31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Safari ya muziki ya mkongwe wa Taarabu Bi Shakila – 1

SHAKILAANA VALERY KIYUNGU

OLD SKUL ndiyo mahala sahihi ambako mimi na wewe msomaji wangu tunakutana na kuweza kufahamisha mambo kadha wa kadha yanayohusu muziki na wanamuziki waliowahi kufanya vyema miaka ya nyuma na wengine mpaka leo hii kazi walizozifanya zinaishi, licha ya wao kutokuwapo kwenye uso wa dunia.

Wiki hii ulimwengu wa muziki ulikumbwa na kiza kinene mara baada ya taarifa za msiba wa mkongwe wa muziki wa taarabu nchini, Shakila Said, maarufu kama Bi Shakila, aliyekuwa mtunzi na mwimbaji machachari katika bendi zote alizowahi kuzitumikia enzi za uhai wake.

KUZALIWA  

Bi Shakila alizaliwa Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga, mnamo mwaka 1955. Utaratibu ni ule ule wa mtoto anapotimiza umri wa kwenda shule basi hamna budi kuandikishwa na kuanza masomo ya shule za msingi katika Shule ya Msingi Pangani, huko huko Tanga.

Muda wote wa masomo yake alikuwa ni mfuatiliaji mzuri wa muziki, hasa muziki wa taarabu, ulioonekana kuwa ndani kabisa ya damu yake, hivyo kwenye shughuli mbalimbali za uimbaji pale shuleni Bi Shakila aliweza kuonyesha kiu yake ya kutaka kuwa nyota wa muziki huo.

NDOTO YAKE YATIMIA 

Ilikuwa mwaka 1961, akiwa na miaka 6, ndipo giza lilipoanza kutoweka na yeye kuona nuru ya ndoto yake ya kuwa mwimbaji ikitimia, baadaye alijiunga na bendi ya Black Star, iliyokuwa inapiga muziki huo wa mwambao wa Pwani huko Tanga.

Yeye alikuwa ni mmoja ya waasisi wa bendi hiyo na hapo alifanikiwa kuimba wimbo wake wa kwanza unaoitwa Jogoo Acha Makuu, ukiwa ni utunzi wa Awadhi Seif na walishirikiana kuimba na mwimbaji Hamadi Mrisho.

Wimbo huo uliwavuta mamia ya mashabiki na kuwajaza kwenye kumbi ambazo Black Star ilikuwa inatoa burudani, hiyo ilitokana na uwezo wa kuchezea sauti aliokuwa nao mkongwe huyu wa taarabu.

Kundi hilo ambalo lilikuwa chini ya Ally Amani na kuongozwa na Hassan Awadhi, lilimpa majukumu mazito Bi Shakila, ambapo karibia nyimbo zote za Black Star, sauti ya Bi Shakila ilisikika na aliweza kuipandisha chati bendi hiyo.

AHAMA BLACK STAR ATUA LUCK STAR

ALIWEZA kudumu ndani ya Black Star kwa miaka kumi, tangu mwaka 1961 mpaka 1971, ambapo ilitosha kabisa kwake kuhama bendi hiyo na kwenda kutafuta maisha bora sehemu nyingine. Hapo ndipo alipotua Luck Star, bendi iliyokuwa huko huko mkoani Tanga.

Black Star na Luck Star zilikuwa ni bendi hasimu kisanaa kuanzia kuimba, kutungiana nyimbo za vijembe mpaka kuibiana wasanii kama ilivyokuwa kwa bendi za TOT na Muungano Cultural Troupe siku za nyuma.

Ndani ya Luck Star, kundi ambalo lilikuwa linamilikiwa na Soud Saidi, Shakila aliweza kufanya makubwa, hususan katika kuimba na kutunga nyimbo na ndani ya mwaka mmoja alifanikiwa kutoa nyimbo kali kama vile Kitumburi, Macho Yanacheka na Kifo cha Mahaba.

Hii ni sehemu ya kwanza, usikose sehemu ya pili ya historia ya Bi Shakila, mkongwe wa muziki wa taarabu nchini.

Maoni -0714288656

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles