23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

RUWASA yawaondolea kero ya maji safi wananchi wilayani Maswa

Na  Samwel Mwanga, Maswa

WANANCHI katika vijiji  vya Sengwa, Isulilo na Nguliguli vilivyoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu waliokuwa wanakabiliwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu hususan wakina mama kwa ajili ya kusaka maji usiku na mchana hatimaye wamepata mkombozi baada ya kukamilika kwa miradi ya maji safi na salama katika vijiji vyao.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Waandishi wa Habari yenye lengo la kutembelea na kuona miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa katika Wilaya hiyo na Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Mkoa wa Simiyu.

Katika ziara hiyo, Meneja wa Ruwasa wilaya ya Maswa, Mhandisi Lucas Madaha amesema kuwa lengo kubwa la Serikali ya awamu ya sita ambayo inaongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya upatikanaji wa maji safi na salama na kuwasadia wananchi wote hasa wakinamama kuwatua ndoo kichwani pamoja kuondoka na kero ya kutembea umbari mrefu.

Amesema kuwa kwa sasa Ruwasa wana kauli mbiu ya “MajiBombani” ambao lengo lake ni kuhakikisha wanawafikishia wananchi ambao wanaishi maeneo ya vijijini maji majumbani ili kuweza kumtua mama ndoo kichwani.

“Hii kauli mbiu Maji bombani tumelenga kumfikishia mwananchi maji majumbani hasa wale ambao wanaishi maeneo ya vijijini ambao ndiyo tunawahudumia maana zamani tuliwasogezea maji umbali wa mita 400.

“Kwa mpango wa sasa tunataka kila mwananchi mwenye uwezo akute maji ndani ya nyumba yake wabaki wale wenye uwezo mdogo waweze kuchota maji kwenye vituo vya kuchotea maji na hapo ndipo ile adhma ya kumtua mama ndoo kichwani itakuwa imekamilka maana atakuwa na maji ndani ya nyumba hatabeba tena madumu ya maji kichwani,” amesema Mhandisi Madaha.

Amesema kuwa kwa sasa miradi mipya wanayoisanifu wameweka asilimia 50 wananchi waweze kuvuta maji majumbani ili kuweza kumtua mama ndoo kichwani.

Akizungumzia hali ya upatikani maji katika wilaya ya Maswa Mhandisi Madaha amesema tangu Rais Samia Suluhu aingie madarakani kipindi cha mwaka mmoja amesema kuwa imeongezeka kwa asilimia 2.2 na kufikia asilimia 72.2 katika maeneo wanayotolea huduma ambayo ni ya vijijini.

Amesema kutokana na kasi ya upatikanaji wa fedha katika miradi ya maji zinatolewa na serikali ya awamu ya sita ifikapo mwaka 2025 watafikia malengo ya asilimia 85 ya upatikanaji wa maji safi na salama vijijini kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Aidha, amewaomba wananchi na viongozi ambapo miradi ya maji imekamika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kuhakikisha kwamba wanailinda miundombinu ya maji isiweze kuharibiwa wala kuibiwa na badala yake waitunze ili iweze kudumu kwa kipindi kirefu bila ya kuwa na mapungufu.

Naye mkazi wa kijiji cha Sengwa wilayani humo, Bahati Focus amepongeza uongozi wa Ruwasa mkoa wa Simiyu na kuwataka waendelee zaidi ya kufikisha huduma ya maji safi na salama katika maeneo mengine ambayo yamekuwa na changamoto kubwa ya wananchi kutokupata huduma hiyo katika wilaya hiyo.

“Sisi tumepata maji safi na salama tena yenye uhakika katika kijiji chetu tena yanatoka Ziwa Victoria hivyo pamoja na kazi nzuri ya Ruwasa mkoa wa Simiyu tunaomba wasogeze huduma hii katika maeneo mengine ambayo yana changamoto ya upatikanaji wa maji,”amesema Focus.

Naye Flora Nunghu mkazi wa kijiji cha Isulilo licha ya kuipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kushirikiana na uongozi wa Ruwasa kwa kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo wa maji katika kijiii hicho  ambao kwa upande wao utakuwa ni mkombozi mkubwa sana.

Ameongeza kuwa kwa miaka mingi wakinamama wa kijiji hicho walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya maji ikiwamo baadhi yao ndoa zao kuvunjika sababu ya kuachwa na wanaume zao kutokana kutumia muda mwingi kutafuta maji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles