Serikali kuzifikiria Simba na Yanga

0
779

_dsc0239-1

Na WINFRIDA NGONYANI-DAR ES SALAAM

SERIKALI huenda ikazifikiria klabu za Simba na Yanga, baada ya jana kukutana na viongozi wa klabu hizo kujadili hatua yake ya kuzipiga marufuku klabu hizo kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Taarifa za uhakika zilizoifikia MTANZANIA jana, zilisema kuwa viongozi hao walikutana na kufanya kikao kirefu kwenye moja ya ukumbi za uwanja huo kujadili hatua hiyo.

Chanzo hicho kilisema kuwa, klabu ya Simba ambayo iliahidi kulipa gharama zote za uharibifu uliotokana na vurugu zilizofanywa na mashabiki wake, itawasilisha barua yao kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF), ambao wataiwasilisha serikalini.

“Tumejadiliana kwa kina na kufikia maamuzi kadhaa, Simba wao wamesema watalipia uharibifu wote, sasa tunasubiri kama ni kweli au maneno tu…na kama watafanya walivyoagizwa, basi Serikali itawafikiria,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.

Akizungumzia upande wa Yanga, alisema klabu hiyo pia italipia gharama zitakazowahusu na kuongeza kuwa, hasara iliyotokana na vurugu hizo itatangazwa hivi karibuni.

Juzi Serikali ilitangaza kuzifungia kwa muda usiojulikana klabu za Simba na Yanga, kufuatia mashabiki kufanya uharibifu mkubwa wa miundombinu ya uwanja huo kwa kung’oa viti zaidi ya 1781 na kuharibu mageti manne ya kuingilia uwanjani hapo.

Katika hatua nyingine, uongozi wa  klabu ya Yanga, umesema hatua hiyo ya Serikali  imeigharimu klabu hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit, alisema kufuatia hatua hiyo, uongozi wa klabu hiyo utakutana na kutoa maamuzi.

“Tumesikitishwa na hatua hii, tutakaa kama uongozi wakati wowote kuanzia sasa na tutatoa taarifa juu ya suala hili haraka iwezekanavyo, kwani hatua hii imeigharimu klabu yetu,” alisema Deusdedit.

Katibu huyo alilaani kitendo cha mashabiki kufanya vurugu hizo na kudai kuwa, hiyo ilikuwa si njia sahihi ya wao kuwasilisha malalamiko yao.

Akizungumzia vurugu ziliziofanywa na mashabiki baada ya mfumo wa tiketi za kielektroniki kushindwa kufanya kazi, Deusdedit alisema vurugu hizo zilitokana na mashabiki kutokuwa na elimu ya  kutosha juu ya mfumo huo mpya.

Katibu huyo pia alisema wakati umefika sasa kwa klabu kuwa na wasimamizi wa mashabiki wakati wa mechi, ili kuepusha vurugu zinazoweza kuzuilika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here