23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

RIPOTI MAALUMU: WIMBI WIZI WA FEDHA ATM LAIKUMBA UINGEREZA

“HAKUNA kizuri kisicho na kasoro”, ni msemo unaoendana na ujio wa Sayansi na Teknolojia, ambayo siku hadi siku inazidi kukua na kumrahisishia binadamu katika mahitaji yake ya kila siku.

Wakati ukuaji wa teknolojia ukileta manufaa makubwa kwa maendeleo ya binadamu, unatumiwa pia vibaya na watu wenye nia ovu, ambao huutumia kuwatandika na kuwaletea maumivu, mateso na mishtuko wenzao.

Moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi na ukuaji huo wa teknolojia kutumiwa vibaya ni sekta ya kibenki, ambayo wateja wanajikuta wakiibiwa fedha kutoka akaunti zao.

Njia zinazotumiwa na wahalifu ni nyingi na zenye kutumia akili, ikiwa ni pamoja na zile, ambazo wahalifu wanaweza kukaa mafichoni wakahamisha fedha kupitia mtandao wa kompyuta.

Au wanaweza kwenda kwenye mashine za kutolea fedha maarufu ATM kuzichokonoa au kuzichezea na kupandikiza vitu kama kamera za siri kabla ya kutimiza malengo yao kwa namna tofauti tofauti.

Aina hii ya wizi imeripotiwa mfululizo nchini Uingereza katika wiki za karibuni kiasi cha kuzishtua mamlaka zinazohusika, ambazo wakati zikikuna kichwa kutafuta namna ya kudhibiti, zimechukua hatua ya kutoa elimu kwa wananchi wachukue tahadhari.

Unapoenda katika mashine ya kuchukulia fedha iliyochezewa jijini London, kwa jicho la kawaida, inaonekana kuwa sawa na mamilioni mengine ya ATM, ambazo watu huzitumia kila siku kuzifikia fedha zao.

Lakini kuna shimo dogo mno la ukubwa wa tundu la sindano katika mfuniko wa nje huficha siri, ambayo inaonesha jinsi wezi walivyoweza kubobobea na kuimarisha utaalamu wao wa teknolojia.

Polisi wanaochunguza mashine zilizochezewa waligundua shimo lililolenga kuchomeka kamera ya udogo huo, ambayo ilifichwa ndani ya mfuniko bandia wa sehemu ya kutolea fedha.

Kamera hiyo inaweza kurekodi nywila, yaani namba za siri za mteja anayechukua fedha au kutaka kufahamu taarifa nyingine za akaunti yake wakati anapoenda ATM.

Mbinu hii inaweza kukamata kadi ya mteja, ambapo huinakili pamoja na namba za siri na utambulisho, kwa ajili ya malengo ya kuiba baadaye.

Mamlaka ziligundua kifaa hicho katika mashine za kutolea fedha za yadi ya Kanisa la Mtakatifu Paul mjini London mwezi uliopita, ikiwa ni mfululizo wa ugunduzi kama huo eneo hilo ulitokea wiki za karibuni.

Machi 7, kamera kama hizo zilikutwa katika mashine nyingine ya kutolea fedha eneo hilo. Safari hii, shimo la kurekodi liliwekwa katika kipande cha plastiki juu ya kibodi (keypad).

Wakati mfuniko feki wa plastiki ulipoondolewa, kifaa kidogo cha kurekodi kilikutwa ndani kikiwa na malengo ya kurekodi namba za siri za wateja.

Polisi sasa wamechapisha picha kuionesha jamii namna vifaa hivyo, ambavyo kwa jicho lisilo la kidadisi ni ngumu kugundua vinavyoweza kukudanganya.

Kwa jicho la kawaida vinaonekana halisi kutokana na namna vinavyofanana na mazingira ya eneo vilivyowekwa mithili ya kinyonga mwenye kujibadili rangi kufuatana na mazingira alimo ili kuwapotezea maadui.

Machi 2 na Machi 8 mwaka huu, polisi walikamata kifaa kingine kinachoaminika kuambatanishwa katika mashine ya kutolea fedha jijini humo na wahalifu hao.

Lilikuwa tukio la karibuni la wizi katika mashine za kutolea fedha, ambalo liliwafanya polisi wawaonye watu kuwa makini na ishara yoyote yenye shaka wanayoikuta katika mashine hizo.

Ofisa wa Polisi, Matt Clarke kutoka Kikosi cha Polisi cha Kupambana na Uhalifu katika Jiji la London anasema: “Kuweni waangalifu wakati wa kutumia mashine za kutolea fedha katikati ya jiji la London na London kwa ujumla wake.

“Iwapo utabaini kitu chochote kisicho cha kawaida kuhusu mashine ya kutolea fedha, au iwapo kuna ishara inayoonyesha mashine ilichezewa, usiitumie. Iwapo una shaka, jaribu na kutumia mashine zilizo ndani ya tawi la benki.”

 Tatizo hilo halipo katika jiji hilo la London pekee. Siku 10 tu zilizopita, polisi wa mji wa Lancashire waliwaonya wakazi wa Preston, Leyland na Bamber Bridge kwamba vifaa hivyo vya kupachika vilionekana katika mashine za kutolea fedha zilizopo katika miji hiyo.

Mashine hizo zilizuia kadi kutoka, wakati kamera kama hizo zilizokutwa London zikirekodi namba za siri za wateja.

Kufuatia ugunduzi huo, polisi walishauri: Kabla ya kutumia mashine, mteja akague kama kuna shaka katika sehemu za kuingizia kadi, keypad na chochote katika eneo kuzunguka eneo hilo. Na ikiwa kuna shaka wafanyakazi wa benki wajulishwe na wafikirie kutumia mashine nyingine.

Aidha, polisi walishauri wakati unapotaka kuweka nywila kukinga kwa mkono ili zisionekane unapoziweka katika eneo la keypad kwa vile mara nyingi shimo lenye kamera huwa pembeni au juu ya keypad.

Wizi huu katika mashine za ATM haupo Uingereza tu bali kote duniani Tanzania ikiwamo.

Nchini Tanzania ni matukio ambayo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara na kuwaliza wengi.

Wahalifu nchini hucheza na nywira (password) za watu wanaopenda kutoa fedha zao kupitia ATM zilizowekwa sehemu mbalimbali hasa kwenye vituo vya kujazia mafuta.

Sababu za kupendelewa kwa sehemu hizo ni kwamba mtu mhalifu anaweza kufanya yake bila kushtukiwa tofauti na maeneo ya kibenki.

Wizi huu hufanyika nyakati za usiku majira ya saa tisa hadi saa tisa, wakati ule wa kutegea kamera zao hufanyika muda ambao huwa na wateja wengi hasa siku za mapumziko.

Wahalifu pamoja na mambo mengine huzima kamera za usalama za eneo husika kwa kuzipulizia rangi maalumu kuzitia ukungu, hivyo kuharibu muonekano wake na kuruhusu wao kuingia eneo hilo bila  kuonekana na kufanya wizi wao.

Baada ya kuzivuruga kamera za usalama huweka kamera zao za siri kwa ajili ya kunasa namba za siri za kufungulia akaunti ambazo huzisoma katika kompyuta na kuzinakiri katika daftari lao maalumu, kisha kuchukua kadi zao bandia na kuchukua fedha.

Kamera hiyo huwekwa juu ya eneo ambako kadi ya ATM huingizwa. Mteja anapochomeka kadi yake bila kujua filamu husoma taarifa zake na kuzibakiza mikononi mwa wezi, ambao huzitumia kuchonga kadi mpya na kumwibia ilihali mteja anayo kadi yake mkononi.

Hata hivyo, wakati mwingine wahalifu hushirikiana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu wa kampuni zinazotengeneza kadi za ATM, kuandaa kadi mpya ili kufanikisha wizi huo au kuuza mfumo wa utengenezaji kadi kwa wahalifu ambao huandaa kadi za bandia kwa lengo la kuwasaidia katika wizi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles