26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

CCM YATIA MKONO SAKATA LA NJAA

*Zitto atishia kujiuzulu ubunge akionyeshwa tani milioni 1.5 za chakula

Na ASHA BANI – Dar es Salaam


 

Pg 2CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeunga mkono kauli ya Serikali kuwa nchi haina njaa, huku kikiwaonya wanasiasa kuacha kuichonganisha dola na wananchi wake.

Kimesema kama kuna njaa, anayeruhusiwa kutangaza ni Rais Dk. John Magufuli na si vinginevyo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, alisema ameshangazwa na wanasiasa kulivalia njuga suala la njaa bila kujua ukweli wa jambo hilo.

“Baa la njaa kuwapo duniani kote ni lazima, ni utaratibu unaofahamika mana si kitu kidogo, mwenye dhamana ya kutoa matangazo hayo kwa umma ni mkuu wa nchi ndugu zangu,’’ alisema Polepole.

Pamoja na angalizo hilo, Polepole alikiri kuwa baadhi ya maeneo yanakabiliwa na tatizo la ukame, hali iliyosababisha kuwapo upungufu wa chakula.

Alisema yeye anafikiria kutokana na baadhi ya maeneo kukumbwa na ukame, kila kiongozi bila kujali itikadi za vyama vyao, wanatakiwa kuhamasisha wafuasi wao kufanya kazi kwa bidii.

Alisema viongozi wanatakiwa kuungana kuwahimiza Watanzania kuhifadhi chakula na kuacha kukitumia kutengeneza pombe za kienyeji.

Polepole alisema hadi sasa Serikali ina akiba ya tani milioni 1.5 za chakula na zipo tayari kupelekwa maeneo ambayo yana uhaba.

“Serikali ina akiba ya tani milioni 1.5 mwaka huu, miaka ya nyuma kulikuwa na akiba ya tani milioni 3  za ziada… kwa msingi huo utaona kiasi hiki kinatosheleza mahitaji.

“Tunashangaa yupo mtu hana mamlaka yeyote serikalini, wala hana uwezo wa kupata taarifa zilizo sahihi, anadiriki kuzungumzia masuala ya njaa, huyu hatutashughulika naye,” alisema.

Alisema umefika wakati sasa viongozi wa siasa kuacha kutumia misingi ya matatizo ya watu kuwa mtaji wa kisiasa.

Akitoa mfano, alisena Mkoa wa Kagera ulikumbwa na tatizo kubwa la tetemeko la ardhi mwaka jana, wanasiasa walitumia mwanya huo kuingiza siasa na kupotosha baadhi ya mambo.

Katika hatua nyingine, Polepole alimpongeza Rais Magufuli kwa hatua yake ya kurudisha heshima ya nchi, ikiwa ni pamoja na kudhibiti rushwa na kuongeza makusanyo ya mapato.

 

ZITTO

Naye Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameandika kwenye ukurasa wake wa Tweeter na Facebook, kuwa kama Serikali ya CCM ikimwonyesha tani milioni 1.5 za chakula ambazo inataka kusambaza, atajiuzulu ubunge wake mara moja.

“Narudia tena, mpaka Oktoba 2016 kulikuwa na nafaka tani 90,400 tu kwenye maghala yote ya chakula ya NFRA.

“Tunashukuru hivi sasa ajenda ya tishio la njaa inapata majawabu na matamko, ndiyo wajibu wa vyama vya siasa kuibua masuala muhimu kwa nchi yetu,” alieleza Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles