Na MWANDISHI WETU -IRINGA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki amevutiwa na uzalishaji wa chakula cha kuku, ufugaji wa kuku pamoja na mbogamboga katika Kongani ya Ihemi kwenye ushoroba wa Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) na kusema kuwa uwekezaji huo unakwenda sambamba na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2015.
Hayo aliyasema jana mjini hapa baada ya kutembelea kwa nyakati tofauti viwanda vya Silverlands, Masifio Estates, Pyrethrum Tanzania (PCT), Qwihaya General Entreprises na Sao Hill.
Kairuki alisema kuwa uwekezaji wa kuku na kilimo cha mbogamboga katika eneo hilo una mchango mkubwa katika kuongeza kipato kwa wakazi wa Iringa.
“Nimevutiwa sana na uwekezaji huu wa kiwanda cha kutengeza chakula cha kuku, ufugaji wa kuku na kilimo cha mbogamboga. Kama Serikali tutaendelea kuboresha na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini.
“Hii siyo hadithi, nimejionea mwenyewe namna uzalishaji mkubwa wa kuku na mbogamboga unavyofanyika, na sisi kama Serikali tutahakikisha tunawaunga mkono ili kujenga na kuimarisha sekta husika pamoja kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi hapa nchini,” alisema Kairuki.
Alisema kiwanda cha Silverlands kimekuwa chachu ya maendeleo kwa upande wa kuku, lakini pia wamekuwa wanunuzi wakubwa wa zao la mahindi kutoka kwa wakulima wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na hivyo kuliongezea thamani zao hilo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema kuwa kiwanda cha Silverlands kimekuwa na mchango mkubwa na kuhakikisha maendeleo ya mkoa huo kwa kuwahakikishia wakulima soko la uhakika la mazao ya mahindi na soya.