Bob Bradley kocha mpya Swansea

0
837
Bob Bradley
Bob Bradley
Bob Bradley

LONDON, ENGLAND

KLABU ya Swansea City imemteua Bob Bradley kuwa kocha mpya wa timu hiyo baada ya kuachana na  kocha, Francesco Guidolin, kutokana na mwelekeo mbaya wa  michezo ya Ligi Kuu England.

Bradley anakuwa kocha wa kwanza kutoka Marekani kufundisha Ligi Kuu England, baada ya klabu  hiyo kuachana na mpango wake wa  kumuajiri Ryan Giggs ambaye  awali alikaribia kujiunga na klabu hiyo.

Bradley alipendekezwa  na wamiliki wa klabu hiyo raia wa Marekani,  Steve Kaplan na  Jason Levien na kufanikiwa kutia saini ya  mkataba wa miaka miwili na nusu ya kuifundisha timu hiyo.

Kitendo hicho ni  pigo kwa kocha Giggs aliyekosa kibarua hicho kwa madai ya  kukosa uzoefu wa kufundisha timu kubwa.

Msimu huu  Swansea wamefanikiwa kupata pointi nne katika michezo saba waliyocheza,  huku wakicheza chini ya kiwango.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Huw Jenkins, alisema klabu hiyo iliumizwa kutokana na kushindwa kwa kocha huyo wa zamani wa timu hiyo.

“Guidolin ni kocha mzuri kutokana na mafanikio aliyoyapata msimu uliopita licha ya kutokuwa  katika  kiwango bora, tulitakiwa kufanya mabadiliko chanya kwa maendeleo ya klabu.

“Tunapenda kumshukuru kwa mafanikio aliyoipa timu yetu na wafanyakazi wa klabu kwa mchango wake na tunamtakia mafanikio mema,” alisema.

Akimzungumzia Bradley, alisema uzoefu wa kocha huyo utaipa mafanikio zaidi klabu hiyo.

“Falsafa yake inafaa na itatufanya tuwe imara na kuwa na ushindani katika michezo ya Ligi Kuu England.

“Si kazi rahisi kubadili kocha kila wakati,  lakini tunaangalia maisha ya baadaye ya klabu  na mafanikio,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here