25.5 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

BABY MADAHA: BANGI HAPANA AISEE ILA MITUNGI SANA TU

Na JOHANES RESPICHIUS

SHINDANO la kusaka vipaji vya kuimba la Bongo Star Search (BSS) ni miongoni mwa machimbo muhimu yaliyozalisha madini muhimu kwenye Bongo Fleva, wasanii kama Peter Msechu, Walter Chilambo, Kala Jeremiah, Kayumba  na wengine wengi.

Swaggaz linatua pande za Kinondoni maeneo ya Mbezi Garden na kukutana na staa wa singo ya Amore, Baby Joseph Madaha ambaye tulianza kumfahamu mwaka 2007 baada ya kushiriki shindano hilo la Bongo Star Search.

Baby Madaha ni mtamu kwenye muziki akitamba na nyimbo kama Nimezama, Summer Holiday, Nawaponda na Mahama Niue. Ukimleta kwenye filamu nako ameweka heshima ya aina yake pale aliposhiriki kwenye filamu za Misukosuko, Ray Of Hope, Tifu la Mwaka na Blessed by God.

Hivi sasa yeye ni msanii wa kutegemewa ndani ya kundi la Scorpion Girls akiwa na Isabela Mpanda ‘Bela’. Kundi hilo lilikuwa na wasanii watatu, lakini sasa wamebaki wawili baada ya mwenzao Miriam Jolwa ‘Kabula’ kujitoa. Kwa sasa kundi hilo linatamba kwa wimbo wao wa ‘Marioo’. Karibu umfahamu zaidi.

UNYUNYU, ‘MAKE UP’ HAKOSI

Baby Madaha anasema kupendeza kwake ni lazima, amekuwa mlevi wa kujipodoa akiwa nyumbani au akiwa ana mtoko, muda mwingine akitaka kulala huoga na kujipaka Make Up kitu kinachompa furaha muda wote.

Siyo kujipodoa pekee, Baby anahusudu sana unyunyu wenye manukato ya kunukia na siyo jambo la ajabu kwake kujinyunyiza pafyumu za aina tatu tofauti.

ANAONGEA LUGHA KIBAO

Wakati mastaa wengi wakipigwa chenga na lugha ya kingereza hasa wanapokutana na watangazaji wa vituo vikubwa vya redio na runinga, Baby Madaha yupo tofauti, mrembo huyu anaongea lugha nne ambazo ni Kiswahili, Kingereza, Kireno na Kihispania.

BANGI VEPEE?

Amekuwa akihisiwa kuwa ni mmoja ya mastaa wanaotumia dawa za kulevya kama vile bangi, Baby Madaha anasema yeye ni mwendo wa mitungi tu na hajawahi kutumia kabisa kutumia mihadarati yoyote.

 “Watu wanajua natumia bangi jambo ambalo siyo la kweli, sijawahi kuvuta wala kutumia aina yoyote ya dawa za kulevya, mimi kilevi changu ni bia tu hata kreti naweza kumaliza, lakini nazima nikipewa kitoti kimoja cha Whisky,” anasema Madaha.

ASILI YA SCORPION GIRLS

Huyu ni mwanzilishi wa kundi hili la Scorpion, Baby Madaha anasema asili ya jina hilo limetokana na nyota yake ya Ng’e kufuatia kuzaliwa mwezi Novemba.

“Wazo la kuunda kundi lilitokea siku ya kumbukumbu yangu ya kuzaliwa hivyo kwa pamoja tukakubaliana kundi letu tuliite Scorpion, kwenye kumbi mbalimbali tulizoingia tulianza kutambulika hivyo,” anasema Baby.

MAPENZI SI SANA!

Kwenye suala zima la mapenzi, Baby Madaha anasema hakuna anayeweza kumzingua kwani yeye ni mchezaji mzuri wa Yoga hivyo kidume atakayetaka kumtibua basi ni lazima ajipange.

“Huwa siwaweki wazi wapenzi wangu hata tukiachana huwa ni kimya kimya ndiyo maana naona ni jambo zuri kumficha mpenzi wangu, mapenzi si jambo muhimu, kitu cha kwanza ni Mungu, kazi, hela kisha mapenzi yanafuata,” anasema.

ALIFUNGA NDOA DUBAI?

Mwaka uliopita kulikuwa na habari za mwanadada huyu kuolewa nchini Dubai, Baby Madaha anasema kwenye maisha yake hajawahi kuolewa na mpaka sasa hajabahatika kuwa na mtoto.

 “Zile taarifa niliziona na niliamua kuacha watu waongee ila ukweli ni kwamba zile picha nilizipiga wakati nakula bata nchini Dubai, sijaolewa na sina mpenzi mzungu, mpenzi wangu ni mtanzania ila siwezi kumtaja kwasababu nitakuwa simtendei haki kulingana na shughuli zake hastaili kusemwa kwenye vyombo vya habari,” anasema Baby Madaha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles