30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali kununua mashine nane kukabili dengue

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto imeagiza mashine nane za kupulizia dawa za kuulia mbu kujikinga na ugonjwa wa dengue huku ikisisitiza kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa ebola.

Pia imewataka waganga wakuu wa mikoa wachukue hatua za kuzuia mbu ambao huambukiza ugonjwa wa dengue.

Hayo yalielezwa jana jijini hapa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati akifungua mkutano wa viongozi wa hospitali za rufaa za mikoa.

“Ninachotaka kusisitiza kwa waganga wakuu, najua wenzetu katika wilaya na halmashauri wanaweza wasituelewe, lakini lazima tuchukue hatua za kudhibiti mbu, hakuna maajabu mengine ambayo tutayafanya zaidi ya kudhibiti mbu.

“Kwa hiyo zile lita chache tunazowapa za dawa kuna wengine wanaona muda unaenda wanaenda katika mito wanazimwaga, hapana, lazima tukafanye kazi ya kunyunyuzia katika mazalia ya mbu,” alisema Ummy.

Alisema mashine hizo zitasambazwa katika baadhi ya mikoa ambayo ina mazalia na kuwataka waganga wakuu kuwabana wakurugenzi watenge bajeti kwa dawa hizo.

“Kipekee nimpokeze Mganga Mkuu wa Dar es Salaam amepambana sana na bahati nzuri Katibu Tawala wake amemshika vizuri, nasema kwamba ukipewa majukumu lazima ufanye kazi.

“Tanga sijaona jitihada zozote kukabiliana na dengue, nasema kweli kwa sababu mimi natoka Tanga ila watu wanaumwa, Pwani angalau kidogo,” alisema.

Kuhusu ugonjwa wa ebola, alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kukabiliana nao kama utatokea huku akiupongeza Mkoa wa Mwanza kwa jinsi ulivyojiandaa kuukabili.

“Ebola bado ni tishio nchini, nilitoa taarifa kwa umma, lakini hakuna ‘case’ mpya zaidi ya zile zilizotokea. Habari mbaya ni kwamba WHO wamesitisha huduma DRC kwa sababu gari la watumishi limechomwa moto kule.

“Ina maana itazidi, kwa hiyo tuendelee kuchukua hatua Mwanza, Kigoma, Rukwa Songwe na Dar es Salaam, ila kipekee nimpongeze Mganga Mkuu wa Mwanza amefanya kazi nzuri kama mgonjwa atatokea jinsi ya kumhudumia,” alisema.

Ummy alisema wameagiza mashine 70 za X-ray ambazo zitafungwa katika hospitali za rufaa za mikoa pamoja na mnashine 20 za X-ray za meno ambazo nazo zitafungwa katika hospital hizo.

“Katika ripoti zenu (waganga wakuu) hakikisheni mnaandika mnataka vifaa vipi, hii itatusaidia sisi, lakini andaeni taarifa kwa wakati,” alisema.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alisema hospitali za rufaa za mikoa zina wajibu wa kuendelea kuboresha huduma zake zikiwemo za afya kwa kusimamia ubora.

Pia aliwataka waganga wakuu wa mikoa kushughulikia malalamiko ambayo yamekuwa yakitolewa na wagonjwa kwani yamekuwa mengi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Zainabu Chaula, alisema watumishi wa wizara hiyo wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi, lakini Serikali imejitahidi kuziondoa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,195FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles