RANIERI: MAHREZ SAHAU TUZO, FANYA KILICHOKULETA

0
647

LONDON, ENGLAND


 

Claudio RanieriKOCHA wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Leicester City, Claudio Ranieri, amemtaka mshambuliaji wake, Riyad Mahrez, kusahau tuzo alizopata msimu uliopita na aangalie kilichomleta ndani ya kikosi.

Msimu uliopita, mchezaji huyo alikuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho akishirikiana na wenzake, kisha kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, hata hivyo, mbali na kutwaa ubingwa huo, lakini aliweza kupewa tuzo ya mchezaji bora wa mashindano hayo.

Hata hivyo, mchezaji huyo Desemba 12 mwaka jana alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mwaka kwa wachezaji kutoka nchini Afrika ambao wanacheza soka la kulipwa barani Ulaya, huku tuzo hiyo ikitolewa na Shirika la Utangazaji la BBC.

Kutokana na hali hiyo, kocha wake, Ranieri anaamini kuwa mchezaji huyo anaweza kubweteka kutokana na tuzo hizo na kusahau kilichomleta ndani ya kikosi cha Leicester City.

Ranieri anaamini alianza kushangaa uwezo wa mchezaji huyo kushuka katika mchezo dhidi ya Everton, ambao ulipigwa siku ya Boxing Day Desemba mwaka jana, huku mabingwa hao wakichezea kichapo cha mabao 2-0.

Kocha huyo amemtaka mchezaji huyo kufuata mifano ya nyota wa dunia hii katika soka kama vile Lionel Messi ambaye anakipiga katika klabu ya Barcelona, na Cristiano Ronaldo ambaye anaitumikia klabu ya Real Madrid, huku wachezaji hao wakiwa wamechukua tuzo mbalimbali, lakini bado wanaonesha uwezo wao.

“Nadhani msimu uliopita ulikuwa ni mara ya kwanza kwa Riyad kutwaa tuzo mbili kubwa, lakini kwa sasa anaonekana kupunguza kasi ambayo alikuwa nayo tangu msimu uliopita.

“Lakini wachezaji wakubwa kama vile Ronaldo na Messi wamefanikiwa kushinda tuzo mbalimbali kama vile Ballon d’Or na nyingine nyingi, ila bado wanatamani kushinda mara kwa mara.

“Kitu ambacho wachezaji hao wanakifanya na kufanikiwa ni kwamba, wanasahau kama wametwaa tuzo hizo na huku wakiangalia mbele kwa ajili ya kutwaa mara kwa mara kama mara yao ya kwanza.

“Riyad ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa, lakini kama atakuwa tayari ametosheka na tuzo hizo alizozipata atakuwa amefanya jambo ambalo si sahihi, kwa sasa anatakiwa kubadilika na kuongeza kasi zaidi,” alisema Ranieri

Inadaiwa kwamba mchezaji huyo alipumzika katika mchezo dhidi ya Everton huku akimwambia kocha wake amechoka na anataka kuchaji betri mwilini kwa ajili ya kuongeza nguvu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here