24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, March 29, 2023

Contact us: [email protected]

Rwanda yazuia raia wake kuzuru Uganda

KIGALI, RWANDA

SERIKALI ya Rwanda imewataka raia wake kusitisha ziara zao nchini Uganda baada ya kuishutumu nchi hiyo kuwanyanyasa wale wanaoishi ama kutembelea nchini humo.

Uganda imeishutumu Rwanda kufunga mipaka baina ya nchi hizi mbili.

Lakini Rwanda imekanusha ikisema mipaka iko wazi.

Alhamisi iliyopita, Mamlaka ya Mapato ya Rwanda iliamrisha malori ya mizigo kutotumia tena mpaka wa Gatuna kwa madai ya shughuli za ujenzi wa kituo kimoja cha mpakani baina yake na Uganda.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo malori yaliombwa kutumia mpaka wa pili wa Kagitumba kaskazini mwa Rwanda.

Hata hivyo, watumiaji hupendelea njia ya mpaka wa Gatuna kwa kuwa ni rahisi na fupi kuliko ya mpaka wa Kagitumba.

Mpaka wa Gatuna ni eneo ambalo huruhusu kupita kwa bidhaa kutoka mji mkuu wa Uganda Kampala au Mombasa nchini Kenya.

Wakazi wanasema ni kama ‘ghala kwa biashara kutoka maeneo hayo’.

Rwanda inaishutumu Uganda kunyanyasa Wanyarwanda wanaoishi ama kufanyia biashara nchini humo na pia kuunga mkono makundi ya waasi.

Miongoni mwa makundi hayo ni Rwanda National Congress (RNC) linalodaiwa kuongozwa na mkuu wa zamani wa majeshi, Jenerali Kayumba Nyamwasa aliyeko uhamishoni nchini Afrika Kusini.

Kwa upande mwingine, Uganda inaishutumu Rwanda kwa vitendo vya kijasusi kwenye ardhi yake huku ikiwashuku baadhi ya raia wa nchi hiyo kuhusika na vitendo hivyo.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) katika eneo la Kisoro, Diwani Abel Bizimana alieleza kwamba hali haijabadilika.

“Tunaathirika kama viongozi wa kieneo, kama jumuiya ya wafanyabiashara na wateja pia tunaowahudumia,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,259FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles