30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 23, 2021

Mbinu zinazotumika kukusanya damu kipindi cha corona kuepuka maambukizi

Na AVELINE KITOMARY, Dar es Salaam

DAMU ni kiowevu (tishu) katika mwili wa binadamu na mnyama, ambapo huzunguka  mwilini kupitia mishipa ikisukumwa na moyo kwa lengo la kumwezesha mtu au mnyama kuishi.

Kazi ya tishu hiyo ni kupeleka lishe na oksijeni kwenye seli za mwili na kutoa uchafu katika seli hizo.

Damu ni kitu ambacho hakiwezi kutengenezwa wala kuundwa katika maabara, la sivyo hupatikana kwa binadamu kuitoa na kumpa mwenzake aliyepungukiwa.

Uhitaji wa damu huja pale ambapo mtu ameishiwa baada ya kuvuja damu nyingi au hata lishe duni na kutakiwa kuongezwa hivyo basi, damu ni muhimu zaidi kwa uhai wa mwanadamu.

Kila ifikapo Juni 14, kila mwaka, Dunia huadhimisha siku ya kimataifa ya  kuchangia damu, tukio hilo linalenga  kuwashukuru watoaji damu  kwa hiari  katika kusaidia maisha ya wahitaji.

Tukio hilo pia linalenga kuhamasisha na kuhakikisha ubora, usalama na uwezekano wa damu kupatikana kuwa mkubwa ili kusaidia wagonjwa wenye uhitaji kwa haraka zaidi.

Licha ya malengo hayo, Juni 14 pia ni siku aliyozaliwa mvumbuzi wa makundi  ya damu ABO, raia wa Australia, Dk. Karl Landsteiner, ambaye alizaliwa mwaka 1868.

Uvumbuzi aliofanya hadi sasa umesaidi damu kuweza kutumika katika makundi na kuepusha hatari iliyokuwapo mwanzo, ya mtu kuongezewa damu na kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), watu milioni 92   wanatoa damu kwa hiari kila mwaka huku karibu asilimia 50 ya watu wanaochangia damu wanatoka katika nchi zilizoendelea.

Kila mtu mmoja anayechangia damu anaweza kuokoa maisha ya watu watatu huku uhifadhi wa mazao ya damu ukiwasaidia wagonjwa wengine kama wa saratani ya damu, moyo, figo na wengine.

Hapa nchini, Mpango wa Taifa wa Damu Salama umekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha damu inapatikana kwenye hospitali zote ili wagonjwa wa dharura na wale wasio wa dharura waweze kupata  kwa haraka.

Hatua hii imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha ya wagonjwa hasa wale wa dharura.

Ukusanyaji wa damu umekuwa ukizingatia  mambo kadhaa kama usalama katika upatikanaji, uhifadhi, usambazaji na ubora unaofaa kwaajili ya matumizi ya binadamu ukizingatia makundi. 

Kwa mwaka huu 2020, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, atakuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo huku kauli mbiu ikiwa ni “Damu Salama Inaokoa Maisha” (Safe Blood Saves Lives).

Kauli mbiu hiyo inaonesha mshikamano katika uchangiaji damu pia inalenga mambo muhimu ambayo yanaonyesha thamani ya mwanadamu kama heshima, huruma, wema na kuwajali wengine vitu hivyo ndio msingi wa kuendeleza uchangiaji damu wa hiari bila malipo yoyote.

Uchangiaji damu ni zoezi ambalo halina mwisho hivyo kila siku watu wanatakiwa kujitokeza kwa hiari kuchangia na inapotokea kuwa hakuna damu hali huwa mbaya kwa wahitaji.

CORONA YAPOROMOSHA KIWANGO CHA DAMU

Licha ya ongezeka la asilimia 60 kutoka 40  ya kiwango cha damu kwa kipindi cha mwaka jana hadi Januari mwaka huu, hivi sasa ongezeko hili limeporomoka kutokana na kiwango cha uchangiaji damu kushuka.

Kushuka kwa kiwango cha uchangiaji damu kumefanya kiwango cha uhitaji damu kuongezeka katika hospiatali mbalimbali hapa nchini hasa zile kubwa.

Kwa sasa, kila kukicha hospitali kadhaa zimekuwa zikihamasisha watu kujitokeza kuchangia damu huku wakitaja kuzingatia maelekezo ya wahuduma wa afya katika kujikinga na Covid-19.   

Mkuu wa Idara ya Ukusanyaji wa Mpango wa Damu Salama, Dk. Avelina Mgasa, anasema katika kipindi hiki cha mlipuko wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid-19), kiwango cha uchangiaji damu kinaendelea kushuka siku hadi siku. 

Dk. Mgasa anasema takwimu zinaonesha kupungua kwa makusanyo ya damu kuanzia Aprili ambapo mpango huo ulikusanya jumla ya chupa 22,044 ikilinganishwa na chupa 25,737 mwezi Machi na 31,502 Februari.

“Hali hii imechangiwa na kufungwa kwa shule, vyuo, kukosa fursa ya kukusanya damu katika ofisi mbalimbali kwani kupitia haya makundi tulikuwa tunapata damu nyingi.

“Kitu kingine ambacho kimepunguza kiwango cha uchangiaji damu ni baada ya serikali kuweka zuio la mikusanyiko katika kukabiliana na corona, hata mtu mmoja mmoja anaogopa kufika kwa sababu ya hofu,” anasema Dk. Mgasa. 

WALIVYOJIPAMGA KUONGEZA KIWANGO CHA DAMU 

Dk. Mgasa anasema kwa sasa wamejipanga kuhakikisha uwapo wa uchangiaji damu ulio salama, kwa kuweka mikakati  mbalimbali ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona katika vituo vya kuchangia damu.

Anasema hatua za kiafya zinazotumika ni uwapo wa maji tiririka na sabuni kwaajili ya kunawa mikono, vitakasa mikono, vifaa kinga kwa watumishi kama barakoa, apron/koti, gloves na Thermo scanner kwaajili ya kupima joto la mwili kwa kila mchangiaji damu.

“Tahadhari nyingine tutakazozichukua ni kutakasa vitanda na vifaa vinavyotumiwa na wachangia damu, tutaweka mpangilio unaozingatia umbali kati ya mtu na mtu (social distance),” anaeleza.

Anasema katika utaratibu huo mpya, watazingatia hatua muhimu sita kwa watumishi wa mpango wa damu salama ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanavaa vifaa kinga ambavyo ni pamoja na gloves na koti maalum.

“Mchangia damu ataelekezwa mahali pa kunawa mikono yake kwa maji tiririka na sabuni au kutakasa mikono yake kwa vitakasa mikono kabla ya kuchangia damu, hii ikiwa ni pamoja na kupimwa joto la mwili.

“Mchangiaji damu atapitishwa kwenye fomu yenye maswali mbalimbali yakiwamo yanayohusu Covid-19 na mtumishi wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama atajaza majibu katika fomu hiyo.

“Anayechangia damu atafanyiwa vipimo vya awali ikiwamo kuangaliwa hali yake (physical assessment), msukumo wa damu (blood pressure) na kiwango cha damu (haemoglobin level) ili kuhakikisha kabla ya kuchangia awe ana afya njema,” anabainisha Dk. Mgasa. 

JE, MWENYE CORONA ANARUHUSIWA KUCHANGIA DAMU?

Wataalamu wa afya wanathibitisha kuwa virusi vya corona huambukizwa kwa njia ya mfumo wa hewa na hivyo kuathiri mapafu.

Virusi hivyo huweza kuingia mwilini kwa kupitia pua, mdomo na macho endapo mtu atakuwa navyo katika mikono yake.

Hii ndio sababu hasa kwa wataalamu wa afya kusisitiza unawaji wa mikono wa mara kwa mara.

Dk. Mgasa anasema hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kuwa virusi vya corona vinaweza kuenea kwa njia ya damu.

“Kutokana na hilo virusi hivyo haviwezi kuambukizwa kwa njia ya damu aidha, kwa kuongezewa damu au kuchangia damu.

“Kabla ya kuchangia damu tutampima mchangiaji vizuri na kuchukua damu lakini kama mtu ana virusi vya corona hataruhusiwa kuchangia damu, tunasubiri hadi apone ndipo ataruhusiwa kuchangia baada ya kuthibitika hana tena virusi hivyo.

“Hivyo, watu ambao waliwahi kuugua virusi vya corona wanaweza kuchangia pia,” anasisitiza.

MALENGO YA KAMPENI

Katika maadhimisho ya mwaka huu,  mpango wa damu salama umeandaa timu za halmashauri, mikoa na hospitali za kanda huku kila moja ikitakiwa kukusanya chupa 100, jumla ya chupa 22,000 zinatarajiwa kukusanywa na timu za kanda.

Dk. Mgasa anasema maeneo yaliyokusudiwa katika kukusanya damu hizo ni vyuo, kambi za jeshi, sehemu za wazi na maofisini.

“Katika kampeni hizo pia tutawafundisha watumishi wa afya juu ya matumizi sahihi ya damu kwa wajawazito na wakati wa kujifungua.

“Mahitaji kwa mwaka 2020 ni chupa 550,000 ambayo ni asilimia moja ya idadi ya wananchi kwa makadirio ya takwimu za mwaka 2020 au chupa 10 kwa kila wananchi 1,000.

“Tunalenga kukusanya chupa 375,000 ambazo ni asilimia 70 ya mahitaji kwa mwaka huu, kwa kipindi kilichopita kuanzia Juni hadi Julai, mwaka 2018, hadi 2019 chupa 309,376, zilikusanywa na katika kipindi cha Juni mwaka 2019 hadi 2020, chupa za damu 322,693 zilikusanywa,” anafafanua Dk. Mgasa.

Dk. Mgasa anatoa wito kwa jamii kujitokeza kuchangia damu kwani uchangiaji damu umewekwa katika mazingira salama.

“Wanaweza kutembelea vituo vyetu vyote  vya kanda za mpango wa Taifa wa Damu Salama, hospitali zote za wilaya na mikoa nchini,” anasema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
157,796FollowersFollow
518,000SubscribersSubscribe

Latest Articles