30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Bodi ya Nafaka yanunua Tani 35,000 za mazao

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Tani 35,000 za mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, mpunga, alizeti na maharage zimenunuliwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko nchini (CPB).

Akizungumza Agosti 7, 2023 na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, John Maige, amesema mwaka huu waliweka malengo ya kutumia Sh bilioni 100 lakini mpaka sasa wametumia Sh bilioni 29.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, John Maige, akionesha bidhaa mbalimbali wanazozalisha kwenye Maonesho ya Nanenane Kitaifa viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.

Amesema wanaendelea na ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima katika vituo vyao mbalimbali vilivyopo Iringa, Arusha, Dodoma, Songea, Sumbawanga na Tunduma.

“Kazi yetu kubwa ni kununua mazao kutoka kwa wakulima, kuyaongezea thamani kisha tunazalisha bidhaa mbalimbali na kuziuza katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesema Maige.

Amesema pia kwenye bodi hiyo kuna fursa mbalimbali zikiwemo za kuuza mazao, uwakala wa kuuza mazao na bidhaa.

“Tunaamini vijana pamoja na wanawake kama kaulimbiu ya Nanenane mwaka huu inavyosema watanufaika na uwepo wa bodi katika maonesho haya na baada ya Nanenane katika ofisi zetu zilizopo katika kanda mbalimbali,” amesema.

Bodi hiyo ina ofisi katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Iringa), Ziwa (Mwanza), Kaskazini (Arusha), Kati (Dodoma) na Mashariki (Dar es Salaam).

“Mwelekeo wetu ni kujiimarisha zaidi katika ufanyaji biashara kwa maana ya ununuzi wa mazao ya wakulima, kuyaongezea thamani na kuyauza katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesema.

Amesema bidhaa wanazozalisha ni bora kwa sababu wanazingatia viwango vya ubora vya Afrika Mashariki na kimataifa kutokana na teknolojia wanazotumia.

“Tuna mitambo ya kisasa inayosindika bidhaa za unga wa mahindi, ngano na mchele. Bidhaa tunazozalisha ni bora kwa watumiaji na zinalinda afya ya walaji,” amesema Maige.

Naye Mkurugenzi wa bodi hiyo, Nicomed Bohay, amesema wanatatua changamoto za masoko ya ndani kwa wakulima.

“Tunanunua nafaka mbalimbali nchi nzima kwahiyo tunatatua changamoto ya soko kwa wakulima wa mahindi, alizeti, mpunga, ngano na nafaka zingine.

“Baada ya kununua tunachakata katika viwanda vyetu vya kisasa vilivyopo maeneo mbalimbali ya nchi na kuuza bidhaa katika maduka ya jumla na rejareja…tunatatua changamoto ya wajasiriamali kupata bidhaa bora,” amesema Bohay.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles