32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, February 5, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali kuwasilisha bungeni mabadiliko ya Sheria ya Vyombo vya Habari

*TEF yasema kuna dalili njema

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imesema inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya Sheria zinazohusu Vyombo vya Habari nchini ili wabunge wakiridhia utekelezaji wake ufanyike huku ikihimiza kuwa dhamira yake katika tasnia hiyo ni njema.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne Desemba 6, 2022 na Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akifungua mkutano wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini(UTPC) uliofanyika katika Ukumbi wa Kisenga jijini Dar es Salaam.

Amesema anatambua kuwa katika tasnia ya habari kuna changamoto na moja ya changamoto ni kuhusu sheria zinazohusu vyombo vya habari ambazo amesema kuwa zinahitaji kurekebishwa na kwamba wamekamilisha majadiliano ngazi ya wadau.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

“Niwahakikishie kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kutengeneza mazingira wezeshi kwa vyombo vya habari kufanya kazi bila bughudha yoyote. Tayari Mheshimiwa Rais ameshamuagiza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kukutana na wadau wa sekta ya habari na kujadili namna ya kuziboresha sheria ambazo siyo rafiki kwa tasnia ya habari.

“Moja ya sheria hizo ni ile ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016 ambapo tayari vikao kadhaa kati ya serikali na wadau vimefanyika na UTPC inashiriki kikamilifu.

“Ninayo furaha kuwajulisha kuwa tumekamilisha majadiliano ngazi ya wadau na mara ya mwisho Waziri Nape mwenyewe alikutana na wadau na kushauriana maeneo ambayo yatafanyiwa marekebisho baada ya majadiliano ya kina ya kupitia kifungu kwa kifungu na kukubalina katika maeneo yote yaliyokuwa yanalalikiwa.

“Kwa sasa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inajiandaa kuwasilisha bungeni mabadiliko ya sheria hii ili wabunge wakiridhia tuendelee na utekelezaji wake,” amesema Msigwa.

Amesema serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wa habari nchini katika kukabili changamoto zilizopo.

“Niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wa habari katika kuhakikisha changamoto zote zinazowakabili waandishi wa habari zikiwamo kutatua sheria zisizo rafiki zinafanyiwa kazi na kuwa na sheria zinazotokana na pande mbili kukubaliana yaani serikali na wadau,” amesema Msigwa.

TEF yasema kuna dalili njema

Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF), Deodatus Balile amekiri kuwa ni kweli ndiyo hatua waliyokubaliana katika mkutano wa mwisho huku akisema kuwa ni imani yao kuwa waliyokubalina yatakuwemo.

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deodatus Balile.

“Ni kweli kabisa alichokisema Msemaji Mkuu wa Serikali (Gerson Msigwa), kwani katika kikao cha mwisho tulikubaliana kwamba mapendekezo hayo yapelekwe kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili yaandikwe kwenye msingi wa kisheria kisha yapelekwe bungeni.

“Ni imani yetu kwamba yale yote tuliyopendekeza yatakuwemo kwa ajili ya ustawi wa tasnia ya habari, hivyo tunaona dalili njema za kulifanikisha hili,” amesema Balile.

Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa ratiba, bunge lijalo litakuwa Januari 31, 2023 ambalo ndilo linatarwajiwa kupokea mapendekezo hayo.

Mchakato wa mabadiliko ya sheria zinazominya uhuru wa habari nchini, ulishika kasi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza serikali na wadau kukaa pamoja na kuangalia namna ya kumaliza kero hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles