24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia aagiza NBS kufanya Sensa kwa ufanisi

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

RAIS Samia Suluhu Hassan ameiagiza Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kuhakikisha inafanya Sensa ya Watu na Makazi kwa Ufasini mkubwa kwa ajili ya kuisaidia Serikali kufanikisha mipango mbalimbali endelevu.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 14, katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma katika wakati wa uzinduzi wa Mkakati wa Uelimishaji na uhamasishaji wa Sensa ya Watu na Makazi 2022 huku akitoa wito kwa viongozi wa Serikali, Viongozi wa Vyama vya Siasa pamoja na Viongozi wa Dini kuendela kuhamasisha wananchi kwa kutoa elimu ili kushiriki Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti Mwakani.

Amesema lengo la zoezi la Sensa ni kufahamu idadi ya watu mahali walipo, rika lao, makazi, shughuli zao na ubora wa makazi kwani taarifa hizo zitawasaidia kujua idadi ya ongezeko la watu na suala la uhamiaji kutoka Vijijini kuja Mijini hata wanaotoka nje ya nchi na kuwezesha serikali kuandaa mipango ya maendeleo.

“Kupitia mkakati huo, serikali itaweza kufanya maamuzi ya ugawaji rasilimali fedha za kijamii hasa maji, elimu na huduma nyingine kulingana na takwimu sahihi ya idadi ya watu,” amesema Rais Samia.

Katika hatua nyingine Rais Samia amesema kuwa dhamira ya Dodoma kuwa Jiji ipo palepale na Ujenzi wa Ikulu umefikia asilimia 75, ambapo serikali imeanza awamu ya pili ya majengo ya Mawaziri mji wa Serikali Mtumba.

Amesema ujenzi wa miundombinu unaendelea na tayari wamesaini mkataba wa ujenzi wa njia nne na umechelewa kutokana na masuala ya fidia na wametenga kiasi chaSh bilioni 17 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi, Nala ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto ya uhaba wa maji.

Awali, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya sensa ya watu na makazi amesema hatua za uhakiki zimefikia asilimia 45 na watahakikisha zoezi hilo linatekelezeka kwa ufanisi mkubwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba amesema katika suala la sensa zipo jamii zimekuwa zikificha watoto wenye ulemavu hivyo uelimishaji wa sensa ni jambo la muhimu kwa ajili ya maendelo na wizara yake itahakikisha fedha zinapatikana kwa wakati.

“Sisi Wizara tumejiandaa na tayari tumeshatoa ridhaa kuhakikisha jambo hili linafanikiwa tunachohitaji ni kila mmoja ajitokeze kuunga mkono jambo hili,”amesema Dk. Nchemba.

Naye, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Tanzania Bara, Dk. Albina Chuwa, amesema mkakati wa kuelimisha watu na kuhesabiwa ni jambo la msingi ambapo matarajio ni kuhesabu kwa asilimia 100.

“Hatuna shaka na serikali yako, tuna utashi wa kisiasa katika hili na tupo tayari kwa nguvu zote kupokea maagizo yako,”amesema Dk. Chuwa.

Naye, Kamisaa  wa Sensa Tanzania Bara ambaye pia ni Spika Mstaafu, Anne Makinda amesema Sensa hiyo ni shirikishi ambapo kwa mwaka 2022 itafanyika kuanzia ngazi ya kitongoji.

“Sensa itasaidia kujua tupo wangapi, na ni shirikishi itaanzia katika vitongoji mpaka katika Sheha kwa upande wa Zanzibar,”amesema Makinda.

Kwa upande wake  Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Balozi Mohammed Haji Hamza amesema kuwa sensa ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi ambapo amesema watahakikisha mkakati huo unatekelezwa ipasavyo kwa kila mmoja kuhesabiwa.

Mtakwimu Mkuu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mayasa Mahfoudh Mwinyi amesema takwimu zenye ubora mwaka 2022 zitakusanywa kwa wakati ambapo tayari maandalizi yameshafanyika asilimia 90.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles