25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

Samia ataka wanawake wengi kugombea Uchaguzi Mkuu

Ramadhan Hassan – Dar es Salaam

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewataka wanawake nchini kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25. 

Pia alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo imepiga hatua katika kuwapatia wanawake nafasi za uongozi ambapo hadi sasa imefika asilimia 36.7.

Akizungumza jana jijini hapa wakati akizundua Mtandao wa Viongozi Wanawake Afrika Tawi la Tanzania, alisema katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu ni jukumu la wanawake kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Samia alisema Tanzania ni nchi ya 14 kuzindua tawi hilo  ambapo Uganda inatarajia kuzindua leo na kuwa nchi ya 15.

Alisema kumekuwa na mabadiliko makubwa ya uwiano wa kijinsia ambapo kwa upande wa Bunge, kati ya wabunge 393, wanawake ni 126 ambao ni sawa na asilimia 36.7, na Baraza la Wawakikilishi la Zanzibar wanawake ni asilimia 38.

“Ni kweli kwamba katika nchi nyingi duniani bado usawa wa kijinsia haujaweza kufikiwa katika nyanja nyingi ikiwemo uongozi,” alisema Samia.

Alisema hali hiyo inagusa pia Tanzania, ingawa kwa kiasi kikubwa wanafanya vizuri ukilinganisha na nchi nyingi barani Afrika ambapo alitolea mfano mihimili mitatu ya dola ambayo imekuwa na mabadiliko makubwa.

“Kiwango hicho ni juu ya uwiano uliowekwa na nchi za SADC, cha angalau asilimia 30. Pamoja na hayo, tulishakuwa na hayo, tulishakuwa na maspika wa mabunge wanawake hapa nchini na pia katika Bunge la Afrika, pia wana manaibu spika wanawake katika Bunge la Baraza la Wawakilishi,” alisema Samia.

Alisema katika Baraza la Mawaziri wanawake ni asilimia 18 wakati naibu mawaziri ni asilimia 33 na upande wa mahakama majaji wanawake wa Mahakama Kuu ni asilimia 30 na Mahakama ya Rufaa ni asilimia 38.

“Kubwa zaidi na la kihistoria kwa nchi yetu ni kuwa katika Serikali ya Awamu ya Tano, kwa mara ya kwanza nafasi ya Makamu wa Rais imeshikiliwa na mwanamke.

“Kwa takwimu hizo utaona kwamba bado hawajaweza kufikia usawa wa kijinsia kwa kiwango kikubwa sana, lakini hiyo ni ishara kwamba uwiano wa kijinsia katika nchi umefikia nafasi za kisiasa zinazoonekana na zinatia moyo,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti mwenza wa Tawi la Tanzania, Mary Rusimbi, alisema uwepo wao katika mkutano huo unalenga katika kujiangalia, kujitathmini, kujitafakari uongozi wa mwanamke uliko.

Alisema umoja huo umeanza mwaka 2017 huku Tanzania ikiwa nchi ya 14 kuuzindua na ulianzishwa kwa ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Rusimbi alisema lengo lilikuwa ni kuunganisha nguvu za pamoja kati ya wanawake na wanawake viongozi.

Kwa upande wake, Balozi wa Norway nchini, Elizabeth Jacoben, alisema ukimwezesha mwanamke kiuchumi umeiwezesha jamii nzima kutokana na kuwa kiungo muhimu katika jamii.

Alisema Norway wamekuwa wakitoa msaada mkubwa kuisaidia Tanzania katika masuala ya wanawake.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles