27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 7, 2024

Contact us: [email protected]

Safari ya Kasongo Mpinda 1945-2015

kasongo-mpindaNA VALERY KIYUNGU

KABLA majonzi, vilio na masikitiko ya tasnia ya muziki kumpoteza mtunzi wa wimbo uliojizolea umaarufu mkubwa ‘Jojina’, David Musa, aliyekuwa kiongozi wa bendi ya siku nyingi ya Safari Trippers hayajapoa, tasnia hiyo imempoteza mwanamuziki mwingine mkongwe, Kasongo Mpinda ‘Clayton’, aliyefariki juzi katika Hospitali ya Mwananyamala, Jijini Dar es Salaam, alikokuwa akisumbuliwa na maradhi ya kisukari na ganzi.

Mpinda alikuwa mwanamuziki wa bendi ya Wazee Sugu, inayoongozwa na King Kiki. Kasongo Mpinda anatokea katika ukoo wa kichifu, alizaliwa Februali 2, mwaka 1945 katika mji wa Lubumbashi, Jimbo la Shaba huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baba yake, Boniface Mpinda, alikuwa mfanyabiashara maarufu katika mji huo, wakati mama yake, Kanku wa Mokendi alikuwa muumuni na mwimbaji mashuhuri katika Kanisa Katoliki mjini humo.

Akiwa kidato cha kwanza wazazi wake wote walifariki, hivyo Mpinda hakuendelea na masomo ya sekondari kutokana na kushindwa kumudu gharama za masomo.

Safari ya muziki

Safari yake ya muziki ilianza katika bendi ya Ode Jazz na Lupe Jazz, zilizokuwa Lubumbashi na alipojua muziki mwaka 1965 alikwenda Kinshasa kutafuta bendi ya kujiunga nayo, ambapo alikutana na Dokta Nico Kasanda, aliyekuwa mmiliki wa bendi ya L’Africa Fiesta Sukisa.

Mwaka 1968 aliachana na Dokta Nico akaelekea Lusaka nchini Zambia, ambapo mwaka 1969 alianzisha bendi yake aliyoiita The Wings Brother’s akiwa na wanamuziki vijana, wakiwemo Kibambe Ramadhani, Lomani, Jozee, Lushiku wa Lushiku na Kayembe Trumbloo.

 

Anaingia Tanzania

Mwaka 1979 akiwa na bendi hiyo waliingia nchini, lakini baada ya muda yeye na baadhi ya wanamuziki wenzake walijiunga na bendi ya Maquis du Zaire, huku wanamuziki wengine wakijiunga na bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS).

Bendi hizo zilianza upinzani mkubwa, kwani Orchestra Safari Sound (OSS) ikipiga ukumbi wa Kimara Resort na Maquis du Zaire walikuwa wakipiga ukumbi wa White House, Ubungo.

Alibadili dini

Mwaka 1984 Mpina alibadili dini kuwa Muislamu na kupewa jina la Abubakar Kasongo ‘Clayton’, ambapo pia alifunga ndoa Jijini Dar es Salaam na Habiba, ambaye walipata watoto Idd na Kiloman.

Baadaye waliungana na Mbombo wa Mbomboka wakaanzisha bendi ya M.K. Group, maarufu ngoma za maghorofani, iliyokuwa ikipiga muziki wake katika Hoteli ya New Africa ya Jijini Dar es Salaam.

Mpinda alidumu kwenye bendi ya M.K. Group kwa takribani miaka nane, kabla ya kutimkia bendi ya Zaita Muzika ya Ndala Kasheba,  ambapo walisafiri na bendi hiyo kwenda London, nchini Uingereza kwa mwaliko wa Watanzania waishio nchini humo.

Aliporejea mwaka 1988 aliiwezesha bendi ya M.K. Group ambayo ilishinda mashindano ya Top Ten Show, kupitia wimbo wake wa ‘Uwajibikaji’, neno ambalo lilikuwa kauli mbiu ya rais wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi kwa miaka hiyo.

King Kiki amwelezea

King Kiki anasema Kasongo Mpina alikuwa mwanamuziki mwenye uwezo mkubwa wa kutunga nyimbo mbalimbali na alikuwa na mchango mkubwa katika bendi mbalimbali alizowahi kufanya nazo kazi, hivyo kifo chake kimeacha pengo kubwa katika bendi yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles