa na hivyo huenda idadi hiyo imefikia zaidi ya milioni 50 tangu kufanyika kwa sensa hiyo ya mwaka 2012.

Ofisa Habari wa Tume ya Mipango Tanzania, Adili Mhina anasema kasi ya ongezeko hilo imesababisha kuwapo kwa changamoto kubwa ya upungufu wa miundombinu na huduma za kutosheleza mahitaji.

“Mahitaji yameongezeka kwa sababu kuna shinikizo la ongezeko la idadi ya watu, kila mwaka vijana milioni 1.2 wanafikia umri wa kuingia
katika soko la ajira lakini vijana 300,000 pekee ndiyo wanaobahatika kuajiriwa.

Athari zake

Mhina anasema kutokana na hali hiyo leo hii kunashuhudiwa wimbi kubwa la watu hasa vijana wakihama katika maeneo ya mijini kutafuta ajira.
“Ndipo pale tunashuhudia uanzishwaji wa maeneo ya biashara zisizo rasmi yasiyoendana na taratibu za ustawi wa jamii pamoja na ujenzi wa makazi holela,” anasema.

Meneja Utetezi wa Shirika la Advance Family Planning (AFP), James Mlali anasema ongezeko hilo ni hatari kwani linaweza kuja kuathiri uchumi wa nchi hapo baadae.
“Kuna uhusiano mkubwa kati ya suala la uzazi wa mpango na maendeleo, leo hii tunashuhudia idadi ya watoto wanaoanza elimu ya msingi haiendani na idadi ya miundombinu iliyopo.

“Yaani mahala pengine majengo hayatoshelezi, vifaa havitoshelezi, walimu hawatoshelezi, idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya navyo siku hizi havitoshelezi,” anasema.

Anaongeza: “Tafiti zinaonesha kama tutazidi kuongezeka miaka 25 ijayo tutahitaji kuwa na vituo vya afya mara tatu ya hivi vilivyopo sasa, yaani kama tuna vituo 7,000 basi tutahitaji kuwa na vituo 21,000 kama tuna shule za msingi 10,000 tutahitaji kuwa na shule 30,000.
“Aidha, tutashuhudia pia ongezeko kubwa la ukosefu wa ajira, upungufu wa wataalamu, ongezeko la watu wanaohamia katika maeneo ya mijini, ni
hatari kwa maendeleo ya nchi,” anabainisha.

Nini kifanyike
Kaimu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA-Tanzania), Dk. Hashina Begum anasema ni muhimu kupanga uzazi.

Anasema afya ya uzazi iliyo nzuri inayoambatana na njia za uzazi wa mpango inaweza kukuza uchumi na kuchangia maendeleo endelevu kwani  anawake hupata fursa ya kumaliza elimu na kuwa sehemu ya nguvu kazi kuchangia pato la taifa na familia zao.

Anasema afya ya uzazi wa mpango ni muhimu katika kufikia lengo namba moja la Maendeleo Endelevu (SDG’s) ambalo ni kutokomeza
umaskini, njaa na mengineyo.

Anasema hata hivyo hali inaonesha kila siku wanawake walio katika mazingira hatarishi hasa walio masikini na wakimbizi wanakumbana na
changamoto za kijamii, kiuchumi na kijiografia zinazowakosesha kupata huduma za uzazi wa mpango.

“Pamoja na hatua kubwa zilizofanywa lakini changamoto bado zipo, wanawake milioni 214 katika nchi zinazoendelea wanakosa taarifa za
uzazi wa mpango na wengi wao wanaishi katika mataifa 69 yaliyo maskini duniani,” anasema.

Dk. Begum anasema shirika hilo limejipanga kuhakikisha linakabili changamoto za kukosekana kwa huduma za uzazi wa mpango nchini ifikapo mwaka 2030 hata hivyo ili kufikia lengo hilo ni lazima pawapo ushirikiano wa dhati kati ya serikali na wadau wengine wa maendeleo.

“Serikali ya Tanzania inajitahidi mno kuwekeza katika suala la uzazi wa mpango lakini jambo tunaloliona ni kwamba elimu zaidi inahitajika kuwafikia jamii, iwapo itapata elimu hiyo na kuitumia vizuri serikali itaweza kuokoa kiasi cha Dola moja hadi sita inazowekeza huko
na kuzitumia katika shughulki zingine za maendeleo,” anabainisha.

Faida ya kupanga uzazi
Mratibu wa Dawa za Uzazi wa Mpango wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Cosmas Swai anasema kuna faida nyingi iwapo wenza wataamua kupanga uzazi.

“Uzazi wa mpango ndiyo njia pekee itakayotuwezesha kukabili ongezeko kubwa la idadi ya watu lililopo sasa,” anasema.
Dk. Swai anasema matumizi ya njia za uzazi wa mpango husaidia kuzuia vifo vya uzazi kwa kina mama kwa kiwango cha asilimia 30 hadi 50.
Anasema pia husaidia kupunguza ongezeko la idadi ya watu na hupunguza uwezekano wa kuharibika kwa mimba.
“Hatua hiyo pia inasaidia kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga, ikiwa tutachagua njia za uzazi wa mpango kupanga uzazi itatuwezesha
pia kuwa na Taaifa bora,” anasema.
Anaongeza: “Wakina mama nao wataweza kushiriki katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na hivyo watakuza uchumi wa familia zao na Taifa kwa ujumla.

Ushauri
Dk. Swai anawatoa hofu wanawake juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango na kusisitiza kuwa njia hizo hazina madhara yoyote kwa
mtumiaji.

“Isipokuwa wanaweza kupata maudhi madogo madogo lakini si wote, inaweza kweli kutokea mwingine akanenepa au akapungua,
lakini kama mwanamke ameanza kutumia njia moja wapo ya uzazi wa mpango na ikamsumbua ni vema arudi kwa wataalamu wa afya wamsaidie,”
anashauri.

Anasema upo mtazamo kwenye jamii kwamba njia za uzazi wa mpango husabisha saratani hata hivyo si kweli kwani husaidia kupunguza uwezekano wa mtu kupata maradhi hayo.

Serikali ilivyojipanga
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Maendeleo  ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Neema Rusibayamila anasema serikali imekusudia kuongeza kiasi cha fedha kutoka Sh bilioni 14 hadi Sh bilioni 17 ifikapo 2020 zitakazotumika kuboresha huduma za uzazi wa
mpango nchini.

Dk. Neema ndiye ambaye aliiwakilisha Tanzania katika mkutano wa kimataifa kuhusu masuala ya uzazi wa mpango uliosimamiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA).

Anasema hatua hiyo imelenga kuhakikisha huduma za kisasa za uzazi wa mpango zinapatikana kwa kiwango cha asilimia 100 ifikapo 2020 kutoka kiwango cha asilimia 94 kilichopo sasa.

“Tumekusudia pia kuongeza idadi ya vituo vya afya vinavyotoa huduma za afya ya uzazi kwa vijana kutoka asilimia 30 mwaka huu hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2020,” anasema na kuongeza:
“Dhamira yetu ni kufikia maelfu ya wanawake na wasichana na kuwapa elimu kuhusu afya ya uzazi na huduma za kisasa za uzazi wa mpango, tumekusudia kuwafikia wasichana 345,000 kufikia mwaka huo.

Naibu Katibu wa Tume ya Mipango, Ibrahim Kalengo anasema ili kukabili hali hiyo mwaka 1992 serikali ilipitisha sera ya Taifa ya Idadi ya
Watu.
“Mwaka 2006 serikali iliandaa sera mpya ambayo kwa sasa nayo inafanyiwa mapitio ili kuendana na mahitaji ya wakati wa sasa kutokana na maendeleo na mabadiliko mbalimbali ya kitaifa na kimataifa,” anasema.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles