24.6 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Panya wa Sua wafundishwa kukabili majanga

CHRISTINA GAULUHANGA Na TUNU NASSOR – DAR ES SALAAM

TAASISI isiyo ya kibiashara ya Apopo – Sua imeanza utafiti kumfundisha panya kubeba kifaa maalumu kitakachosaidia kuokoa maisha ya binadamu katika majanga mbalimbali ikiwamo tetemeko la ardhi.

Akizungumza na MTANZANIA katika maonyesho ya Wiki ya Ubunifu yanayoendelea Dar es Salaam katika Kijiji cha Makumbusho, mwendesha mafunzo wa panya hao kutoka tawi la taasisi hiyo lililopo chini ya Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Said Mshana, alisema kifaa hicho kitakuwa na kamera, kifaa cha kunasa sauti na kadi yenye uwezo wa kurekodi matukio.

Alisema panya huyo ana uwezo wa kutembea umbali wa kilometa 50 wa eneo la tukio kunusa na kubaini endapo kuna binadamu amekandamizwa na kifusi, kusikiliza kelele za waombaji msaada au kunusa kama kuna mabomu.

“Tunaendelea kufanya maboresho kwa sasa ili panya huyu aweze kubebeka kirahisi na kukusanya taarifa zilizo katika eneo la tukio na kuzihifadhi kwenye kadi maalumu ambayo inatuma taarifa kwenye kompyuta na ina uwezo wa kuchomolewa na kuhamisha taarifa hizo,” alisema Mshana.

Alisema kwa sasa wanaendelea na maboresho ya hatua za mwisho ili panya huyo aweze kufanya kazi kwa kiwango kikubwa na haraka zaidi.

Pia mwalimu wa panya kutoka taasisi hiyo, Pius Mhapuly alisema panya buku ‘ Herorats – panya mashujaa’ wamekuwa na uwezo mkubwa wa kubaini vimelea vya kifua kikuu kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi hayo hapa nchini.

Alisema panya hao ambao kwa Dar es Salaam wapo tisa na Morogoro 100, wamefundishwa  kutambua vimelea hivyo kwa njia ya kunusa.

Mhapuly alisema katika kubaini ugonjwa huo, hutumia sampuli ya makohozi ambayo panya huyo hunusa na endapo kuna ugonjwa huendelea kuchimba chini au kukaa kwa dakika tatu hadi tano.

“Panya huyu ameleta matokeo makubwa katika kubaini vimelea hivi kwakuwa endapo makohozi hayo hayana dalili zozote za ugonjwa huyo, hupita haraka na kuondoka zake na ukiona amesita kwa dakika kadhaa ujue tayari mgonjwa amepata maambukizi hayo,” alisema Mhapuly.

Alisema sampuli za kupima huzipata katika vituo mbalimbali vya afya ambapo wafanyakazi wao hupita na kuzikusanya.

Mhapuly alisema kwa siku wamekuwa wakifanya uchunguzi wa makohozi ya wagonjwa watano hadi kumi kwa tawi la Temeke, Dar es Salaam.

“Inategemea na sampuli za wiki hiyo ambapo tukiwa na sampuli 400 au 200 tunaweza kupata wagonjwa 10 hadi 15 wenye vimelea vya kifua kikuu – TB,” alisema Mhapuly.

Alisema panya hao wamekuwa wakifundishwa mafunzo kwa muda wa miezi tisa ndio aweze kufanya kazi hiyo kwa umakini.

Mhapuly alisema tafiti za panya hao zilianza mwaka 1997 ambao kwa majaribio ya awali walipelekwa panya nane nchini Ubelgiji na walirejea sita baada ya wawili kufariki kwa sababu ya hali ya hewa.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,538FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles