28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

SAMAKI WA BAHARINI WANASABABISHA UGUMBA

 

Na VERONICA ROMWALD – ALIYEKUWA KENYA


KWA kawaida ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu mwanamke na mwanamume wakubaliane kuanza maisha ya ndoa, hutegemewa kupata mtoto.

Kinapovuka kipindi hicho, wataalamu wa afya ya uzazi wanaeleza kwamba huenda mmoja wao au wote wawili wanakabiliwa na tatizo la uzazi.

Hivyo, huwa wanashauri wanandoa kuchunguza afya zao mapema na kujiandaa na kipindi hicho muhimu katika maisha yao.

Kwani ikiwa mimba haitapatikana katika kipindi hicho wanapaswa kufanyiwa uchunguzi zaidi mapema na kupatiwa matibabu lakini wakichelewa mambo huwa magumu zaidi.

 Simulizi ya Linda

Linda Hiaduwa (36) raia wa Namibia anasema hawezi kuficha hisia zake na hata kutokwa na machozi anapokuwa akisimulia mkasa uliomkumba wa kukosa mtoto ndani ya ndoa yake.

“Sijawahi kupata mtoto, mume wangu amekuwa mwelewa na msaada mkubwa kwangu, lakini jamii inayonizunguka imekuwa ikinisimanga na kuninyooshea kidole kila wakati,” anasema Linda huku akilengwa na machozi.

Anaongeza: “Gharama za mtu kuweza kupata mtoto kwa kupandikiza ni ghali nchini kwetu, natamani serikali iweze kuwezesha huduma hizi zipatikane kwa gharama nafuu na kwa wepesi kama ilivyo kwa huduma za uchunguzi na tiba dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.

 Tafiti za WHO

Tafiti zilizofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha matatizo ya afya ya uzazi hasa ugumba na utasa yanaonekana kuwakabili watu wengi ulimwenguni.

WHO inakadiria zaidi ya wanandoa 180 hukabiliwa na matatizo ya uzazi yanayosababisha kukosa watoto hasa katika nchi zinazoendelea zilizopo barani Afrika.

Shirika hilo linaeleza asilimia 85 ya wanawake katika nchi hizo wanakabiliwa na matatizo ya uzazi ikilinganishwa na asilimia 33 ya wanawake wengine ulimwenguni.

WHO linaeleza sababu kubwa inayoonekana kuwa chanzo cha wanawake kupata matatizo hayo ni magonjwa ya maambukizi hasa yasipotibiwa vema.

 Daktari

Pauline Kibui ni Mtafiti Mbobezi na Daktari Bingwa wa Masuala ya uzazi nchini Kenya, anasema asilimia 10 hadi 15 ya wanawake ambao hawakutibiwa vema ugonjwa wa ‘clamidia’ huwa kwenye uwezekano wa kushindwa kushika mimba maishani mwao.

“Kwa sababu huwasababishia maumivu makali katika via vya uzazi na wakati mwingine husababisha mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi na hata kuharibika kabisa,” anasema.

Anasema kitendo cha kutoa mimba ovyo nacho ni miongoni mwa visababishi vinavyochangia mwanamke kupata matatizo ya uzazi ikiwamo kushindwa kushika mimba na hata kuharibika mara kwa mara.

“Kuna visababishi vingi mno, ikiwamo pia unene na uzito kupita kiasi, si jambo jema kwani huharibu mfumo na uwiano wa homoni (vichocheo vya mwili) na hata kupelekea mwanamke kushindwa kushika mimba,” anabainisha.

 Lishe duni

Daktari huyo anasema mwanamke akiwa na lishe duni mwili wake hukosa virutubisho muhimu vinavyohitajika kumuwezesha kupokea mimba.

“Ulaji usiofaa nao ni tatizo linaloweza kusababisha matatizo ya ugumba na utasa, unene na uzito kupitiliza husababisha uwiano usio sawa wa homoni (vichocheo vya mwilini) na hivyo kushindwa kupata mimba au kuharibu,” anabainisha.

Anaongeza: “Kiujumla mtindo mbovu wa maisha huchochea hali hiyo kutokea: Uvutaji wa sigara, unywaji pombe kupita kiasi, matumizi ya dawa za kulevya, kutokufanya mazoezi na mambo mengine kama hayo huchangia matatizo ya uzazi.

Dk. Pauline anasema unywaji wa kahawa kupita kiasi nao huweza husababisha tatizo hilo kutokea kwani ina kiwango kikubwa cha caffeine.

 Samaki wa baharini

“Mtu anapokula samaki wa baharini kupita kiasi anajiweka katika hatari ya kupata tatizo la ugumba na hata utasa, kwa sababu huwa wana kiwango kikubwa cha madini ya chuma na mercury,” anasema.

Anaongeza: “Wakati meli zinaposafirisha mizigo baharini na kutia nanga bandarini huwa kuna mafuta ambayo hutoka kwenye meli na kuingia baharini.

“Wale samaki hupokea madini yaliyopo kwenye mafuta hayo na yanapowaingia mwilini, binadamu anapokuja kumla samaki husika naye hupokea madini hayo.

“Yanapoingia katika mwili wa binadamu ikiwa ni mjamzito basi yule mtoto au watoto aliowabeba tumboni mwake hupokea madini hayo.

“Mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na matatizo ya uzazi tayari na katika kizazi chao wataendelea kuzaa watoto ambao wana matatizo haya hasa ugumba na utasa, tafiti nyingi zimefanyika zinaonesha hivyo,” anasema.

Anasema mjamzito naye anaweza kupata matatizo kadhaa mwilini mwake kwani madini hayo mara nyingi huweza kuathiri mfumo wa fahamu (nervous system).

“Ndiyo maana tunashauri zaidi watu kula samaki wa ziwani angalau wale huwa hawajaathiriwa na mafuta yanayotoka kwenye meli kuliko wale wa baharini, au anapokula wale wa baharini ale kwa kiasi na si sana,” anasema.

 Matunda na mbogamboga

Daktari huyo anasema matunda na mbogamboga ambazo zimeandaliwa kwa kuwekewa dawa za kuua wadudu zinaweza kusababisha matatizo ya ugumba na utasa.

“Ikiwa mjamzito atakula matunda au mbogamboga hizo, mtoto aliye tumboni anaweza kuzaliwa akiwa tayari ana tatizo la ugumba au utasa.

“Hivyo, inashauriwa watu wale kwa kiasi hasa samaki wa baharini na kuepuka kula matunda na mbogamboga zilizotiwa dawa za kuua wadudu.

“Kuna aina fulani ya samaki wenyewe huwa ni wadogo wadogo huko baharini, tunashauri pia watu kula kwa kiasi ili kuepuka matatizo haya,” anaibainisha.

 Dawa za nywele

Anasema kwa kawaida mwili wa binadamu una kiwango fulani cha madini ya zebaki ambacho hakitakiwi kuzidi, kinapozidi ni hatari kwa afya yake.

“Hata dawa za nywele, wanawake wanapaswa kuangalia aina ya dawa na ni vema kununua kutoka kwa watengenezaji waliopewa kibali na serikali za nchi husika.

“Wapo watengenezaji ambao huwa si waaminifu hasa wasiokata vibali ambao huweza kuongeza vitu ambavyo ni hatari kwa afya zao,” anasema.

Umri mkubwa

Anasema jambo jingine linalochangia matatizo hayo ni umri mkubwa.

“Hasa kwa wanawake kwa kawaida anapaswa kupata mtoto au watoto kabla au katika kipindi cha miaka 35 ikivuka miaka hiyo huwa kwenye hatari ya kuwa na matatizo haya ya uzazi.

“Tuna namna ya kuwasaidia hasa sisi wataalamu wa masuala ya uzazi, ikizingatiwa kwamba kuna magonjwa ambayo yasipotibiwa sawa sawa yanaweza kusababisha kushikana kwa nyumba ya uzazi au kuziba kabisa kwa mirija,” anasema.

Anasema matatizo ya ugumba na utasa tafiti zinaonesha huwapata watu wa jinsi zote mbili kwa kati ya kiwango cha asilimia 40 hadi 50.

“Yaani zinaonesha huchangiwa kwa kiwango sawa kati ya wanaume na wanawake, ndiyo maana tunashauri wanandoa kwenda wote wawili hospitalini kufanyiwa uchunguzi ili kama mwanaume ana tatizo atibiwe au kama mwanamke ana tatizo atibiwe kwa wakati,” anasema.

Anaongeza: “Ikiwa watachelewa mno kupata tiba na kujipata wakiwa na umri wa miaka zaidi ya 35 huwa matibabu yake ni magumu na kama itazidi zaidi ya miaka hiyo mambo huwa magumu zaidi.

“Hapo watahitaji huduma ya kupandikiza (IVF) na wakati mwingine huhitaji kuchangiwa mayai na mbegu za uzazi kutoka kwa watu wengine na gharama zake huwa kubwa zaidi.”

 Changamoto

Waziri wa Afya wa Uganda, Sarah Opendi, anasema jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya uzazi.

“Takwimu za WHO zinaonesha jinsi tatizo lilivyo kubwa duniani hasa katika nchi zinazoendelea ikiwamo Uganda, ni changamoto kubwa ambayo lazima tuongeze nguvu na juhudi kuzikabili,” anasema.

Anasema waandishi wa habari wanalo jukumu la kutumia vema kalamu zao kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya ya uzazi ili kuunga mkono juhudi za serikali katika nchi zao za kupambana na matatizo ya uzazi.

“Tumieni vema mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe sahihi kuhusu masuala ya uzazi na kutoa taarifa zitakazoijenga jamii na si kuwabomoa,” anasema.

Naye Naibu Waziri wa Afya nchini Kenya, Dk. Rashid Aman, anasema ikiwa jamii itapewa elimu sahihi itasaidia kukabili changamoto hiyo kwani asilimia 80 ya matatizo yanaweza kuzuilika.

“Ndoa nyingi zinavunjika kwa kukosa watoto, watu wanakumbana na unyanyasaji huko kwenye jamii, tunapaswa kupaza sauti kuzisaidia jamii zetu,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dk. Rasha Kelej, anasema matatizo hayo huwakumba watu wa jinsi zote hata hivyo, katika jamii nyingi wanawake pekee ndiyo hunyooshewa kidole.

“Wataalamu wanaeleza vipo visababishi vingi vinavyoweza kuchangia hali hiyo kutokea, ikiwamo magonjwa ya ngono, utoaji mimba ovyo, sababu kama hizi zinaweza kuepukwa kwa kuelimisha jamii,” alisisitiza.

 Kuhusu tuzo

Dk. Kejel anasema ili kuhamasisha waandishi wa habari kujikita zaidi kuelimisha jamii juu ya masuala hayo, Julai 9, mwaka huu taasisi hiyo ilikabidhi tuzo kwa waandishi.

Hafla hiyo iliyofanyika mjini Nairobi, nchini Kenya jumla ya waandishi 200 kutoka katika nchi 17 za Barani Afrika.

Mashaka Mgeta, ambaye ni mwandishi pekee kutoka Tanzania (Gazeti la Jambo Leo) aliye miongoni mwa washindi katika tuzo hizo, anasema waandishi wa habari wanapaswa kuwekeza zaidi katika masuala yanayohusu afya ya uzazi.

Anasema hatua hiyo itaiwezesha jamii kupata taarifa sahihi zitakazosaidia jamii kukabiliana na changamoto za afya ya uzazi na ambazo zimekuwa chanzo cha matatizo kadhaa ya kiafya na kijamii.

“Ingawa vyombo vya habari vinashiriki katika kuandika na kutangaza masuala ya afya ya uzazi, lakini ipo haja ya kuongeza ubunifu na weledi vitakavyoyafanya masuala hayo kuwa moja ya ajenda za kuchochea mabadiliko katika sekta hizo nchini,” anasema.

Mgeta ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Afya (THJ), anasema katika kuchangia ukuzaji uelewa, chama hicho kinaandaa mpango wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu namna bora zaidi ya kuandika na kutangaza habari za afya ya uzazi.

Mwandishi wa makala haya alitunukiwa cheti cha heshima kwa kuwasilisha kazi yake katika shindano la tuzo hizo kama sehemu ya kuutambua mchango wake katika kuelimisha jamii juu ya masuala hayo ya afya ya uzazi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles