26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Serikali yatakiwa kupunguza kodi vifaa vya intaneti

internet-marketing-2

Na JONAS MUSHI, DAR ES SALAAM

SERIKALI imeshauriwa kupunguza ushuru wa vifaa vinavyotumia intaneti ili kuongeza kasi ya maendeleo ya shughuli za kiuchumi na kijamii zinazotegemea huduma hiyo.

Wito huo umetolewa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni inayotoa huduma za mitandao ya Ericsson, Frode Dyrdal, wakati wa uzinduzi wa mitambo ya gharama nafuu ya kusambaza intaneti.

Alisema huduma ya intaneti inasaidia kuendeleza sekta za elimu, afya, fedha na burudani, hivyo ni kiungo muhimu katika kuinua uchumi wa nchi.

“Wakati sisi tunajitahidi kuhakikisha upatikanaji wa intaneti kwa gharama nafuu, ni vyema Serikali ikaangalia namna ya kuwafanya watu wengi wawe na vifaa vinavyotumia intaneti na njia mojawapo ni kupunguza ushuru wa bidhaa za aina hiyo,” alisema.

Alisema utafiti unaonyesha kwamba ni watu wanne kati ya 10 ndio wanaoweza kupata intaneti barani Afrika.

Alisema hali hiyo ni tofauti na nchi zilizoendelea ambapo watu tisa kati ya 10 wanapata huduma ya intaneti suala, linalosaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumzia kuhusu mitambo yao, alisema imelenga kutatua changamoto za upatikanaji mdogo, maendeleo endelevu na gharama kubwa za huduma ya intaneti nchini.

“Bado upatikanaji wa intaneti nchini Tanzania ni mdogo ikilinganishwa na mahitaji na takwimu zinaonyesha kwamba kwa bara la Afrika, watu 500,000 wanahitaji huduma hiyo kila siku,” alisema Dyrdal na kuongeza:

“Pamoja na upatikanaji mdogo, umekuwa wa gharama kubwa kutokana na gharama kubwa za uwekezaji na umiliki wa miundombinu yake.”

Naye Mkuu wa Bidhaa za Mtandao wa Ericsson, Henric Linnet, alisema kutokana na changamoto hizo, wameweza kugundua mitambo ya kusambaza intaneti ambayo inapunguza gharama za uwekezaji kwa asilimia 40.

“Tumegundua mtambo wa mawimbi (Radio) ambao unatumia nishati ndogo na unaweza kuwekwa kwenye mnara na kusambaza intaneti za 2G, 3G na 4G,” alisema Linnet.

Alisema ugunduzi huo ni fursa kwa mitando ya simu kuwapatia wateja wengi huduma ya intaneti yenye ubora kwa gharama nafuu sehemu yoyote nchini.

“Kutokana na mitambo yetu kutumia nishati ndogo, inaweza kufungwa sehemu ambazo hazina umeme kwa sababu zinaweza kuendeshwa kwa umeme wa jua na hivyo itasaidia kufikia watu wengi wenye uhitaji wa intaneti,” alisema Linnet.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,663FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles