31.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia atoa maagizo Nane Nanenane

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wateule wake kuzingatia maeneo manane ya msingi ikiwamo kupitia upya bei za mbolea.

Rais Samia ametoa maagizo hayo Agosti 8, 2023 wakati akifunga Manonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi maarufu Nanenane yaliyofanyika kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Amesema ajenda ya Serikali ni kuongeza mchango wa sekta ya kilimo hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

“Ndio maana tumekuwa tukielekeza nguvu kubwa kwenye sekta ya kilimo ambapo masuala ya kilimo, uvuvi na ufugaji yamepewa umuhimu mkubwa,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema lengo la Serikali ni kutumia hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambapo kwa sasa ni hekta 727,280 ndizo zinazotumika huku hekta milioni 28.6 zikiwa bado zinahitaji kuendelezwa.

MAAGIZO KILIMO, MIFUGO

Katika eneo la umwagiliaji ameagiza wizara kutoza ada watumiaji wa skimu za umwagiliaji ili kusaidia kuzitunza na kuziendeleza.

“Kuna visima 68,000 vinakwenda kuchimbwa kwenye mashamba ya wakulima lakini kuna skimu nyingi ambazo serikali tunazijenga.

“Skimu moja ikijengwa ichangie kujengwa kwa skimu nyingine kupitia ada ndogondogo ambazo wakulima watachangia,” amesema Rais Samia.

Ametoa wito kwa maofisa ugani kuhakikisha wanakaa kwenye vituo walivyopangiwa ili kuwasaidia wakulima, wafugaji na wavuvi kwa kuwapatia utaalam na mbinu za kisasa za uzalishaji.

Kuhusu mbolea ameagiza kupitiwa upya kwa bei ili kumpunguzia mzigo mkulima.

“Nakumbuka bei za mwisho mwaka jana zilifika Sh 70,000, mara hii umekwenda mpaka Sh 85,000 ikiwa ni gharama ya kufikisha mbolea kwa wakulima, nikuagize (Waziri wa Kilimo) kaa na waziri wa fedha uone mtakapoweza kukata gharama za usambazaji…mnaweza mkaenda mpaka 80,000 ile tano (Sh 5,000) itoe.

“Sisi tuchangie, wakulima wachangie lakini mbolea ifike, tusimtwike mzigo mkubwa sana mkulima kwahiyo naomba mkazitazame bei za mbolea,” amesema Rais Samia.

Eneo lingine ni viuatilifu ambapo ameiagiza wizara ya kilimo kuwaunga mkono wawekezaji wa ndani ili wazalishe na kufanya utafiti zaidi.

“Kuna viuatilifu ambavyo vimezalishwa na mtaalam wa ndani na ameshavijaribu kwa wakulima wa nyanya, mahindi na pamba kupambana na wadudu wabaya…lalamiko lake ni kuwa Serikali tunaagiza viuatilifu nje.

“Ingawa vya nje tunapata ‘certification’ lakini mara kadhaa tumekuwa tukilia na viuatilifu feki. Hivi vya ndani naomba muwasimamie muwape fursa waweze kujiendeleza vizuri,” amesema Rais Samia.

Kuhusu uuzaji mazao nje ya nchi ameitaka wizara ya kilimo kwa kushirikiana na Tamisemi, TRA na Uhamiaji waweke mfumo wa pamoja kusimamia biashara hiyo ili wakulima wanufaike.

“Sasa hivi wakulima hamna ruhusa ya kuuza mazao nje bila kuwa na mfumo wowote wa kiserikali,” amesema.

Eneo la ushirika amesema anataka vyama vinavyoweza kumsaidia na sio kumnyonya mkulima.

Rais Samia ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ijipange kujenga nyumba za kulala mifugo kwa kuhakikisha miundombinu inawekwa na kuwa tayari kupokea wanyama wanaokuja kunenepeshwa.

MAJIBU YA MAOMBI

Rais Samia ameahidi kulipa fidia Sh bilioni 26.6 kwa wananchi wanaotakiwa kuhamishwa katika eneo la Mbarali mapema mwezi ujao na kumtaka Waziri wa Ardhi kujipanga kwa zoezi hilo.

Aidha amesema suala la usafri wa ndege kutoka Mbeya – Dodoma litafanyiwa kazi sambamba na ujenzi wa kilomita 20 za barabara za ndani ya jiji la Mbeya.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, ameiomba Serikali kujenga bandari kavu kwa ajili ya mkoa huo na Songwe kwani kunapotokea mgomo katika eneo la Tunduma kunakuwa na changamoto kubwa.

Maonesho ya Nanenane 2023 yameongozwa na kaulimbiu inayosema ‘Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula’.

Mwakani maonesho na Nanenane Kitaifa yatafanyika jijini Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles