31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WANANCHI MTWARA WALILIA KIWANDA CHA KUSINDIKA MATUNDA

 

Na Benny Mwaipaja, WFM, Mtwara


WAKAZI wa Kijiji cha Kilambo, Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara, wameiomba Serikali iwasaidie kuwatafutia mwekezaji atakayejenga kiwanda cha kusindika matunda na mazao ya kilimo katika kijiji chao kutokana na kijiji hicho kuwa na matunda na mazao mbalimbali yanayokosa soko na kuwasababishia umasikini.

Wakazi hao, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo, Mohamed Mkama, wametoa ombi hilo mbele ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Philip Mpango, aliyefanya ziara ya kikazi katika Kituo cha Forodha cha Kilambo, kilichoko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji, mkoani Mtwara,  kwamba kijiji chao kina fursa nyingi za kilimo zinazohitaji viwanda vya kuongeza thamani ya mazao yao na kutoa ajira kwa vijana.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo, Mohamed Mkama, alisema  kijiji chao kinapakana na nchi ya Msumbiji ambako kuna mwingiliano mkubwa wa watu katika masuala ya biashara na uhusiano wa kijamii ikiwemo pande mbili za nchi kuoleana hivyo kuwafanya wananchi wa Msumbiji waishio mpakani kutegemea bidhaa kwa wingi kutoka katika kijiji chao.

“Watu kutoka Msumbiji wananunua sana chakula na bidhaa nyingine kutoka kwetu lakini tunawauzia bidhaa bila kuongeza thamani hivyo uwepo wa kiwanda utakuza uchumi wa kijiji chetu na tunakuomba Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango, utusaidie kupata kiwanda ili nasi tuweze kunufaika.

“Waziri sisi ni wakulima wazuri wa matunda, matunda yetu wakati wa msimu yanakosa soka, yanaoza  na tunayatupa jambo linalotulazimu tukuombe utusaidie kuhamasisha wawezezaji waje wajenge kiwanda cha kusindika juisi katika kijiji chetu ili nasi tuondokane na umasikini,” alisema Selemani Kumamba

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, aliwaambia wakazi hao inabidi ufanyike utafiti wa kutosha ili kubaini wingi wa mazao yanayozalishwa na wakulima katika kijiji hicho na vijiji jirani ili kupata takwimu sahihi za uzalishaji wa mazao hayo yakiwemo matunda ili kuiwezesha Serikali kuwashawishi wawekezaji kujenga kiwanda katika eneo hilo na kuwapongeza wakulima hao kwa kufanya kazi kwa bidii na mawazo yao ya kujiletea maendeleo.

“Tukiwa na uhakika huo hata mwekezaji anayekuja tutamwambia kwa mwaka mmoja, kwa wastani, kijiji hiki na vijiji jirani vinazalisha maenbe kiasi fulani, kwa hiyo wazo la kutaka kuwa ni kiwanda ni  zuri lakini linahitaji kufanyiwa kazi zaidi” alisema Dkt. Mpango aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara. Evod Mmanda

Aliwasahauri wanakijiji hao kuanzisha mashamba mapya ya matunda na kupanda mbegu za kisasa zinazozaa kwa wingi na kuushauri uongozi wa wilaya kuwasaidia wananchi hao kupata miche ya kisasa inayozaa kwa muda mfupi ili waweze kushawishi zaidi kupatikana kwa kiwanda kijijini hapo.

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles