Na Ramadhan Hassan,Dodoma
WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema jamii ina wajibu wa kuhakikisha inawalea vizuri na kuwaondoa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Septemba 14,2021 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. John Jingu wakati akifunga kikao cha kujadili na kuweka mikakati ya kushughulikia tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.
Dk. Jingu pia ametoa vitendea kazi ambayo ni miongozo ya sheria mbalimbali ya jinsi ya kushughulikia tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kwa Makatibu Tawala wa Mikoa nchini, Makamanda wa Polisi na wadau mbalimbali.
Amesema Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na wadau mbalimbali wanawajibu wa kuhakikisha inaondoa tatizo la watoto wa mitaani na wanaofanya kazi mitaani.
“Tutafute mwarobaini wakiendelea kuwepo kule hatuwatendei haki tuna kila sababu ya kuwalea na kuwaondoa mtaani. Nafurahi tumezitendea haki siku mbili ambazo tulikuwa humu kwani kila Taasisi,Idara na NGÓS zimetoa maazimio ya nini kifanyike,”amesema Dk. Jingu.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo amewatataka washiriki wa kikao hicho kwenda kuyafanya waliyokubaliana kwa vitendo ili kuondoa tatizo la watoto wanaoishi mitaani na kufanya kazi mitaani.
“Nitawaomba twende tukayatekeleze yale tuliyoyazungumza tukienda kuyatekeleza tutakuwa tunaitendea haki kumbukeni mtaa hauzai mtoto,”amesema.
Katibu Mkuu huyo amesema wanawajibu wa kutoa elimu kwa wananchi ili kupunguza watoto wa mitaani ikiwa ni pamoja na kufuata sheria kwa wale ambao wamekuwa wagumu kuelewa.
“Tukafanye kampeni kubwa tunajua sio wote wataelewa hivyo nendeni mkasimamie sheria pia tukafanye kazi kama timu ili kufanikisha haya mambo.Pia tukafanye kazi kimtandao,”amesema.