23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Kusaya ateuliwa Katibu Mkuu Kilimo

Mwandishi Wetu

RAIS Dk. John Magufuli amemteua Gerald Kusaya kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, kuchukua nafasi ya Mathew Mtigumwe, ambaye amepangiwa kazi nyingine katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

Ikumbukwe kuwa kabla ya kuteuliwa, Kusaya alikuwa mwenyekiti wa timu maalumu iliyoundwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa uchunguzi wa masuala mbalimbali katika tasnia ya zao la mkonge mkoani Tanga.

Machi 1 mwaka huu, Kusaya aliwasilisha ripoti ya awali ya timu hiyo wakati Majaliwa alipoanza ziara mkoani Tanga, ambapo alisema wamebaini upotevu wa mabilioni ya shilingi uliosababishwa na uongozi wa Kampuni ya Katani Ltd.

Kusaya alisema timu yake ilibaini ubadhirifu wa mabilioni ya fedha katika Kampuni ya Katani Ltd iliyopewa jukumu la kusimamia mashamba matano ya mkonge, ambayo iliingia katika madeni ambayo haiwezi kuyalipa.

Alisema kutokana na ubadhirifu huo, uwezo wa Katani Ltd kulipa madeni ni mdogo kwa kuwa hadi Desemba 31 mwaka jana yalifikia zaidi ya Sh bilioni 70 wakati mali alizonazo zina thamani ya Sh bilioni 43.

Kusaya alisema madeni hayo yanahusisha mikopo kutoka NSSF ambayo ni Sh bilioni 33.7 na makato ya kawaida ya NSSF yanayofikia Sh bilioni 1.5, kodi za TRA Sh bilioni 8.2 na madai ya wakulima Sh bilioni 31 na kwamba anaiomba Serikali muda zaidi ili wakamilishe ripoti hiyo na kuwashughulikia wahusika.

Alisema hatua hizo ni pamoja na kutaifisha mali zilizochukuliwa na waliokuwa viongozi wa Katani Ltd kinyume cha utaratibu ikiwemo nyumba na mashamba na uuzaji wa hisa ambao haukufuata utaratibu.

Mapendekezo mengine ni ya kurejeshwa serikalini kwa nyumba namba 176 eneo la Bombo ambayo ilimilikishwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Katani Ltd, Salum Shamte na nyumba 10 zilizoko ndani ya Jiji la Tanga katika maeneo ya Raskazone, Bombo, Nguvumali na Market Street ambazo zilidaiwa kununuliwa na watumishi hao kwa udanganyifu.

Timu hiyo maalumu ya uchunguzi iliyokuwa na wajumbe 13, iliyohusisha maofisa kutoka ofisi mbalimbali za Serikali, iliundwa na Waziri Mkuu na ilifanya uchunguzi mkoani Tanga kuanzia Novemba 29, mwaka jana hadi Februari 7, mwaka huu. 

Uchunguzi huo maalumu ulihusu masuala mbalimbali katika tasnia ya zao la mkonge mkoani Tanga ambayo ni pamoja na uzalishaji wa mkonge, bei ya zao la mkonge katika soko la ndani na nje ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles