26.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

Makala: Je Marekani inaelekea mwisho wa zama zake kama Taifa lenye nguvu zaidi duniani?

Haijalishi ni wakati mgumu kiasi gani, lakini lazima wakati huo utapita ndivyo dunia ilivyo, zimepita nyakati ngumu nyingi, wamekuwepo watu wenye nguvu wengi lakini nyakati zao zilipita na tawala zao zilianguka.

Ipo mifano mingi alikuwepo Ramses aliyekuwa Farao kwenye ufalme wa Misri ambae utawala wake ndiyo uliokuwa wa kuogopwa zaidi kwa sababu ya ukatili, ndiyo mtawala aliyesababisha Mungu akaipiga Misri kwa mapigo kumi kutokana na moyo mgumu aliokuwanao Farao huyo kama tulivyosoma kwenye vitabu vya dini lakini pamoja na ukatili na moyo mgumu aliokuwanao Farao Ramses ilifika wakati utawala wake ulifika mwisho.

Augustus wa Roma alieifanya Roman empire kuwa na nguvu duniani lakini wakati ulifika Roman empire ikaanguka.

Pia ulikuwepo utawala wenye nguvu wa Macedonia ukiongozwa na Alexander the Great lakini ulipofika muda utawala huo ulianguka.

Ilikuepo Ottoman empire ikiongozwa na Suleyman the magnificent lakini nayo ilifikia mwisho wake.

Ukija Afrika nako pia zilikuepo tawala mbali mbali zilizokuwa na nguvu lakini nazo pia zilifikia mwisho, alikuepo Mansa Musa wa Mali empire lakini pia Menelik wa kwanza kwa upande wa ufalme wa Ethiopia. Hiyo yote ni kuonyesha kwamba hakuna utawala utakaodumu milele.

Sasa kwanini nimeanza na kuelezea swala la nyakati? Ni wazi kwamba kil utawala una wakati wake duniani na hakuna utawala ambao uliamua kuanguka bali kila utawala ulikuwa na lengo la kutawala milele hakuna anayependa kuachia madaraka kupoteza nguvu, mamlaka, utajiri na ushawishi kwa watu na ndio sababu kwenye kuanguka utawala wowote ule kulienda sambamba na kupotea kwa maisha ya watu wengi.

Ni wazi kwamba kuingia na kutoka kwa utawala wowote lazima kuhusishe umwagaji damu hata kwenye maandiko matakatifu kabla Joshua hajawaingiza waisraeli kwenye nchi ya Kanaani alipigana vita kuuondoa utawala uliokuepo.

Dunia imekuwa ikipitia mabadiliko mbalimbali kutokana na tawala/utawala uliokuepo na mahitaji ya ulimwengu kwa wakati huo. Mara nyingi mabadiliko yanapotokea duniani huwa ni kutokana na kuishiwa uvumilivu kwa tabaka linalotawaliwa.

Tabaka la watawala linapokaa muda mrefu kwenye utawala linaanza kujisahau na kufikiri tabaka linalotawaliwa halina nguvu ya kuweza kuangusha utawala hivyo hupuuza mahitaji na haki kwa tabaka la watu masikini.

Tukirejea kwenye historia tunaona kwamba zile tawala kubwa zilzoitawala dunia zilianguka kutokana na ukandamizaji wa haki kwa tabaka la chini. Kwa mfano Roman Empire ilianguka kutokana na kuishiwa uvumilivu kwa tabaka la watawaliwa dhidi ya utawala wa mabavu wa Roma kama ilivyokuwa pia kwa Ottoman empire.

Karne za hivi karibuni kumekuwa na mabadiliko kutoka kwenye tawala za kifalme kwenda kwenye tawala za kidemokrasia baadhi ya mataifa yalitoka kwenye tawala za kifalme kufanya umma uwe na nguvu ya kufanya maamuzi.

Mapinduzi ya Uingereza ya mwaka 1689 yalitokana na ufalme wa Uingereza kukandamiza tabaka la watawaliwa kama ilivyotokea kwa mapinduzi ya Ufaransa mwaka 1789 kwa sababu kama hizo.

Baada ya mapinduzi ya Uingereza ilifanikiwa kuwa taifa lenye nguvu za kiuchumi na kufanikiwa kumiliki makoloni ambayo yalikuwa yakizalisha rasilimali nyingi kwa ajili ya kuustawisha uchumi wa Uingereza.

Huo ndio ulikuwa wakati ambao Uingereza lilikuwa taifa lenye nguvu zaidi duniani kwenye karne ya 18 mpaka mwanzoni kwa karne ya 20 kabla ya vita kuu ya kwanza ya dunia, takribani nchi 56 zimewahi kutawaliwa na Uingereza.

Baada ya kuwa taifa lenye uchumi mkubwa zaidi duniani kwa takribani karne mbili hatimaye wakati wa kuanguka kwa taifa la Uingereza kama taifa kubwa zaidi ulifika na ndipo uchumi wa taifa hilo uliathiriwa kwa kiasi kikubwa na vita kuu ya dunia mwaka 1914-1918.

Baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia mataifa mengi yaliathirika kiuchumi biashara zilizorota, ulitokea mtikisiko mkubwa wa kiuchumi hivyo nchi ya Uingereza ilijikita kwenye kuufufua uchumi wake ambao uliathiriwa na vita na ndio ulikuwa mwisho wa taifa la Uingereza kuwa taifa lenye uchumi mkubwa zaidi duniani na nguvu kubwa iliyokuwa nayo ikawa imefika mwisho.

Baada ya wakati wa Uingereza kama taifa lenye nguvu zaidi kufika mwisho likaibuka taifa la Marekani na kuwa taifa lenye nguvu zaidi kiuchumi. Safari ya Marekani haikuwa ya usiku mmoja lilishapitia hatua mbalimbali kwenye ukuaji wa kiuchumi mpaka kufika hapo.

Ikumbukwe kwamba taifa la Marekani lilipata uhuru wake kutoka Uingereza mnamo mwaka 1776 na ndio wakati ambapo taifa hilo lilianza safari yake kuelekea kuwa taifa lenye nguvu zaidi duniani. Sera za kiuchumi zenye tija zilianza kutekelezwa na Marekani na kupiga hatua kubwa hasa kwenye uzalishaji wa kutosheleza kwenye soko la ndani.

Baada ya safari ya muda mrefu hatimaye Marekani imekuwa nchi yenye nguvu zaidi kiuchumi duniani lakini kama ambayo hakuna taifa au utawala utakaotawala milele itafika siku Marekani itaanguka kutoka kwenye nafasi iliyopo na utakuja utawala mwingine.

Baada ya muda mrefu tangu taifa la Marekani kuwa taifa lenye nguvu zaidi kiuchumi na kisiasa duniani vimeanza kujitokeza viashiria vya taifa hilo kupoteza nafasi liliyonayo.

Kama tunavyojua kwamba mabadiliko huwa yanatokana na tabaka la watawaliwa kuchoka kutawaliwa na kukandamizwa na tabaka tawala zimeanza kuonekana ishara kwa matukio yanayoendelea sasa duniani.

Taifa la Marekani limekuwa taifa lisilotosheka kila uchao linatafuta namna ya kupora rasilimali za mataifa mengine kwa namna yoyote. Mataifa mengi yamepoteza rasilimali zake kwa faida ya Marekani na viongozi ambao walidiriki kukataa unyonyaji wa taifa hilo la kibeberu waliishia kuchonganishwa na wananchi kupitia propaganda na hatimaye kuleta machafuko.

Yapo mataifa yaliyoathiriwa na ukoloni mamboleo unaofanywa na Marekani kama Iraq, Afghanistan, Libya pia yapo mataifa ambayo yamewekewa vikwazo vya kiuchumi kwa sababu viongozi wa mataifa hayo hawazifuati sera za kinyonyaji za Marekani kwa mfano Iran, Urusi, Venezuela n.k

Sera ya kujipanua kisiasa (Geopolitics) imesababisha kuna vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine. Tukirejea kwenye miaka ya 1950-1991 kulikuwa na vita baridi kati ya nchi za umoja wa kisovieti (USSR) zikiongozwa na Urusi dhidi ya nchi za umoja wa kujihami za Atlantiki (nchi za magharibi) zikiongozwa na Marekani.

Mwaka 1991 umoja wa nchi za kisoviet ulivunjika hakukuwa tena na USSR, ilipofika 1997 Urusi na nchi za NATO waliingia makubaliano ya namna watakavyokuwa wanashirikiana kuepuka kuibuka kwa migogoro.

Moja ya makubaliano waliyoingia ni kuheshimu mipaka na kutokuingilia mambo ya ndani ya mataifa ya upande wa Ulaya mashariki kujaribu kushawishi kuyaingiza kwenye nchi za NATO kufanya hivyo ni kutishia usalama wa taifa la Urusi.

Pamoja na makubaliano hayo Marekani na washirika wake hawakuheshimu makubaliano hayo badala yake mwaka 1999 mataifa matatu (Jamhuri ya Czech, Hungary na Poland) yaliyokuwa kwenye umoja wa nchi za kisoviet yalijiunga na umoja wa nchi za magharibi.

Kwa maana hiyo Marekani iliendelea kupanua mipaka yake kuelekea iliko nchi ya Urusi jambo ambalo Urusi inaliona kama tishio kwa usalama wake.

Kama nilivyokwisha kueleza mwanzo kwamba tabaka tawaliwa likishindwa kuvumilia mateso yanayosababishwa na watawala kinachofuata ni mabadiliko basi ndio sababu inayofanya taifa la Urusi kuivamia kijeshi Ukraine kwa lengo la kushinikiza kuondolewa kwa mpango wa Ukraine kujiunga na umoja wa NATO.

Kutokana na vita hiyo Marekani imeiwekea Urusi vikwazo vya kiuchumi pamoja na kuzikamata mali za Urusi ambazo ziko kwenye mataifa ya NATO lakini haikuishia hapo Marekani inalazimisha nchi nyingine ziwe upande wake kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Kuyalazimisha mataifa mengine kuwa upande wake ni jambo ambalo halikubaliki na linafanya Marekani inapoteza ushawishi kwa mataifa hayo.

Kwa muelekeo wa vita inayoendelea nchini Ukraine ni wazi kwamba mataifa mengi hayataki kulazimishwa kuhusika na kadiri yanavyolazimishwa na Marekani ndivyo ushawishi wa taifa hilo unazidi kupungua.

Siku chache zilizopita Urusi ilikuwa na mkutano na nchi za Afrika na maitaifa mengi ya Afrika yalishiriki mkutano huo. Moja ya ajenda iliyojadiliwa ni pamoja na ushirikiano kwenye maeneo nyeti ya upatikanaji wa nafaka ambapo Urusi imehadi kuyapa nafaka bila malipo baadhi ya mataifa ya Afrika pia itakuwa ikiziuzia nchi za Afrika nafaka kwa gharama nafuu.

Ajenda nyingine iliyozungumziwa ni ushirikiano kwenye ulinzi na usalama ambapo mataifa ya Afrika yataweza kupata silaha kwa ajili ya ulinzi na usalama wa mipaka hali ambayo itasaidia kupambana na tatizo la ugaidi ambalo limezidi kushamiri kila uchao.

Mkutano huo unaleta matumaini kwa waafrika wengi ambao wamechoka na umasikini wakati mataifa yao yana rasilimali za kutosha, Rais wa Burkina Faso Ibrahim Traore alitoa hotuba iliyowasisimua waafrika wengi na kuonekana kuwa shujaa ajaye baada ya Thomas Sankara nchini humo. Kwenye hotuba yake aligusia matatizo yanayoisumbua Afrika hasa tatizo la ukoloni mamboleo linalosababisha Afrika iendelee kuwa masikini huku rasilimali zake zikiwanufaisha mabepari.

Ingawa Afrika imeonyesha kuchoshwa na inaonekana kuanza kuchukua hatua kujikwamua kutoka kwenye ukoloni mamboleo lakini kuna kazi kubwa ya kufanya kwani mabeberu hawatakubali kupoteza rasilimali walizokuwa wakizipata kirahisi na hawana mbadala wa rasilimali hizo. Viongozi wa Afrika wajiandae kukabiliana na changamoto kwenye uongozi kwani mataifa ya magharibi yana mbinu nyingi za kuhujumu jitihada za viongozi wazalendo wa Afrika.

Waafrika wanatakiwa kuelimishwa wajue adui yao halisi ni nani ili wasirubuniwe na vibaraka watakaotumiwa na mabeberu kutaka kuvuruga nchi za Afrika. Kwa miaka mingi Afrika imekuwa ikiongozwa na vibaraka wa mabeberu ndio sababu Afrika imeendelea kuwa masikini hivyo ni vyema waafrika wote kutambua mbinu zote zinazotumika kupenyeza maslahi ya mabeberu na kuzikabili ili kutowapa nafasi mabeberu kuendelea kuiba rasilimali.

Baadhi ya mbinu wanaozotumia mabeberu ni pamoja na kutufanya tuendelee kuwa tegemezi kwa kutoa mikopo yenye masharti magumu kupitia taasisi walizozianzisha kwa ajili ya kudidimiza uchumi wa Afrika kupitia mikopo kama IMF na World Bank.

Hivyo waafrika tunapaswa kuwa na uhuru wa kiuchumi ili tusiamuliwe namna ya kufanya mambo yetu. Kujiondoa kwenye utegemezi wa kiuchumi kunakuja na maumivu hivyo ni vyema tukapata maumivu kwa muda mfupi ili tujenge uchumi wetu watoto wetu wasikute nchi isiyoweza kujitegemea kwa bajeti yake pamoja na kuwa na miaka zaidi ya sitini tangu kupata uhuru. Hakuna maana ya kuadhimisha kumbukumbu ya kupata uhuru wakati kiuchumi hatuko huru na uhuru wa kweli ni uchumi.

Nasisitiza tena ili kuleta mabadiliko ya kweli lazima tukatae kukandamizwa na mabeberu, wapo waafrika wenzetu watakaokuwa upande wa mabeberu sababu wanatafuta manufaa yao binafsi ni vyema tukawatambua na tusiwaruhusu kutuvuruga tumeshateseka na umasikini kwa muda mrefu kwa sababu ya kuwa na viongozi wasio wazalendo. Kiongozi yeyote wa nchi ya Afrika anyepewa sifa na mabeberu sio kiongozi ambae yuko kwa maslahi ya wananchi wake.

Endapo tutafanikiwa kuwadhibiti wanyonyaji wa rasilimali zetu pamoja na vibaraka wao tutafanikiwa kuuangusha utawala dhalimu wa kinyonyaji unaoongozwa na Marekani na washirika wake na dunia itakuwa huru kila nchi itakuwa huru kujiamulia mambo yake yenyewe bila kuingiliwa. Kwa sasa tunahitaji kuwa na umoja kuliko wakati wowote ule viashiria vya kumshinda adui vimeanza kuonekana kupitia Urusi, ni wakati wa Marekani na washirika wake kuanguka kwa sababu ya uonevu wanaoufanya kwa mataifa mengine.

Mwandishi wa Makala haya ni Davidi Shebughe ambaye anapatikana kwa namba: 0719600872

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles