RELI YA KISASA YAZINDULIWA KENYA

0
591

 

 

MOMBASA, KENYA

NI mwanzo mpya kwa sekta ya usafirishaji nchini hapa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuzindua huduma za treni mpya ya kisasa mjini Mombasa juzi.

Msisimko ulikuwa mkubwa katika mitandao ya jamii, ikiwamo Facebook na Twitter, huku wengi wakionekana kusifia hatua hiyo ambayo inaonekana kuwapunguzia Wakenya gharama za usafiri.

Lakini kilichowasisimua Wakenya zaidi ni tangazo la Rais Kenyatta kuwa nauli mpya kwa abiria watakaotumia treni hiyo itakuwa Sh 700 za Kenya (sawa na Sh 14,000 za Tanzania) kutoka Mombasa hadi Nairobi kwa daraja la kawaida.

"Abiria yeyote asilipishwe zaidi ya Sh 700 kutoka Mombasa hadi Nairobi au Nairobi hadi Mombasa," alisema Rais Kenyatta huku wengi wakishangilia tangazo hilo.

Awali Waziri wa Uchukuzi, James Macharia, alisema kuwa nauli kati ya Mombasa na Nairobi kwa kutumia treni mpya itakuwa nusu ya viwango vinavyotozwa na mabasi.

Alisema kwa watumiaji wa daraja la kawaida, yaani economy class, watalipa Sh 900 za Kenya (sawa na Sh 18,000 za Tanzania) kwa njia hiyo.

Wale wa daraja la kibiashara watalazimika kulipa Sh 3,000 za Kenya (sawa na Sh 60,000 za Tanzania) kwa njia hiyo hiyo.

“Tuliangalia viwango vya nauli sokoni, na viwango bora kwa wananchi na biashara. Tunataka viwango vitakavyowawezesha wananchi kufurahia huduma na wakati huohuo viwango vinavyoendeleza huduma hiyo,” alisema.

“Aina ya pili ya treni inatarajiwa kuzinduliwa Desemba na nauli itakuwa chini zaidi,” alisema Macharia.

Safari ya kutoka Mombasa kuelekea Nairobi na treni ya kisasa itachukua saa nne na nusu, ikilinganishwa na saa tisa kwa kutumia basi na saa 12 kwa kutumia treni ya zamani.

Rais Kenyatta alionekana kuipunguza nauli kwa Sh 200 na ikizingatiwa ni wakati wakampeni za uchaguzi, Serikali itatumia kila jambo kuwavuta  wapigakura kuichagua tena hapo Agosti 8.

Aidha, uzinduzi huo ulipata wakosoaji wengi mtandaoni, hasa wa upinzani, waliodai kuwa hiyo ni mbinu tu ya kujipigia debe.

Walisema kuwa mradi huo wa reli ya kisasa (Standard Gauge – SGR) ulianzishwa na Rais mstaafu Mwai Kibaki, hivyo Serikali ya Kenyatta haipaswi kujitapa eti imewaletea Wakenya maendeleo.

Kilichowaudhi zaidi ni kuzuiwa kwa Gavana wa Mombasa, Hassan Joho, kuhudhuria uzinduzi huo baada ya kutaka kuelezwa sababu ya gharama ya ujenzi wa SGR kupandishwa kwa Sh bilioni 100.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here