28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Daktari: Wenye VVU wanaweza kupandikiziwa mimba wakajifungua salama

Aveline Kitomary – Dar es Salaam

WANAWAKE wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) sasa wana uwezo wa kupandikizwa mimba na hatimaye mtoto kuzaliwa bila kuwa na maambukizi hayo.

Hayo yameelezwa na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Vicent Tarimo katika mahojiano maalumu na MTANZANIA.

Katika mahojiano hayo yaliyofanyika Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii, Dk. Tarimo alisema kuwa upandikizaji mimba watakaofanya ni mtu kupandikizwa yai lake mwenyewe, hivyo hata wagonjwa wa VVU wataweza kupandikizwa mimba na mtoto atazaliwa akiwa salama kabisa.

Alisema kutokana na upandikizaji huo, hatua hiyo itakuwa ni njia salama isiyoruhusu maambukizi na mtoto atakayetungwa katika mimba hiyo atakuwa salama kwa kuwa maambukizi ya VVU kwa mtoto kipindi akiwa tumboni inakuwa asilimia ndogo.

“Mama mwenye VVU ana uwezo wa kumzaa mtoto ambaye hana maambukizi kwa asilimia 45 bila kutumia dawa yoyote, kwani mwili unamkinga mtoto asipate maambukizi.

“Hivyo VVU haizuii upandikizaji wa mimba, na hata kwa wale wenye magonjwa mengine tutashauriwa na daktari wa ugonjwa husika ili tuweze kuona kama hali ya mgonjwa inaruhusu kupandikizwa miamba au la,” alisema Dk. Tarimo.

Kwa mujibu wa daktari huyo, kigezo cha kwanza kwa upandikizaji mimba ni lazima wahusika wawe wanandoa, kwa kuwa hiyo ndiyo njia rahisi zaidi kwa sasa, hasa kwa kuepuka migogoro.

Alisema katika hilo, ili kuweka mazingira mazuri, kabla ya kuanza kutoa huduma ya upandikizaji mimba, taratibu na sheria zitatungwa kulingana na tamaduni ili kuepusha migogoro.

“Sisi tuna taratibu na tamaduni, hivyo sheria itapangwa na wadau wa afya ili kuepusha migogoro baada ya upandikizaji mimba, ili kuweza kukabiliana na changamoto hizo, taratibu ziwekwe, lazima sheria ya upandikizaji mimba iwepo kabla ya kuanza upandikizaji,” alisema Dk. Tarimo.

Alieleza kuwa uhitaji wa huduma ya upandikizaji mimba ni mkubwa nchini ambapo katika kliniki yake ya siku moja anawaona wahitaji saba hadi nane.

“Wapo watu wengi tu wanaotamani huduma hii ianze kutolewa, hivyo kuna uhitaji mkubwa zaidi, hasa kwa wanandoa ambao wanahudhuria kwenye kliniki,” alisema Dk. Tarimo.

Hata hivyo alisema gharama za huduma hiyo ni kubwa kutokana na uhalisia wa gharama za afya kuwa za bei ghali.

“Kiuhalisia huduma za afya ni gharama sana, ndiyo maana hata Serikali inasisitiza matumizi ya bima kwa watu wote ili kupunguza mzigo wa gharama zinazotokana na msamaha,” alibainisha Dk. Tarimo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,186FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles