27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Shahidi: Tulipiga risasi 90 kutawanya Chadema

PATRICIA KIMELEMETA –Dar es Salaam

MKUU wa Operesheni Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, SSP Gerald Ngichi, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa walifyatua risasi zaidi ya 90 kwa ajili ya kuwatawanya waandamanaji waliojitokeza katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Shahidi huyo wa upande wa mashtaka katika kesi ya kufanya mkusanyiko usio halali inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake wanane, alieleza hayo mahakamani hapo jana wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya ushahidi.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Ngichi alieleza hayo baada ya wakili wa utetezi John Malya kumuuliza idadi ya risasi zilizofyatuliwa katika maandamano hayo.

Alidai kuwa alilazimika kuwaamuru askari polisi zaidi ya sita kufyatua risasi baada ya kuona kuna waandamanaji zaidi ya 500 waliokuwa wakielekea Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.

“Kulikuwa na waandamanaji zaidi ya 500 waliokuwa wakielekea Ofisi ya Mkurugenzi Kinondoni, tuliwakataza lakini walikaidi, nililazimika kuwaamuru askari zaidi ya watano waliokuwa na silaha AK 47 kufyatua risasi hewani ili kuwazuia,” alidai Ngichi.

Alidai kuwa wakati wanawatawanya, walikuwa mita 100 kutoka kwa waandamanaji, ambao waliwaangalia uso kwa uso huku wakiendelea kuwasisitiza wasiandamane.

Ngichi alidai kuwa risasi zikipigwa hewani zinakwenda umbali wa mita 500 na zaidi, lakini zikishuka chini zinakuwa umbali wa mita 20 hadi 30, lakini inakuwa haina madhara.

Alieleza kuwa ikiwa wataleta ushahidi wa watu ambao wameumia wakati wa maandamano hayo, mahakama itaamua.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka umewakilishwa na jopo la mawakili Faraja Nchimbi, Paul Kadushi, Wankyo Saimon na Jacline Nyantori wakati upande wa utetezi ulikuwa na jopo la mawakili Profesa Abdalah Safari, Peter Kibatala, John Malya, Hekuma Mwasipu na Jeremiah Ntobesya.

 Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kusababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles