23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 9, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi St. Mathew wahamasishwa kujifunza Kichina

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari St. Mathew iliyopo Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani wamehamasishwa kujifunza lugha ya Kichina ili kupata fursa zaidi za kujiendeleza kimasomo.

Shule hiyo imekuwa ikifundisha lugha ya Kichina tangu mwaka 2016 na hadi sasa wanafunzi 100 wamenufaika kwa na wengine wamepata ufadhili wa masomo nchini China.

Hayo yamesemwa Aprili 26,2024 na Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucious ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inayofundisha lugha ya Kichina (CI), Profesa Zhang Xiaozhen, wakati akikabidhi msaada wa vitabu 100 kwa wanafunzi wa shule hiyo ili kujifunza lugha ya Kichina.

Msaada huo umetolewa kwa ushirikiano wa Kampuni ya Ujenzi inayomilikiwa na Serikali ya China (CCCC) na CI.

“Kuna hatua sita za kujifunza lugha ya Kichina na mtu anayefikia hatua ya tatu anaweza kuomba ufadhili wa kwenda kusoma China,” amesema Profesa Xiaozhen.

Mmoja wa wanafunzi wanaosoma lugha ya Kichina shuleni hapo, Rahel Njovu wa kidato cha kwanza, amesema amevutiwa kujifunza ili aweze kuwa na uwanda mpana wa kuelewa lugha za mataifa mbalimbali. Mkuu wa Shule ya Sekondari St. Mathew, Joseph Nalaila, amesema kutokana na utandawazi ulioko duniani hivi sasa ili mtoto aweze kufanikiwa ni vema akajifunza lugha mbalimbali ikiwemo ya Kichina.

“China ni kati ya nchi zinazokua kwa kasi kiuchumi na kibiashara na lugha ya Kichina inatumika sana hivyo, tumeona watoto wetu ili waweze kufanikiwa zaidi katika maisha yao, wanasoma masomo ya darasani kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita pamoja na hayo wanasoma lugha ya Kichina. Tulianza mwaka 2016 mpaka sasa katika miaka hii minane tuna mafanikio makubwa.

“Watoto 100 wamenufaika kwa kujifunza lugha ya Kichina na wengine wamepata ufadhili wa kusoma China, wengine ni wafanyabiashara wakubwa wanakwenda China na kurudi…tumeona lugha ya Kichina ina mafanikio,” amesema Mwalimu Nalaila.

Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya Ujenzi inayomilikiwa na Serikali ya China (CCCC), Li Yu Liang (Wapili kushoto), akimkabidhi kitabu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya St. Mathew, Joseph Nalaila, baada ya kutoa msaada wa vitabu kwa wanafunzi wa shule hiyo waweze kujifunza Kichina. Kushoto ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucious ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inayofundisha lugha ya Kichina (CI), Profesa, Zhang Xiaozhen.

Mkurugenzi wa Shule ya St. Mathew, Peter Mutembei, amesema wameweka nguvu kubwa kuhakikisha wanafunzi kuanzia shule ya msingi hadi sekondari wanafundishwa lugha ya Kichina kwa ufasaha ili kuwawezesha kuwa washindani katika dunia ya sasa.

“Tunahakikisha tunatafuta fursa zozote ambazo zipo zitakazowawezesha watoto wetu kufanikiwa katika ulimwengu wa sasa na mojawapo ni kufahamu Kichina. Huwezi kukwepa lugha ya Kichina kutokana na namna walivyowekeza katika dunia ya sasa,” amesema Mutembei.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles