Msoto miaka tisa wampa ubilionea

0
590

Na JANETH MUSHI -MIRERANI

MCHIMBAJI mdogo wa Tanzanite, Saniniu Laizer (52), sasa ni bilionea mpya mjini hapa baada ya kusota kwa miaka tisa akichimba madini hayo na kufanikiwa kupata mawe mawili, moja likiwa na kilo tisa ambalo limevunja rekodi ya dunia kwa ukubwa.

Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, jiwe kubwa zaidi la Tanzanite lilikuwa na kilo 3.38 na lilichimbwa mwaka 2005.

Sasa Laizer anaweka historia mpya ya madini hayo ambayo yanapatikana eneo la Mirerani pekee wilayani Simanjiro baada ya kupata mawe mawili; moja likiwa na kilo tano na jingine tisa.

Kutokana na unyeti wa suala hilo, Waziri wa Madini, Doto Biteko, jana alisema Rais Dk. John Magufuli ameamua mawe yote hayo yanunuliwe na Serikali na yatahifadhiwa kama hazina ya taifa.

Mbali na Biteko, tukio hilo lilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga, watendaji wengine pamoja na wawakilishi wa wachimbaji wa madini nchini.

WAZIRI BITEKO

Biteko akizungumza kabla ya kumkabidhi Laizer mfano wa hundi ya thamani ya Sh bilioni 7.44, alimpongeza kwa kukubali kuwa mzalendo na kuuza serikalini madini hayo kwa kuwa huo ni ushahidi kuwa hata wachimbaji wadogo wanaweza.

Alisema mara baada ya madini hayo kupatikana Rais Dk. Magufuli, aliagiza Serikali kuyanunua ili yawekwe kwenye makumbusho ili kuidhihirisha dunia kuwa Tanzania ndiyo kitovu cha madini hayo badala ya kuuzia nchi zingine wakapate sifa wao.

Biteko alisema wakati ukuta wa kuzunguka machimbo hayo ukijengwa, maneno mengi yalisemwa ila kupitia Laizer imedhihirika wachimbaji wadogo wanaweza kuleta mabadiliko katika sekta hiyo muhimu.

“Kwa namna ya pekee niwashukuru wachimbaji wadogo kwani mengi yalisemwa na kuwatisha kuwa nyie hamuwezi kuzalisha kwamba hamna mitaji na teknolojia, tukio la leo ni kielelezo wachimbaji wadogo wanaweza.

“Watanzania tunaweza kufanya mabadiliko ndio, japo tunahitaji wageni, ila tusikubali, tusimame imara sisi tunaweza kubadilisha nchi yetu, walikuwa wakiwatisha na kudharau wachimbaji wadogo hawawezi kuchimba mita 1,000 ila tukio la Laizer limekuwa ni kielelezo kuwa wachimbaji wadogo wanaweza kwani Laizer amechimba mita 1,800,” alisema Biteko.

Alitolea mfano wakati wa mabadiliko ya sheria, walitishiwa na wengine wakafanya sanaa kuwa wachimbaji wakubwa wanaondoka, hivyo sekta hiyo haitaendelea.

“Wakafunga wamerudi wenyewe wakasema tuzungumze, tunamshukuru sana Profesa Kabudi na wengine waliofanikisha hili, tumefanikiwa sana, nikitolea mfano katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 walikadiria kukusanya Sh bilioni 470.2 ila wamevuka lengo na kukusanya zaidi ya Sh bilioni 526 huku kiwango kikubwa kikiwa ni kutoka kwa wachimbaji wadogo.

“Leo Laizer ametukusanya na kuvunja rekodi, tuwalee wachimbaji wadogo. Watendaji wadogo tuwasikilize na kuwahudumia wachimbaji wadogo,” alisema Biteko.

Alisema Rais Dk. Magufuli aliwaagiza kuhakikisha mchimbaji huyo hadhulumiwi fedha zake na kuelekeza Serikali tununue madini haya.

“Rais alisema tusiponunua Serikali wageni watayanunua kama vile China na tutaenda nchini kwao kuyaangalia, alisema mchimbaji asidhulumiwe na alipwe fedha zake zote na ndiyo maana ya kuwapo Naibu Waziri wa Fedha na Gavana na wengine wote, ameelekeza yanunuliwe na kuwekwa katika makumbusho yetu,” alisema Biteko.

Aidha aliwapongeza wachimbaji wadogo kote nchini kwa kuhama kutoka kutorosha madini na badala yake wamekuwa wakitoa taarifa kwa baadhi ya wenzao wanaotorosha madini na kuwa kwa sasa wanalipa kodi na kukuza sekta hiyo.

MAOMBI KITALU C

Aidha kuhusu maombi ya wachimbaji wadogo ya kuomba kupewa kitalu C, kilichokuwa kinamilikiwa na mwekezaji Tanzanite One kwa ubia wa Serikali, Biteko alisema Serikali inafanyia kazi na  inaweka utaratibu ambao utawanufaisha wachimbaji wadogo.

Aidha aliwataka wachimbaji hao kutokuvamia kitalu hicho na kuagiza uongozi wa mkoa kukilinda ambapo kwa sasa ni mali ya Serikali.

“Tunafanyia kazi ombi hili ila kati ya mikoa yenye maneno mengi katika sekta ya madini ni huu, kuna mafundi wa kusema na wengi wao sio wachimbaji, hivyo msidanganywe na mtu na kufanya mambo kinyume na sheria, mbaki na siasa zenu,” aliongeza Biteko.

“Mnatamani kuchimba kitalu C, lakini mko tayari kulinda rasilimali badala ya kuzua maneno, kuheshimu sheria? Kama mko tayari, Serikali inaweka utaratibu mzuri kwani Rais anataka uchumi wa madini ukue katika sehemu yake.

“Kitalu C kisivamiwe, ni mali ya Serikali na mkivamia mkakutana na chamoto msinipigie simu,” alisema Biteko.

JPM AMPONGEZA

Aidha wakati hafla hiyo ikiendelea, Rais Magufuli alimpigia simu Biteko na akazungumza na mchimbaji huyo pamoja na wadau wengine waliokuwa wamehudhuria.

“Nampongeza raia huyo na hii ndiyo faida ya wachimbaji wadogo kwani inadhihirisha kwamba Tanzania sisi ni matajiri, nawapongeza wote na namshukuru Gavana na Serikali kwa ujumla kwa kuamua kununua madini hayo, nilikuwa naangalia hapa nimefurahi sana,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Nyongo alimpongeza mchimbaji huyo kwa kuwa mwaminifu na kuwa katika kipindi cha mwaka 2019/20 amefanikiwa kupata madini ya Tanzanite yenye uzito wa kilo 108 na Serikali ikapata mrabaha wa Sh milioni 638.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Kijaji alisema Serikali imenunua madini hayo na kuwa mchimbaji huyo amekabidhiwa fedha zake zote.

“Wapo waliokuwa wanabeza ukuta huu kwani hatujajua kabla ya ukuta huu mangapi kama haya yameibiwa, Sh bilioni 8 ni kitu gani, tumekuja na mlipaji mkuu wa Serikali, na hizi siyo pesa za kukopa, ni fedha za Watanzania,” alisema Dk. Kijaji.

Awali Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Msanjila alisema madini yenye uzito huo hayajawahi kupatikana katika eneo hilo ambalo ndilo eneo pekee ambalo madini hayo yanapatikana duniani.

MBUNGE AWAOMBEA WACHIMBAJI WADOGO KITALU C

Awali aliyekuwa mbunge wa Simanjiro, James ole Millya aliiomba Serikali iwape Watanzania ambao ni wachimbaji wadogo kitalu C kwa sababu kupitia Laizer wamedhihirsha uwezo wanao wa kuchimba.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mhandisi Zephania Chaula, alisema kupatikana kwa madini hayo yenye uzito mkubwa ni matunda ya ujenzi wa ukuta katika eneo hilo, ambao umesaidia madini yasitoroshwe na kuwa hawaangalii cheo cha mtu katika kuhakikisha madini hayatotoshwi.

“JWTZ msione huruma katika hili na tunapongeza kwani kutoka kilo 300 za madini ya Tanzanite kwa mwaka yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 4 ila kwa sasa yanafika kilo 4,000 kwa mwaka yakiwa na thamani ya Sh bilioni 50, ndoto ya Rais ya kulinda rasilimali zinufaishe Watanzania zinatimia,” alisema Chaula.

MIPANGO YA LAIZER

Akizungumza katika hafla hiyo Laizer aliishukuru Serikali kwa kununua madini hayo na kuwa atatumia fedha hizo katika uwekezaji wa miradi mbalimbali hapa nchini pamoja na kusaidia miradi mbalimbali ya jamii ikiwemo elimu.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here