24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Sajaki ilivyojikita kuwajengea uwezo wanajamii kukabili ukatili

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

UCHUMI wa nchi, maendeleo ya jamii na ya mwanadamu yanategemea kwa sehemu kubwa katika uwezeshaji na elimu kwani ndio rasilimali pekee inayoweza kupeleka mbele malengo ya kitaifa.

Hata hivyo malengo ya kitaifa yamekuwa hayafikiwi ipasavyo kutokana na kuwapo kwa changamoto ukatili ambao kwa kiasi kikubwa unawaathiri wanawake na watoto.

Kuna idadi kubwa ya wanawake na watoto ambao wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa aina mbalimbali kama vile ukatili wa kingono, kimwili, kiuchumi na kisaikolojia.

Wanajamii wakiwa kwenye majadiliano wakati wa mafunzo kwa viongozi wa mashirika, vikundi, vyama vya siasa na wafanyakazi wa majumbani yaliyoandaliwa na Shirika la Sauti ya Jamii Kipunguni.

Takwimu zinaonesha kuwa mwanamke 1 kati ya 5 ametoa taarifa ya kufanyiwa ukatili wa kingono katika Maisha yake, msichana 1 kati ya 3 na mvulana 1 kati ya 7 walifanyiwa ukatili wa kingono kabla ya umri wa miaka 18.

Zipo jitihada kadhaa zinazofanywa na Serikali pamoja na asasi za kiraia kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Mathalani Serikali kwa kushirikiana na wadau inatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ulioanza 2017,2018 mpaka 2021,2022 kwa lengo la kukabiliana na changamoto za ulinzi wa wanawake na watoto nchini.

Aidha asasi za kiraia zimekuwa zikielimisha umma kuhusu masuala ya kijinsia na ukatili kupitia njia mbalimbali kama vile machapisho, mafunzo kwa viongozi na jamii kwa ujumla na kutoa huduma ya msaada wa kisheria.

Miongoni mwa asasi hizo ni Shirika la Sauti ya Jamii Kipunguni (SAJAKI) ambalo limekuwa likifanya kazi ya kutetea haki za jamii na kusaidia juhudi za kupambana na ukatili.

Kwa sasa shirika hilo linatekeleza mradi wa wezesha uelewa wa haki, zuia rushwa ya ngono ndani ya jamii, ongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika ngazi za maamuzi unaofadhiliwa na Women Trust Fund (WTF).

Kupitia mradi huo wanajamii wanajengewa uwezo ili waweze kutambua haki zao, namna ya kuendesha vikundi, kushiriki katika ngazi za maamuzi na kukomesha vitendo vya ukatili.

Hivi karibuni shirika hilo liliendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo makundi mbalimbali ya kijamii ambayo yalijumuisha viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, wafanyakazi wa ndani na wananchi wa kawaida.

Kupitia mafunzo hayo washiriki walijadili ukatili wa kijinsia, aina, chanzo, sababu, viashiria vya ukatili pamoja na matokeo ya ukatili wa kijinsia.

Pia wanapatiwa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo waweze kutambua haki zao, namna ya kuendesha vikundi na kushiriki katika ngazi za maamuzi.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Amani, Asia Ally, akizungumza wakati wa mafunzo kwa viongozi wa mashirika, vikundi, vyama vya siasa na wafanyakazi wa majumbani yaliyoandaliwa na Shirika la Sauti ya Jamii Kipunguni.

Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Seleman Bishagazi, anasema wanawajengea uwezo wanajamii ili waweze kutambua haki zao, namna ya kuendesha vikundi, kushiriki katika ngazi za maamuzi na kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Anasema wanawake wengi ambao pia ndio wahanga wakubwa wa ukatili hawana ufahamu juu ya sheria na misingi ya haki za binadamu na utawala bora.

“Washiriki wanaeleza uzoefu wao na changamoto zao kisha tunajadiliana kwa pamoja na kupata suluhisho la kuwasaidia kukuza malengo yao,” anasema Bishagazi.

Anatolea mfano kwenye vyama vya siasa na kwa wafanyakazi wa majumbani kwamba ni maeneo ambayo mara kadhaa yamekuwa yakikabiliwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa rushwa ya ngono hivyo, mafunzo hayo yatasaidia kukabili vitendo hivyo.

Kuhusu uendeshaji wa vikundi anasema wanayawezesha makundi hayo kupanua wigo wa kuendesha vikundi kwa kuzingatia kanuni na taratibu zitakazowawezesha kufikia malengo yao.

Katika mafunzo hayo washiriki walikuwa wakijadiliana katika makundi na wengine walikuwa huru kueleza visa mkasa kutokana na changamoto mbalimbali walizopitia kwenye maisha kama njia ya kuzidi kujifunza na kubadilishana maarifa.

WANUFAIKA

Kwa upande wao wanajamii waliopatiwa mafunzo hayo wanasema wamefarijika kwani wamejifunza mengi na kwamba wanatarajia yatawasaidia kukuza shughuli zao na kufikia malengo waliyojiwekea.

Pia wameweka mkakati wa kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vinazidi kuongezeka.

Mkakati huo unahusisha kwenda kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya kijamii ili kuyawezesha kujua dhana ya ukatili wa kijinsia na kukomesha vitendo hivyo sambamba na masuala ya uongozi.

Mwenyekiti wa Wajane Mtaa wa Machimbo Kata ya Kipunguni, Mboni Lyamuya, anasema wajane wengi hawafahamu haki zao za msingi na kwamba wamekuwa wakinyanyaswa na ndugu wa waume zao hasa wanapofuatilia mirathi.

“Kwangu Machimbo tuko wajane 36 lakini si wote wanaofahamu haki zao, hivyo nitakutana nao na kuwaelimisha na wenye matatizo nijue jinsi gani watapata haki zao,” anasema Mboni.

Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Amani Kata ya Kipunguni, Asia Ally, anasema vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekithiri hasa kwa wanawake na watoto na kuahidi kwenda kutoa elimu kwa jamii iweze kuwafichua wahusika.

Mshiriki mwingine wa mafunzo hayo Rachel Isaya kutoka Mtaa wa Amani Kipunguni, anasema kikundi chao kinalegalega kwenye uongozi hivyo atakwenda kuwafundisha wenzake ili kiweze kukaa sawa.

Naye Vida Shabani anayetarajia kujiunga na masomo ya elimu ya juu Oktoba mwaka huu, anasema atakwenda kutoa elimu kwa wanafunzi wenzake ili wafahamu viashiria vya rushwa ya ngono na namna ya kuiepuka.

Bishagazi anasema mafunzo hayo ni endelevu kwa makundi mbalimbali ya kijamii na kwamba wanatarajia yatakuwa na matokeo chanya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles