30 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Serikali yawatua ndoo kichwani kina mama Mkata

Na JOVINA BUJULU – MAELEZO

ZAIDI ya Sh bilioni mbili zilizotolewa na Serikali zimerejesha matumaini kwa wakazi wa vijiji vya Mkata Mashariki na Magharibi baada ya kuwapatia maji safi na salama kutoka katika chanzo cha maji kilichopo Bwawa la Mkata na kufanikiwa kuwatua ndoo kichwani kina mama wa vijiji hivyo. 

Kwa muda wa zaidi ya miaka kumi, wananchi wa Mji wa Mkata na vitongoji vyake wamekuwa wakihangaika kutafuta maji mabondeni kwenye visima au kusubiri maji ya kununua kwenye magari. Mbali na kupata maji kwa shida, walikuwa wakitumia muda mwingi kufuata maji hayo huku uzalishaji ukidorora.

Ofisa Mipango wa Wilaya ya Handeni Vijijini, Edina Katalaiya, anasema mradi huu ulianza mwaka 2013 ukiwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP), lakini haukuweza kuwafikishia maji wananchi wa Mkata kutokana na utendaji usioridhisha wa wasimamizi waliokuwapo wakati huo.

“Mradi huu ulikuwa umetekelezwa chini ya kiwango hivyo kushindwa kuwapatia wananchi wa Mkata maji, lakini baada ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani mwaka 2016, ilitoa cha Sh 960,683,299 kwa ajili ya kujenga bwawa na Sh 1,370,421,695 kwa ajili ya kutandaza mabomba ya kusambaza maji kutoka katika bwawa la Mkata na kuyapeleka kwenye vijiji hivyo,” anasema Katalaiya.

Anabainisha kuwa mradi huo uliokamilika mwaka 2019 mwishoni, unawahudumia wananchi wapatao 14,550 ambao ni sawa na asilimia 77 ya wakazi wote wa vijiji vya Mkata Mashariki na Magharibi, ambapo kuna vituo vya maji 28.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumiaji wa Maji katika Mji wa Mkata, Aweso Juma, anasema wakazi wa mji huo hawakuwa na maji kwa zaidi ya miaka kumi ambapo kina mama walikuwa wakiamka alfajiri kwenda bondeni kufuata maji, hali ambayo ilikuwa kero katika familia zao na hata wakati mwingine kusababisha ugomvi ndani ya familia.

Anaongeza kuwa maji hayo yalikuwa na chumvi lakini ilibidi wayatumie hivyo hivyo na wakati mwingine ilikuwa ikiwalazimu kununua maji yaliyokuwa yanaletwa na magari kutoka Mbwewe ambapo ndoo moja iliuzwa kwa Sh 500 hadi 800.

“Natoa shukrani nyingi kwa Rais Dk. John Magufuli na serikali yake kwa kutuona wananchi wa Mkata na kuweza kutatua kero hii iliyodumu kwa zaidi ya miaka kumi ambapo kina mama walikuwa wakifuata maji kwa zaidi ya kilometa moja na nusu kilasiku na kuwafanya kushindwa kufanya shughuli nyingine za uzalishaji mali kwa sababu hiyo,” anasema Aweso.

Akielezea namna wanavyolipia maji hayo, anasema mara baada ya Serikali kuwafikishia maji hayo katika vituo vya maji, walianzisha Jumuiya  za watumiaji wa maji ambapo walifungua akaunti benki kwa ajili ya kuweka fedha wanazokusanya baada ya kuuza maji ambapo ndoo moja huuzwa kwa Sh 50.

“Vituo vyote vya maji vinasimamiwa na Jumuiya za watumiaji wa maji ambapo fedha zote zinazokusanywa zinawekwa benki na inapotokea uharibifu au uchakavu wa mabomba katika kituo chochote hutumika kwa ajili ya matengenezo,” anasema Aweso.

Kwa upande wake mkazi wa Mkata ambaye amenufaika na mradi huo, Mwanahamisi Said, anaelezea furaha yake ya kufikishiwa maji kijijini hapo na kuishukuru Serikali kwa kuwatua ndoo kichwani kina mama hao kwani kero ya maji ilikuwa kubwa kwao kiasi cha kuwasababishia ugomvi mkubwa wanapokuwa visimani kufuatilia maji.

Mwananchi mwingine, Mbaraka Chumi, ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Negero, Mkata, anasema walikuwa wananunua maji kwa gharama kubwa na wakati mwingine yalikuwa hayapatikani ambapo walilazimika kutumia saa mbili hadi tatu kushuka bondeni kufuata maji yenye chumvi yasiyoweza kunyweka, ambayo walikuwa wanauziwa ndoo moja kwa Sh 100 hadi 200.

Utekelezaji wa mradi wa maji, Mkata, umewanufaisha wananchi wa Mji wa Mkata zaidi ya 14,000. Mji huo una vijiji vitatu na vitongoji 15, ambapo Serikali ya imeliona tatizo hilo lililowakabili kwa muda mrefu na kulitafutia ufumbuzi.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,348FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles