27.5 C
Dar es Salaam
Sunday, December 3, 2023

Contact us: [email protected]

SERIKALI YASALIMU AMRI KWA WENYEVITI WA MITAA

Na Aziza Masoud-Dar es Salaam


George SimbachaweneSERIKALI imesitisha mwongozo wa Novemba mwaka jana uliowataka wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vijiji kurudisha mihuri, hadi utaratibu mzuri wa kutekeleza agizo hilo utakapopangwa.

Umuzi huo wa Serikali umekuja siku moja baada ya wenyeviti hao wa Mkoa wa Dar es Salaam kutangaza kususia shughuli za maendeleo kwenye mitaa yao ikiwemo kufichua wahalifu.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (Tamisemi), George Simbachawene,  alisema kusitishwa kwa mwongozo huo kumetokana na  baadhi ya wenyeviti kulichukulia agizo hilo kama hujuma za  kutaka kupokwa madaraka waliyonayo katika maeneo yao jambo ambalo si kweli.

“Nasitisha mwongozo uliotolewa hadi tutakaposhirikiana na wahusika kuona namna bora ya kuutumia, lakini wahusika wanapaswa kufahamu kwamba hatukuwa na nia mbaya bali lengo lilikuwa ni kuwabana wenyeviti  wasio waaminifu.

“Suala hili limetuletea madhara makubwa kwa ngazi ya Serikali za Mitaa mpaka kuna watu wametangaza kwenda mahakamani kuhoji hatua hii na wengine wanaendelea kufanya mikutano katika maeneo yao.

“Kwa hali hiyo nafuta mwongozo huu  ili wenyeviti mwendelee kuwa na mihuri mpaka tutakaposhirikiana kuona namna bora ya kutumia agizo hili,” alisema Simbachawene.

Alisema Serikali iliamua kuweka mwongozo huo kwa lengo la kupunguza migogoro mbalimbali inayojitokeza hasa ya ardhi inayotokana na wenyeviti ambao wanatumia mihuri hiyo kumilikisha watu maeneo kinyume cha sheria.

Alisema katika maeneo ya vijijini wapo baadhi ya wenyeviti  wa vijiji ambao wanatoa vibali vya ufugaji kwa  kutumia mihuri hiyo.

“Mtu akishapatiwa eneo na kupewa karatasi yenye muhuri wa Serikali ya Mtaaa ama kijiji  ambao una nembo ya  Serikali anatumia karatasi hiyo kama silaha za kupata uhalali wa kumiliki eneo husika hata kama kapatiwa kinyume na sheria kwa hivyo hii mihuri mnaitaka kwa sababu tu ya faida zenu chanya, ” alisema Simbachawene.

Alisema Sheria ya Mipango Miji namba nane ya mwaka 2007 inaonyesha maeneo ya mipango miji yanayopaswa kuwa wazi lakini wenyeviti kwa kutumia mihuri wamekuwa wakishiriki kuuza maeneo hayo.

“Tumefika hapa kwa sababu ya mazoea tuliyonayo baadhi ya wenyeviti wamekuwa wakitembea na mihuri mifukoni  na kuwagongea watu kuwatambulisha hata wasio husika na kuuza viwanja vya Serikali jambo ambalo si sawa,” alisema Simbachawene.

Alisema Wenyeviti wa Serikali za Mitaa si lazima kumiliki muhuri kisheria kwa mujibu wa tangazo la Serikali namba tatu la mwaka 1994  linaelekeza vifaa anavyopaswa kumiliki  kiongozi huyo ambavyo ni bendera, orodha ya wakazi wa eneo husika na daftari la kumbukumbu.

“Mimi naona pengine tumetofautiana katika tafsiri katika jambo hili, mtu anayegonga muhuri lazima awe na kibali anachokitoa kisheria na si vinginevyo,” alisema Simbachawene.

Aliongeza si kweli kwamba kutokuwa na muhuri kutamfanya mwenyekiti ashindwe kufanya shughuli zake za kila siku kwa kuwa kila kinachofanyika kuhusu mtaa anapaswa kushirikiana na mtendaji ambaye anamiliki muhuri.

“Tukisema kila mtu awe na muhuri haiwezekani, mfano Rais Dk. John Magufuli hana muhuri, akitaka muhuri anaenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi huo ndiyo utaratibu sasa kwa wenzetu hawa kwa kuwa wameshazoea kumiliki vitu hivi wanaona kama wanaonewa,” alisema Simbachawene.

Naye Katibu wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wa  Mkoa wa Dar es Salaam,  Mariam Machacha,  alisema wamefurahishwa na uamuzi huo wa Serikali na kwamba wanaamini jambo hilo litafanyiwa kazi kwa ufasaha.

Tangu kuanza kwa mgogoro huo wenyeviti wa mikoa mbalimbali nchini wameingia katika mvutano mkali na watendaji wa mikoa na wilaya huku wengine wakitishia kujiuzulu nyadhifa zao.

Juzi wenyeviti wa serikali za mitaa wa Mkoa wa Dar es Salaam zaidi ya 500 walitoa tamko la kutishia  kuachia nyadhifa zao pamoja na kwenda mahamakani kuomba tafsiri ya kisheria kuhusu viongozi hao kumiliki mihuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles