24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS MAGUFULI AVUNJA MWIKO WA SAFARI NJE


NA EVANS MAGEGE – Dar es Salaam

HATIMAE Rais Dk. John Magufuli amevunja mwiko kwa kusafiri kwenda jijini Addis Ababa, Ethiopia kuhudhuria Mkutano wa 28 wa Baraza Kuu la Umoja wa Afrika (AU).

Safari hiyo inakuwa ni ya kwanza kwa Rais Magufuli kuhudhuria mkutano wa kimataifa nje ya nchi tangu aingie madarakani mwaka juzi, ingawa kwa nyakati tofauti amewahi kufanya ziara za kikazi katika mataifa ya Rwanda, Uganda na Kenya.

Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli amekuwa akituma wawakilishi katika shughuli na mikutano mbalimbali ya kimataifa nje ya nchi.

Katika mikutano kama hiyo mara kadhaa Rais Magufuli amekuwa akiwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Agustine Mahiga, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Samia amewahi kumwakilisha Rais Magufuli katika mikutano iliyofanyika nchi za Rwanda, Ethiopia, Papua New Guinea, Swaziland, Zambia na Afrika Kusini huku Waziri Mkuu Majaliwa akimwakilisha katika mikutano iliyofanyika Botswana, Uingereza na Kenya.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, alilithibitishia MTANZANIA Jumapili jana kuwapo kwa safari hiyo na kwa muda wa saa 10: 53 aliopigiwa simu, alisema alikuwa akiandaa taarifa kwa vyombo vya habari.

Katika mkutano huo, Rais Magufuli anaungana na  marais kutoka nchi wanachama wa AU ambao watafanya vikao kesho na keshokutwa (Januari 30-31).

Hadi tunakwenda mitamboni, Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Uhuru Kenyatta wa Kenya walikuwa wamekwishawasili jijini Addis Ababa.

Mkutano huo unatajwa kuwa na ajenda mbalimbali, ikiwamo uchaguzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika na makamu wake pamoja na maombi ya Serikali ya Morocco ya kutaka kurejea katika umoja huo.

Kuhusu ajenda ya Morocco, taarifa aliyotolewa  Alhamisi iliyopita na Mwenyekiti wa Tume ya Afrika anayemaliza muda wake, Dk. Nkosazana Zuma,  inatanabaisha kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Salaheddine Mezouar amewasili katika mkutano huo kwa utetezi wa ajenda ya taifa lao kurejeshwa AU.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa hatima ya maombi ya Morocco kurudishwa AU itajulikana Januari 30 au 31.

Itakumbukwa Mfalme wa Morocco, Mohammed VI alifanya ziara hapa nchini Oktoba 23, mwaka jana huku baadhi ya wachambuzi wakidai kuwa moja ya ajenda zake ilikuwa ni kuishawishi Tanzania iunge mkono uamuzi wake wa kurudi AU.

Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano huo ambayo imechapishwa kwenye tovuti ya AU, uchaguzi wa Mwenyekiti wa tume ya umoja huo na makamu wake utafanyika kesho ambapo matokeo yatatajwa keshokutwa.

Wagombea wanaowania nafasi hiyo ni Pelonomi Moitoi kutoka Botswana, Moussa Mahamati (Chad), Agapito Mokuy (Equatorial Guinea), Balozi Dk. Amina Mohammed (Kenya) na Dk. Abdoulaye Bathily (Senegal).

Duru zaidi za mambo zinadai kwamba uchaguzi huo unafanyika wakati kukiwa na ushindani mkali wa kanda zinazotokana na Jumuiya za Maendeleo kwa nchi wanachama wa AU.

Kwamba, Moitoi anaungwa mkono na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wakati Balozi Dk. Amina akiungwa mkono na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashari (EAC).

Kwa upande wake, Mahamati, Mokuy na Dk. Bathily wanaungwa mkono na Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS).

Pia ushindani huo unachochewa zaidi na msukumo wa nchi zinazozungumzaKiingereza(Anglophone) na zile zinazozungumza Kifaransa (Francophone).

Wakati nchi za Francophone zinapigania kutwaa kiti hicho, zile za Anglophone zikipambana kutetea.

RATIBA

Ratiba inaonyesha kwamba Mkutano wa Baraza Kuu utafunguliwa na mwenyekiti wa baraza hilo ambaye anamaliza muda wake, Idriss Deby.

Baada ya ufunguzi, Mwenyekiti wa Tume ya Afrika ambaye naye atakuwa anamaliza muda wake, Dk. Nkosazana Zuma atahutubia mkutano huo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk. Antonio Guterres na Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas watafuatia kuhutubia mkutano huo.

Baada ya hotuba za viongozi hao, yatatangazwa matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Afrika ambapo mshindi atapewa nafasi ya kuhutubia baraza hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles