28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

SENETA AMLAUMU KENYATTA KUPAISHA UMAARUFU WA JOHO

MOMBASA, KENYA


SENETA wa Mombasa, Hassan Omar, amemshutumu Rais, Uhuru Kenyatta, kwa kupaisha umaarufu wa Gavana wa kaunti hiyo, Hassan Joho.

Akizungumza na wakazi wa Changamwe kauntini hapa juzi, Omar ambaye anagombea ugavana wa Mombasa alimtaka Rais Uhuru akome kuingilia siasa za Mombasa na kwamba yeye angependa kuona akikabana koo na Joho katika kinyang’anyiro cha ugavana wa kaunti hiyo.

 “Ninamtaka yule jamaa aliyepata ‘D’- awe kwenye karatasi ya kura. Nitamshinda kwa sababu hajawafanyia chochote wakazi wa Mombasa,” alisema.

Kauli zake zimechochewa na masahibu ambayo yamekuwa yakimkumba Joho kutoka kwa utawala wa Serikali ya Jubilee, ambayo yalizidi kushamiri mwezi uliopita.

Umaarufu wa gavana huyo umeenea kitaifa kutokana na jinsi ambavyo amekuwa akipokewa katika maeneo tofautitofauti nchini tangu wiki iliyopita.

Joho amekuwa akigonga vichwa vya habari kutokana na jinsi anavyoandamwa kuanzia kuhusu biashara zake hadi matokeo yake ya Mtihani wa Taifa wa Sekondari (KCSE), ambao anadaiwa alifeli lakini akaghushi cheti kumwezesha kuingia chuo kikuu.

Naibu Kiongozi huyo wa Chama cha ODM amekuwa akidai masahibu yanayomwandama yametokana na ukosoaji wake dhidi ya serikali na kwamba Jubilee inatafuta sababu ya kumzuia asigombee ugavana katika uchaguzi mkuu wa Agosti.

Hata hivyo, Omar alisema gavana huyo hapaswi kuzuiwa kugombea wadhifa huo hata kama alishindwa  katika mtihani wa KCSE.

Kwa mujibu wa Omar, Joho kwa sasa anatumia masahibu yake ili wakazi wa Mombasa wamhurumie na kumchagua tena licha ya kuwa hajawatumikia ipasavyo.

“Hakuna kitu kama kura za huruma. Kama huonei huruma wakazi wa Mombasa, huruma usiitarajie kutoka kwao hapo Agosti 8,” alisema katibu huyo mkuu wa chama cha Wiper.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles