25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Freeman Mbowe azungumzia waliomzomea kwenye mkutano

Mwandishi Wetu – Hai

MWENYEKITI wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, amesema kikundi cha watu waliomzomea katika mkutano wake wa kibunge uliofanyika juzi, kiliandaliwa na kuratibiwa na viongozi wa CCM kwa nia ya kuvuruga mkutano huo.

Akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari kwenye ofisi yake wilayani Hai jana, Mbowe alisema kabla mkutano huo wa tano wa kibunge uliofanyika katika Kijiji cha Kikavu, Kata ya Machame Weruweru, walikuwa na taarifa zote kuhusu kikundi hicho.

“Mkutano ulikuwa na taarifa zote za mapema, kwamba kuna mpango unaoratibiwa na baadhi ya viongozi wa CCM na tuliripoti tukio hili polisi, kwamba kuna taarifa ya watu waliokuwa wakiletwa kutoka maeneo mengine ili kuvuruga mkutano.

“Lakini tulishangaa kuona genge hilo la vijana lilipojitokeza mbele ya Kamanda wa Polisi wa Wilaya, alionekana kuwalinda na kuwaacha wakivuruga mkutano kwa zaidi ya dakika 15, wakionekana wakipiga kelele na mayowe bila kuchukuliwa hatua yoyote,” alisema Mbowe.

Alisema mpango huo unaonekana ulikuwa wa makusudi kwa kuwa hata polisi hawakutaka kuchukua hatua yoyote kuwadhibiti vijana hao, na wao kama viongozi walilazimika kuwashauri vijana wao ambao walikuwa tayari kuulinda mkutano wasichukue hatua yoyote dhidi ya vijana wale kwa sababu hawakuzoea vurugu.

Mbowe alisema vijana hao walipelekwa eneo la mkutano huo kwa magari manne na wamewapa polisi picha zao, namba za magari hayo na wote wanajulikana kwa kuwa hata polisi wenyewe walipiga picha, hivyo wanategemea kuona polisi wakichukua hatua dhidi ya watu hao.

Alisema hakuna aliyedhurika kwa watu wa pande zote kwa kuwa watu wa Chadema hawakupambana nao kwa kuwa walifahamu kuwa jambo hilo liliratibiwa na kiongozi mmoja ambaye anawalinda wahalifu kwa sababu ametumwa.

“Wananchi wenyewe wa eneo lile wanawajua wahusika kuwa hawakutoka kabisa katika eneo lile wala katika kata ile na waliletwa kwa mabasi, baada ya kupewa pombe ili waende kuvuruga mkutano huo,” alisema Mbowe.

Baada ya tukio hilo, kwenye mitandao ya kijamii zilianza kusambaa picha zilizoonyesha watu waliovaa nguo za CCM wakidaiwa kuwa ndio waliokuwa wakifanya fujo kwenye mkutano huo.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Jimmy Prosper alisema wanatambua kuwa walipelekwa vijana hao wa kihuni kutoka Kiyungi, Bomang’ombe, Makiyusa, Mabogini ili waharibu mkutano huo.  

“Na sisi tuliwafahamu mapema ndiyo maana tulikuwa tukiwalinda, kila walipotaka kuingia eneo la mbunge tuliwarudisha nyuma, baadaye walipoona tumewadhibiti vya kutosha wakaanza kuzomea na kumtukana mbunge.

“Askari walikuwepo pale akiwemo OCD, tuliwaeleza waondoeni hawa watu sio wa eneo hili, lakini hawakufanya chochote na kwamba anasema hawezi kufanya chochote kwa sababu wote ni wananchi wake,” alisema Prosper.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles