23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

NDESAMBURO UMEKWENDA! UTABAKI ALAMA YA DEMOKRASIA

 

 

Na Zitto Kabwe,

SALAM zangu za rambirambi kwa dada yangu mpenzi, Lucy Owenya, kwa kupotelewa na baba mzazi Mzee Philemon Kiwelu Ndesamburo.

Ni msiba mkubwa kwa watu wa Kilimanjaro na hasa Moshi Mjini ambapo Mzee ‘Ndesa Pesa’ alikuwa mwakilishi wake bungeni kuanzia mwaka 2000 hadi 2015.

Mkoa wa Kilimanjaro umepoteza mtu ambaye aliweka masilahi ya mkoa wake mbele kuliko kitu kingine chochote.

Ni msiba mkubwa kwa wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho alikuwa Mwenyekiti wake wa mkoa tangu chama hicho kilipoanzishwa mpaka mauti yalipomkuta.

Huwezi kutaja maendeleo ya Chadema kwa nchi yetu bila ya kutaja jina la Mzee Ndesamburo. Nimepata bahati ya kufanya naye kazi kwa karibu, naweza kutamka bila wasiwasi kwamba ni mmoja wa watu waliokipenda chama chake kwa dhati kabisa.

Huu ni msiba mkubwa kwa Watanzania, mzee Ndesamburo alitumia uwezo wake wa fedha na akili kuimarisha mfumo wa vyama vingi nchini kwetu.

Ni wazi mchango wake katika kupigania demokrasia nchini ni wa kupigiwa mfano na kwa kweli wengi wetu leo tunafaidi matunda ya vyama vingi kwa sababu ya kazi kubwa ambayo Mzee Ndesamburo na wenzake walio hai na waliotangulia mbele ya haki waliifanya.

Mzee Ndesamburo amechangia sana ukuaji wa Sekta ya Utalii nchini ambapo kupitia kampuni zake za Keys Hotels ameweza kuchangia sana ukuaji wa sekta ya utalii hapa nchini kwetu.

Bungeni alikuwa mstari wa mbele kutaka uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro kutokana na tishio la theluji kuondoka katika uhai wetu.

Kwa hakika vyuo vikuu vyetu vya umma vingekuwa vinatenda haki Mzee huyu angepewa Shahada ya Uzamivu ya heshima kwa mchango wake katika maendeleo ya Sekta ya Utalii nchini.

Nawapa pole sana watoto, wajukuu na vitukuu vya Mzee Ndesamburo ambapo mzee wetu huyu aliishi maisha yake na ameacha ‘Legacy’ (alama) yake.

Najua maumivu yenu lakini tupo wengi tunaoumia nanyi na ninamuomba Mwenyezi  Mungu awavushe kwenye mtihani huu mkubwa kwa kuwa na umoja na mshikamano miongoni mwenu.

Poleni sana ndugu zangu wa Chadema kwa kupotelewa na kiongozi wenu na kiongozi wetu pia.

Poleni sana wana Moshi Mjini na wana Kilimanjaro wote, poleni Watanzania.

Pumzika kwa amani Philemon Kiwelu Ndesamburo hiyo ndiyo njia yetu sote. Amina

Mwandishi wa makala haya ni Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles