23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Samia azungumzia ukubwa tatizo la ajira

Nora Damian – Dar es Salaam

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, amesema zaidi ya watu milioni 187 duniani hawana ajira na kushauri kuwepo kwa uwiano kati ya matumizi ya nguvu kazi na teknolojia, kuhakikisha vijana wanaendelea kunufaika.

Kwa Tanzania utafiti wa nguvu kazi uliofanyika mwaka 2018 unaonyesha vijana wenye uwezo wa kufanya kazi ni milioni 15.7, lakini asilimia 9.7 hawana ajira.

Akizungumza jana wakati akifungua mkutano wa mawaziri wa sekta ya kazi na ajira katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Samia alisema ni lazima jumuiya hiyo iweke mikakati ya kupambana na changamoto ya ukosefu wa ajira.

“Teknolojia inakuwa nzuri pale inapozalisha ajira na si inapopunguza matumizi au rasilimali ya nguvu kazi, kinachohitajika ni kuhakikisha kunakuwa na uwiano kati ya matumizi ya nguvu kazi na teknolojia,” alisema Samia.

Akinukuu Ripoti ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuhusu mwenendo wa soko la ajira kwa mwaka 2020, Samia alisema vijana milioni 429 sawa na asilimia 39 ya vijana wote duniani ndio waliopo kwenye mafunzo na waliopo katika ajira ni milioni 509 sawa na asilimia 42.

Aidha alisema takribani wafanyakazi bilioni 2 sawa na asilimia 61 wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi huku zaidi ya watu milioni 267 sawa na asilimia 22 (miaka 15 hadi 24) hawapo mwenye mafunzo wala ajira.

 “Takwimu hizi zinaonyesha ukubwa wa changamoto tuliyonayo, SADC kama sehemu ya dunia, tunalazimika kuweka mikakati katika kupambana nayo.

“Mikutano mingi katika ngazi ya SADC inafanyika na mengi yanazungumzwa, inawezekana changamoto ni kushusha katika nchi zetu mojamoja, vyama vya wafanyakazi, Serikali na waajiri je, tunatatua matatizo ya wafanyakazi, tunakubaliana vipi kutengeneza ajira zenye staha kwa ajili ya vijana wetu?” alihoji.

Alisema pia zaidi ya asilimia 60 ya nguvu kazi katika jumuiya hiyo ni vijana, hivyo akashauri itumike ipasavyo kuondoa umasikini na kuimarisha uchumi wa nchi wanachama.

Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, alisema kupitia programu ya mafunzo kwa vitendo mahala pa kazi, vijana 5,967 wamepatiwa mafunzo na kati yao 3,967 wamehitimu na 1,827 wameajiriwa katika maeneo mbalimbali, hasa sekta binafsi.

Jenista alisema vijana wengine 2,000 wanaendelea na mafunzo nchi nzima kwa udhamini wa Serikali kwa kusaidiana na sekta binafsi na kati yao 600 wanatoka Dar es Salaam.

Alisema pia vijana 14,890 walio katika sekta isiyo rasmi wamepatiwa mafunzo kuhusu ujasiriamali na kurasimisha biashara zao na 9,300 walipatiwa mafunzo ya kuongeza thamani katika mazao ya kilimo na mifugo huku 13,500 wakifundishwa kuhusu uanzishwaji na uimarishaji wa kampuni.

“Baadhi ya waajiri wameamua kuifanya programu hii kuwa muhimu ndani ya maeneo yao, ombi langu watumie mwongozo wa taifa wa ‘Internship’ kuwezesha iwe endelevu katika maeneo yao ya kazi,” alisema Jenista.

Miongoni mwa masuala yatakatojadiliwa ni suala la uimarishaji wa nguvu kazi ili kuona kama kila nchi inaweza kuchukua uzoefu na kuupeleka nchi nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles