24.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Serikali kufanyia maboresho sera ya ubunifu

Christina Gauluhanga Na Tunu Nasssor -Dar es salaam

SERIKALI imesema ipo hatua za mwisho kufanyia maboresho sera inayoongoza sekta ya ubunifu nchini ili iendane na kasi ya teknolojia ya sasa.

Akizungumza jana Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Ubunifu, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wilium ole Nasha alisema sera hiyo imekuwa ya muda mrefu, haiendani na mazingira ya sasa ya ukuaji wa teknolojia.

“Tupo katika hatua za mwisho kuihuisha sera iliyopo ili masuala ya ubunifu yaweze kupata nafasi zaidi kwakuwa awali ilitambua zaidi teknolojia huku ikiweka kando ubunifu,” alisema Ole Nasha.

Alisema kwa sasa Tanzania imepanda katika mizania ya ubunifu kutoka nafasi ya 123 na kushika namba 97 huku ikiongoza Afrika kwa ubunifu.

Ole Nasha alisema kwa sasa wamedhamiria kuwashirikisha wabunifu kutoka kona mbalimbali za nchi huku wakitambua wale wa vijijini ambako ndiko kuna changamoto nyingi.

“Miradi mingi ya ubunifu huibuliwa kwenye maeneo yenye changamoto hizo, hivyo kwa vijijini tumebaini kuna bunifu nyingi ambazo zinatakiwa kuendelezwa,” alisema Ole Nasha.

Alisema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha bunifu hizo zinasonga mbele ili zisiishie kwenye wazo, ziwe hadi bidhaa.

Ole Nasha alisema hali hiyo imesababisha kuanzisha mashindano ya kutafuta wabunifu ambapo watazunguka nchi nzima hadi vijijini kupata washiriki ambao wameanzisha ubunifu, lakini unahitaji kuendelezwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk. Amos Nungu alisema ni mwaka wa sita sasa wamekuwa wakikutanisha wabunifu na kuonyesha kazi zao.

Alisema lengo la wiki hiyo ni kusaidia wabunifu kutangaza kazi zao na kuzimalizia ili zisiishie kwa wazo.

Dk. Nungu alisema wiki ijayo watawakutanisha wabunifu hao mkoani Dodoma ambapo lengo kuu ni kuwajenga vijana wa kitanzania wafikiri kwa kina na kubuni wazo lenye kujenga manufaa kwa jamii.

Aliziomba sekta binafsi kushirikiana na wadau kuangalia miradi ya ubunifu inayoweza kuendelezwa na kupata bidhaa ambayo italeta suluhisho la changamoto katika jamii.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,538FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles