24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

SARATANI YAONGEZEKA MARADUFU KWA WANAWAKE KULIKO WANAUME

NA JOSEPH HIZA,

STAILI mbovu za maisha zinapaisha viwango vya saratani mbalimbali mara sita kwa kasi miongoni mwa wanawake kuliko wanaume, ripoti mpya ya utafiti nchini Uingereza imeonya.

Unene, uvutaji wa sigara, kutojishughulisha na unywaji wa pombe umeelezwa kuwa kisababishi kikuu cha ongezeko hilo.

Visababishi hivyo kwa sasa vinatarajia kupaisha kesi za maradhi ya saratani za matiti, kizazi, ini na mapafu kwa kipindi cha miaka 20 ijayo. 

Utafiti huo ulioendeshwa na taasisi ya Utafiti wa Maradhi ya Saratani Uingereza (CRUK) unakadiria kuwa kesi za maradhi ya saratani zimeongezeka kwa asilimia 3.2 miongoni mwa wanawake hadi mwaka 2035, ukilinganisha na asilimia 0.5 tu miongoni mwa wanaume.

Huko nyuma, maradhi ya saratani yalikuwa yakiwakumba zaidi wanaume.

Lakini pengo la jinsia limeanza kukaribiana huku takwimu zikionesha wanawake milioni 4.5 na wanaume milioni 4.8 waligundulika na maradhi hayo kati ya mwaka 2014 na 2015.

Sababu mojawapo ni kuwa wanawake wengi zaidi huvuta sigara na kunywa pombe kuliko ilivyowahi kutokea huko nyuma na hivyo kuongeza hatari ya maradhi ya mapafu, ini na saratani ya mdomo.

Lakini lawama za ukuaji huo wa takwimu zinaelekezwa kwa ongezeko la kiwango cha unene miongoni mwa wanawake, ambacho kwa karibu kinahusishwa na saratani zinazowaandama wanawake. 

Hatari ya saratani za matiti, tumbo na kizazi zinaongezeka miongoni mwa wanawake wenye uzito mkubwa, ambao unadhaniwa kwa sababu unene na huathiri homoni zinazochochea tendo la ndoa kama vile oestrogen, ambazo husababisha ukuaji wa uvimbe.

Asilimia 67 ya wanaume na 57 ya wanawake nchini Uingereza ni wenye uzito mkubwa au wanene.

Hata hivyo, saratani ambazo huwaathiri wanaume pekee kama vile saratani ya tezi dume na saratani ya korodani, hazihusishwi na ongezeko la mafuta mwilini.

Utafiti uliochapishwa na Jarida la Saratani la Uingereza, (British Journal of Cancer), unakadiria kuwa kesi za saratani ya matiti zitaongezeka kwa asilimia 30 kutoka 54,000 mwaka 2014 hadi 71,000 mwaka 2035.

Idadi ya kesi za saratani ya kizazi kwa mwaka itapaa asilimia 43 hadi 10,500 kwa mwaka na ya tumbo itaongezeka asilimia 24 hadi kesi 11,500 kwa mwaka.

Kesi za saratani inayowapata wanawake ya dundumio (thyroid cancer), ambayo pia kwa karibu inahusishwa na unene, itaongezeka karibu mara mbili hadi 4,800 kwa mwaka.

Saratani ya mapafu kwa wanawake, ubashiri unaonesha itaongezeka kwa asilimia 38 hadi kesi 30,000 kwa mwaka na saratani ya ini kwa asilimia 78 kufikia kesi 3,400 kwa mwaka.

Saratani ya kizazi pia inakadiriwa kupaa ijapokuwa watafiti wanamatumaini kwamba chanjo iliyopatikana karibuni ya HPV  kwa wasichana wa shule itabadili mwelekeo.

Kiongozi wa utafiti huo, Dk. Rebecca Smittenaar anasema: “Huku kiwango cha unene kikiongezeka katika miaka ya karibuni tunaanza kuona pia saratani hizi zikiongezeka miongoni mwa wanawake.

“Ijapokuwa wastani wa viwango vya uvutaji wa sigara vinaanguka nchini Uingereza, kihistoria wanawake walijiingiza katika uvutaji sigara kwa idadi kubwa baada ya tabia hiyo kuzoeleka miongoni mwa wanaume.” 

Dk. Smittenaar anaongeza: “Bado hatujaona kilele cha kesi za saratani ya mapafu miongoni mwa wanawake, ambazo tayari zinapungua miongoni mwa wanaume.”

Wanawake walianza kuvuta sigara katika miaka ya 1950, 1960 na 1970 kwa sasa wamekutwa na saratani ya mapafu. 

Wataalamu wa afya wametoa wito kwa wanawake kuzingatia matokeo haya na kubadili staili yao ya maisha ili kupunguza hatari.

Dk. Richard Berks, wa Taasisi ya Saratani ya Matiti ya Breast Cancer Now, anasema maradhi hayo tayari ni tatizo la kiafya na litazidi kuwa kubwa.

Anaongeza: “Ubadilishaji wa staili ya maisha kama vile kulinda afya ya uzito, kufanya mazoezi ya mara kwa mara na kupunguza kiwango cha unywaji pombe kitasaidia kupunguza viwango vya saratani nyingine pia.”

Sarah Toule wa asasi ya utafiti wa saratani, World Cancer Research Fund, anasema: “Ushahidi wetu unaonesha kwamba theluthi moja ya kesi za saratani zilizozoeleka inaweza kuzuilika iwapo watu watakuwa na uzito wenye afya, mlo kamili na kujishughulisha kimwili.

Kwa saratani ya matiti, hilo linamaanisha itazuia kesi mbili kati ya tano hivi.”

Professa Kevin Fenton wa Public Health England, anasema vitu vikuu vinavyoweza kuzuia na kupunguza hatari ya saratani ni kuacha kuvuta sigara, kulinda uzito wa mwili, kujishughulisha kimwili na kuhudhuria uchunguzi wa saratani kila inapobidi.

Wataalamu wengine wanatoa wito kwa serikali kuingilia kati kwa kuwekeza utafiti na tiba zaidi. 

Katherine Taylor wa Taasisi ya Saratani ya Kizazi (OCA), anasema utabiri wa kuwapo kwa ongezeko kubwa la kesi za maradhi haya unatakiwa usitokee kweli. Takwimu hizi hazitakuwa kitu cha kuogopesha iwapo saratani ya kizazi itapewa kipaumbele inachostahili.

Naye Robert Music wa Shirika la Saratani ya Kizazi la Jo's Cervical Cancer Trust, anasema ongezeko kubwa la saratani zinazowakabili wanawake linatisha.

Ongezeko hilo linaoana na kupungua kwa idadi ya wanawake wanaojitokeza mara kwa mara kuchunguzwa seratani ya kizazi, ambayo kwa mwaka wa 19 mfululizo liko kwa kiwango cha chini England.

Sir Harpal Kumar, ambaye ni  Ofisa Mtendaji Mkuu wa Cancer Research UK anasema takwimu hizi mpya zinabainisha changamoto kubwa wanayoendelea kukabiliana nayo Uingereza na duniani kote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles