23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Serikali kudhibiti mipaka 53 isiyo rasmi

Na MWANDISHI WETU- KIGOMA

WIZARA ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na wizara nyingine zitadhibiti mipaka isiyo rasmi 53 katika mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa ili kukabiliana na changamoto ya uingizaji holela wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini Kigoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Riziki Shemdoe wakati wa hafla ya uzinduzi wa ofisi ya Shirika la Viwango (TBS) Kanda ya Magharibi itakayohudumia mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa.

Alisema kwa sasa TBS ishirikiane na taasisi nyingine za Serikali katika kushughulikia suala hilo wakati wizara ikiendelea na taratibu za kulipatia ufumbuzi.

Profesa  Shemdoe alitoa ahadi hiyo kutokana na taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS,  Dk. Athuman Ngenya ambaye pamoja na mambo mengine alieleza uwepo wa mipaka isiyo rasmi ambayo inakwamisha juhudi za shirika za kudhibiti  uingizwaji wa bidhaa hafifu katika soko la Tanzania.

Katika taarifa hiyo, Dk. Ngenya alisema kuwa kati ya mipaka hiyo 53, Mkoa wa Rukwa unaongoza kwa kuwa na mipaka isiyo rasmi 35 ikifuatiwa na Kigoma 14  na Katavi minne.

Profesa Shemdoe alisema suala la mipaka ni mtambuka, hivyo atawasiliana na wizara nyingine ili kupata ufumbuzi wa suala hili kwani uwepo wa mipaka isiyo rasmi pia nchi inapoteza mapato.

Aliushukuru uongozi wa Mkoa wa Kigoma kwa ushirikiano wanaoutoa kwa taasisi zilizopo mkoani hapa na amezitaka pia taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kushirikiana na uongozi wa mkoa ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi.

“Ni imani yangu  kuwa kufunguliwa  kwa  ofisi ya TBS mkoani Kigoma itakuwa ni chachu ya maendeleo kwa mikoa ya Kanda ya Magharibi,” alisema Profesa Shemdoe.

Uzinduzi wa ofisi ya Kanda ya  Magharibi unafanya TBS kuwa na ofisi za kanda sita zikiwemo za Kanda ya Ziwa (Mwanza, Kagera, Shinyanga, Geita na Simiyu), Kaskazini (Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga), Kati (Dodoma, Singida na Tabora) na Ķusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma).

Pia ofisi za Makao makuu  Dar es Salaam zinafanya  kazi katika mikoa iliyopo  mashariki mwa nchi yaani Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,460FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles