27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

SHERIA ZA WAUZA UNGA NI ‘KUUA’ WALIO MBALI

Na Mwandishi Wetu,

NAUPENDA wimbo wa Ten Crack Commandments ulioimbwa na Christopher Wallace ‘Notorious BIG’. Kwa Kiswahili chepesi, wimbo huo unaweza kuuita Amri 10 za Dawa za Kulevya.

Sababu ya kuupenda wimbo huo ni kuwa amri zote 10 kama ambavyo BIG a.k.a Big Small aliziorodhesha katika shairi lake kisha kuimba kwenye mdundo mzuri wa Hip Hop, zinajenga picha wauza unga ni watu wa namna gani.

BIG kwa kutambua kuwa wangeweza kutokea watu wakambishia katika hizo amri zake 10, anaanza kwa kutamba kuwa hakuna mtu wa kumwambia kitu kwenye biashara ya dawa za kulevya. Anasema aliifanya biashara hiyo kwa miaka kadhaa na ilimfanya awe mnyama.

Chukua mstari huo; biashara ya dawa za kulevya ilimfanya BIG awe mnyama. Maana yake ukiwa muuza dawa za kulevya unakuwa mnyama. Yaani unapoteza roho ya utu.

Amri zote nazikubali, lakini huvutiwa zaidi na amri ya nne; Never get high on your own supply.

Kiswahili: Kamwe usitumie unachouza.

Kwamba unapokuwa muuza unga unajua kuwa hicho ni kilevi cha maangamizi, kwa hiyo BIG anakufahamisha kuwa usijaribu kutumia, maana utaangamia.

Amri ya tano ni muhimu; never sell no crack where you rest at. I don't care if they want a ounce, tell 'em "bounce!"

Kiswahili: Usiuze dawa kwenye maeneo yako ya kujidai. Sijali kama watataka japo cha ukucha, waambie imegonga mwamba.

Ufafanuzi ni kuwa unga ni maangamizi, kwa hiyo unatakiwa kuuza mbali, siyo kwenye maeneo unayoishi, maana utawaangamiza watu wanaokuzunguka.

Ipo amri ya saba ambayo BIG anasema; “tenganisha biashara na familia yako”, kwamba haitakiwi hata kidogo watu wa familia yako wahusike na uharamia wako ili ukipata msala ujikute matatizoni peke yako.

Amri ya nane pia anaelekeza “usijibebeshe mzigo mwenyewe”, kwamba ukiwa muuza unga unafahamu kuwa ni kimeo, kwahiyo wabebeshe wengine ili wakikamatwa uwe msala wao.

Alichokiimba BIG, ndicho hasa wauza dawa za kulevya wakubwa huzungumza. Muunza unga hufahamu kwamba dawa za kulevya ni kifo, kwa hiyo huhakikisha anauza mbali ili ‘aue’ watu baki.

Curtis Jackson ‘50 Cent’ ambaye alipata mafanikio makubwa katika biashara ya dawa za kulevya akiwa na umri wa miaka 12 tu kabla ya kuacha baadaye kujikita kwenye muziki wa Hip Hop na filamu, anasema kuwa muuza unga wa kweli hatumii.

50 Cent anakiri kuwa alikuwa ‘mnyama’ wa kuuza unga, anasema: “Ngoja niwaambieni, ukiona mtu anatumia ujue si muuzaji. Na kama ni muuzaji ujue hiyo kazi haiwezi. Muuzaji anayeijua kazi yake huwa hatumii.”

Uzoefu wake na mafanikio aliyoyapata kupitia biashara ya dawa za kulevya, 50 Cent ameeleza kwenye documentary inayoitwa How to Make Money Selling Drug, iliyotengenezwa Hollywood, Marekani.

SERA YA WAUZA UNGA

Afghanistan wakati wa utawala wa Taliban chini ya Mullah Omar, walikuwa wastawishaji wakubwa wa cocaine. Hata hivyo, sera yao ilikuwa na kanuni mbili.

Kanuni ya kwanza; cocaine yote iliyokuwa inastawishwa kutouzwa nchini humo. Yaani ni lazima isafirishwe yote kwenda nje. Hawakutaka ibaki Afghanistan kisha raia wa nchi hiyo watumie na kuangamia.

Kanuni ya pili; wasafirishaji lazima wathibitishe kuwa cocaine yote wataipeleka Marekani na Ulaya. Shabaha yao ilikuwa kuhakikisha vijana wengi wa Marekani na Ulaya hasa Uingereza, wanatumia dawa za kulevya ili kudhoofisha kizazi cha mataifa hasimu.

Ukichukua sera hiyo kuwa hakuna kuuza unga nyumbani na sharti ni kuwauzia maadui, unaungana na amri ya tano ya Big Small kuwa ‘ngada’ haiuzwi maeneo ya kujidai. Kuuza nyumbani ni uharibifu wa kizazi.

Muuza unga akimkuta mwanaye anatumia atalia kisha atamtafuta mtu ambaye anamuuzia na akimkamata vita yake haitakuwa ndogo. Maana anajua kazi ambayo anaifanya kwa watoto wa wenzake.

Ni kwamba muuza unga hutaka utajiri kupitia kuharibu watoto wa wenzake lakini huwalinda wa kwake na matumizi ya ‘madubwasha’ hayo.

KICHEKO CHA MUUZA UNGA

Unapomuona teja ameharibikiwa na matumizi ya dawa za kulevya, maana yake muuza unga anakenua vizuri kabisa, kwani anakuwa ameshafanya biashara na kuingiza fedha nyingi.

Muuza unga hana tofauti na mtu ambaye anamtoa kafara mtu mwingine ili apate utajiri. Muuza unga ni sawa na mchawi anayemiliki misukule.

Kijana na nguvu zake anaanza kutumia unga kisha anakuwa mtumwa wa kilevi hicho cha maangamizi. Jinsi anavyoendelea kutumia ndivyo anavyoteketea.

Muuza unga hawezi kumhurumia teja anayeangamia na unga kwa sababu kadiri teja anavyoangamia ndivyo inavyomaanisha yeye kuzidi kuingiza fedha na kutajirika.

Ukiona kijana alikuwa na mwili mzuri, afya bora kabisa, ghafla anaanza kudhoofika na kupukutika. Hapo piga mahesabu kwamba kuna wauza unga wamejenga majumba, kununua magari na kufanya kufuru nyingi za starehe kupitia afya ya kijana huyo na fedha zake.

Hivyo, kwa kila mtu mwenye moyo wa kibinadamu, anayeumizwa na vijana wengi kutopea kwenye mihadarati, anapaswa kila akimuona teja anateseka, aanze kusikitika.

Tofauti yako na muuza unga lazima ionekane pale nyote mnapomtazama mtumia dawa za kulevya. Muuza unga achekelee kwa sababu ananufaika kwa kuingiza fedha kupitia mabadiliko ya kiafya ya teja. Wewe unapaswa kuumia maana nguvu kazi inapotea.

Inapotokea wewe unamcheka teja kama ilivyo kwa muuza unga, maana yake hapo tofauti yenu haionekani. Nyote mpo sawa! Je, wewe unakuwa umeingiza nini kwa mabadiliko ya kiafya ya teja zaidi ya kushuhudia nguvu kazi inapotea?

Vijana wengi ambao walikuwa na nguvu zao, walikuwa wakifanya kazi na kuingiza vipato halali, mara wakajikuta kwenye vishawishi na kuanza kutumia. Walipoanza wakashindwa kutoka, mwisho wameteketea.

Je, huoni kama taifa tunakuwa tunapoteza mzunguko wa wachapakazi? Na hiyo ni hasara kubwa mno katika nchi.

MITEGO YA MUUZA UNGA

Kwa taarifa hizo kwa ukamilifu wake, jawabu ni kuwa mitego ya kunasa wauza unga huwekwa mbali. Mara nyingi wapelelezi hufanya makosa kwa kuwachunguza wauza unga kwenye maeneo wanayoishi.

Wauza unga kwa utaratibu wao wa kibiashara, huwa hawafanyi mgawanyo wa bidhaa zao kwenye maeneo wanayoishi. Kumfuata nyumbani na kumpekua ni kujisumbua tu. Wauza unga wengi hukwepa familia zao kujua kuhusu biashara zao.

Muuza unga huchunguzwa hatua kwa hatua. Kwa kuanzia watu anaokutana nao, halafu nao wanafuatiliwa mpaka mwisho wa mzunguko. Kutaka kufupisha mzunguko wa upelelezi ni sababu ya wauza unga wengi kuendelea kutamba mitaani kuwa hawahusiki.

Kutokana na teknolojia ya kukwepa simu kufuatiliwa au kuingiliwa, inakuwa vigumu kunasa ushahidi wa muuza unga kwenye mawasiliano yao, hivyo njia isiyo na shaka ni kutengeneza mnyororo.

Mtu anayehisiwa anauza dawa za kulevya, hufuatiliwa kwa kumchunguza mmoja baada ya mwingine katika mzunguko wa watu ambao huwasiliana nao au kukutana nao. Kila mmoja hufuatiliwa kwa mzunguko wake.

Baada ya mtu kwenye mtandao kunaswa, hutumika kunasa wengine wote mpaka yule mhusika mkuu. Mtindo unaotumika ni kumkamata mmoja na kuwachia huru kwa masharti ili asaidie kupata wengi.

Mataifa makubwa, askari wake wakishamkamata mtu mdogo yeye hupewa ahadi ya kuachiwa huru lakini mpaka asaidie mtandao wake wote ukamatwe. Ni hapo ndipo kazi hufanyika kwa ufanisi zaidi mpaka wale mapapa kabisa kukamatwa.

Hivyo, ni kosa kufupisha mzunguko wa upelelezi kwa kutegemea kumkamata muuza unga na kumpata akiwa na vidhibiti nyumbani kwake au kwenye maeneo anayoishi. Wauzaji hasa hupiga mishale ya mbali kisha kukusanya mabilioni yao bila presha.

Itaendelea Alhamisi ijayo…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles