24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Mwinyi ameleta mageuzi Zanzibar-Wadau

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WADAU wa nyanja mbalimbali nchini wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapunduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa anamna ambavyo ameleta mageuzi visiwani humo ikiwamo kudumisha Demoktrasia.

Wadau hao wametoa pongezi hizo wakati wakichangia mada katika Mdahalo wa Tathimini ya Uongozi wa Dk. Hussein Ali Mwinyi katika Demokrasia Zanzibar na kudumisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa, uliofanyika kwa njia ya mtandao wa Zoom kwa Uratibu wa Watch Tanzania, Novemba 19, mwaka huu.

Ikumbukwe kuwa pongezi hizo zinakuja ikiwa ni miaka miwili tu imepita tangu Dk. Mwinyi alipochaguliwa na Wazanzibar kuwa Rais wa Nane wa Visiwa hivyo.

Akichangia mjadala huo Mwanasiasa Mkongwe kutoka visiwani humo, Baraka Shamte amesema kuwa Rais Mwinyi amejitahidi kuhubiri juu ya Umoja na Kudumisha Amani baina ya Wazanzibar licha ya changamoto za hapa na pale.

“Rais Dk. Mwinyi amejitahidi kuhubili sana kuhusu Umoja na kudumisha Amani baina ya Wazanzibarlicha ya vipingamizi vidogo vidogo ila kwa juhudi ya rais wetu na wasaidizi wake nchi imefanikiwa kuwa na amani na utulivu.

“Pia amewasaidia sana wajasiriamali wadogo wadogo hasa wakulima wa mwani ameweza kuwapa vifaa mbalimbali na bei za kuuza zao hilo kuwa nzuri kuliko hapo mwanzo, hivyo haya ni mambo ya kupongezwa kwani ameweza kuyatekeleza ndani ya kipindi hiki kifupi cha uongozi wake,” amesema Shamte.

Upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir amesema kuwa Rais Mwinyi amefanya kazi kubwa katika kuhakikisha Wazanzibar wanapata maendeleo hukua kihimiza Vyama vya Siasa kuunga mkono juhudi hizo.

“Mimi nachukua fursa hii kumpongeza Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ili kuhakikisha Wazanzibar wanapata Maendeleo, Wito wangu kwake aendelee kutekeleza dharma yake njema kwa Wazanzibar.

“Sisi vyama vya Siasa tunapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha tunaunganisha jamii na si kuleta mtafuruku kwa jamii, kinapotokea chama kimeenda kinyume basi wanapashwa kujitokeza kuomba radhi kinyume na hapo chama hicho kitaonesha kwa jamii namna kilivyokosa muelekeo wa kuwa chama cha kisiasa,” amesema Ameir.

Leila Ngozi ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, amesema kuwa: “Kumekuwa na kasumba ya vyama vya upinzani wakiutwa jina hilo basi kunakuwa na uadui kati ya chama tawala na vyama pinzani, hii haipo sawa vyama vya upinzani vipo nchini kikatiba sio kwa ajili ya kuwa adui bali ni wasaidizi wa Serikali pale ambapo jicho la serikali halioni vizuri.

“Bahati nzuri mwenye macho haambiwi tazama kila kitu kipo wazi katika maendeleo yanaonekana, uchumi unaimarika achilia mbali changamoto za kidunia ya vita na magonjwa,” amesema Laila.

Juma Khatibu kutoka Chama cha ADATADEA amesema kuwa upinzani wa vyama sio uadui, badala yake nikuweza kuisaidia serikali pale ambapo inapotoa ahadi kwa wananchi wake na kuisaidia kuikumbusha na sio kuitusi kama viongozi wa serikali hasa vyama pinzani wanavyofanya.

“Pamoja na changamoto zote za kidunia Rais Mwinyi amefanikiwa kuiweka nchi katika hali ya umoja, amani na utulivu pia kuinyanyua Zanzibar kiuchumi, hili ni jambo jema na lakupongeza kabisa,” amesema Khatibu.

Amedhibiti Ukatili

Mweenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania(TAMWA), Joyce Shebe amesema kuwa awali kulikuwa na changamoto ya watoto wa kike kubakwa na kulawitiwa jambo ambalo lilikuwa kero visiwani humo lakini kwa sasa limedhibitiwa.

“Hapo nyuma watoto wa kike kubakwa na kulawitiwa ilikuwa ni kero kubwa sana hivi sasa tatizo hili halipo tena hii ni juhudi za Mhe. Rais kutetea na kuwa makini katika kulitafutia suhulu hii tatizo la ubakaji na ulawiti.

“Rais Mwinyi alisema tangu mwanzo kwamba atashughulikia hili tatizo la ubakaji na ulawiti ndio maana alianzisha mahakama maalum ambayo haina zamana kwa mtu ambaye atabainika amehusika moja kwa moja kufufanya kitendo hicho cha ukatili,” amesema Shebe.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TEF), Deodatus Balile amesema kupitia mikutano ya waandishi wa habari na Rais ilimfanya rais kwenda kojani ambako hakuwahi kwenda kiongozi Mkuu wa Nchi kwa kipindi cha miaka 30 na zaidi lakini Rais Mwinyi amefanikiwa kwenda na kuwasikiliza wananchi wale na kutatua changamoto zao.

“Rais Mwinyi alipoingia madarakani ameweza kurudisha vikao vya kila mwezi yaani Rais kukutana na wahariri na waandishi wa habari pale ikulu na kila mara tukishiriki hii mikutano tunapata fursa ya kumfikishia moja kwa moja hoja kutoka kwa wananchi,” amesema Balile.

Mwanahabari na Mtangazaji Juma Mohammed akichangia mada katika mdahalo huo amesema kuwa upinzani wa vyama sio uadui, upinzani nikuweza kuisaidia serikali pale ambapo inapotoa ahadi kwa wananchi wake na kuisaidia kuikumbusha na sio kuitusi kama viongozi wa vyama pinzani wanavyofanya.

“Pamoja na changamoto zote za kidunia Rais Mwinyi amefanikiwa kuiweka nchi katika hali ya umoja, amani na utulivu pia kuinyanyua Zanzibar kiuchumi, hili ni jambo jema na lakupongeza kabisa,” amesema Mohammed.

Akichangia katika mdahalo huo Wakili wa Kujitegemea, Hassani Kijogoo amesesema kuwa wanamshukuru Rais Mwinyi kwa kujitahidi kushirikisha vijana katika maslahi ya utawala bora.

“Katika teuzi nyingi tunazoziona tunamwona rais anajitahidi kuchagua vijana zaidi ndio maana kuna kauli huwa anapenda kusema kwamba vijana ni taifa la leo.

“Mheshimiwa Rais ametengeneza mazingira sahihi ya kumsikiliza wananchi kutoka kila mahali, anatumia njia mbalimbali kuwafikia watu wake ikiwemo mikutano ya hadhara, mikutano ya ndani, mitandao ya kijamii na kupitia wasaidizi wake,” amesema Kijogoo.

Akihitimisha mdahalo huo, Mwenyekiti wa Jitegemee Co. Ltd, Joseph Meza amesema kuwa kwa mujibu wa Kanuni na Sheria za Nchi Rais ndiye kiongozi Mkuu wa Nchi hivyo ukiwa na jambo lolote katika kumshauri unapaswa kufuata kanuni na taratibu kinyume chake ni kumvunjia heshima na kukiuka taratibu za nchi,”

“Tabia zetu ni kuheshimu viongozi na watu wazima na kama unamshauri ni kupitia taratibu za kiheshima sio kutoa amri mitandaoni,” amesema Meza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles