23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Dk. Mwinyi aahidi Zanzibar ya ‘Uchumi wa Bluu’

Na MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameahidi kuijenga Zanzibar mpya kwa kupitia uchumi wa kisasa wa Buluu (Blue Economy).

Dk Mwinyi alitoa ahadi hiyo jana, katika hotuba yake ya uzinduzi wa Baraza la 10 la Wawakilishi lililofanyika huko katika ukumbi wa Baraza hilo Chukwani, nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.

Hafla ahiyo ilihudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Zanzibar Amani Abeid Karume, Dk. Ali Mohammed Shein, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Maryam Mwinyi, wake wa Marais wastaafu, mabalozi na viongozi wengineo.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Mwinyi alisema kuwa moja ya ahadi yake kubwa aliyoitoa kwa wananchi na ambayo imeelezwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kujenga uchumi wa kisasa wa Buluu (Blue Economy).

Alisema kuwa Uchumi wa Buluu ama uchumi wa bahari unafungamanisha kwa pamoja sekta za uvuvi, ufugaji samaki, ujenzi wa viwanda vya samaki, ukulima wa mwani, uchimbaji wa mafuta na gesi, matumizi bora ya rasilimali mbali mbali za bahari pamoja na shughuli za utalii wa fukwe na michezo ya baharini.

Aliongeza kuwa uchumi wa Buluu haukamiliki bila ya kuwepo kwa Bandari za kisasa zenye ufanisi wa hali ya juu.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Mwinyi alieleza kuwa miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya utawala bora ni rushwa, uzembe, kukosa uwajibikaji, kutofuata sheria na kukiukwa kwa maadili hivyo, alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itakabiliana ipasavyo na vitendo vyote vinavyoathiri utekelezaji wa misingi ya utawala bora.

Alirejea ahadi yake kwa wananchi mbele ya Baraza hilo kwamba atapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi wala kuoneana muhali na kuwaomba Wawakilishi na Wananchi wote wamuunge mkono wakati wa mapambano hayo.

“Tutashinda vita hii endapo wananchi pia watatuunga mkono. Sina shaka kuwa kwa vile wao, kwa wingi wao, wanachukia rushwa na ufisadi, watakuwa tayari kutoa ushirikiano wao katika mapambano haya. Ni matumaini yangu pia vyombo husika katika jambo hili vitatekeleza wajibu wao,” alisema.

Katika hotuba hiyo pia, alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa Chama cha ACT Wazalendo, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Marehemu Abubakar Khamis Bakari ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Katiba na Sheria katika Serikali ya Awamu ya Saba kipindi cha kwanza.

Rais Mwinyi aliweka wazi kuwa kiongozi yoyote atakayemteua kwa mamlaka aliyonayo kikatiba, atamuwajibisha mara moja pindi tu akibaini na kujiridhisha kuwa anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi.

Aliongeza kuwa uteuzi wa viongozi na watendaji katika Serikali yake utazingatia uwezo wa mtu kitaaluma, uwajibikaji na uaminifu.

Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane itasimamia kwa umakini  nidhamu na uwajibikaji wa watumishi wa umma na haitakuwa na muhali kwa mtendaji yoyote ambae hatowajibika katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aliongeza kuwa atakayeshindwa kuwajibika aelewe kuwa atawajibishwa kwani uzembe na ukosefu wa nidhamu kazini huzorotesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwa hivyo, tabia hiyo hatoivumilia. 

Aliwataka viongozi wote atakaowateua katika nafasi mbali mbali wawe wabunifu na waweze kuishauri Serikali juu ya masuala yanayohusu fani na utaalamu wao huku akisisiza kwamba Serikali haitowavumilia viongozi wenye kusubiri kuambiwa kutoka kwake au Serikalini nini wafanye katika kutekeleza majukumu yao.

Akieleza kuhusu sekta ya mafuta na gesi, Rais Mwinyi alisema kwamba Serikali ya Awamu ya Nane itaziimarisha na kuzijengea uwezo wa kitaaluma na nguvukazi Kampuni ya Mafuta Zanzibar (ZPDC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mafuta na Gesi (ZPRA) ili ziweze kuiongoza sekta hiyo muhimu.

Vile vile, alisema kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na Kampuni mbali mbali zenye dhamira njema ya kuwekeza hapa nchini katika sekta hiyo.

Aidha, alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane ina malengo ya kujenga bandari kubwa ya kisasa katika maeneo ya Mangapwani itakayokuwa na sehemu kadhaa za kutolea huduma zikiwemo sehemu za kuhudumia meli zitakazobeba mafuta na gesi, chelezo kwa ajili ya matengenezo ya meli, eneo la kuhudumia meli zinazobeba mizigo na makontena, bandari ya uvuvi pamoja na bandari ya meli za kitalii.

Aligusia kuwepo kwa malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kucheleweshwa mizigo yao bandarini na msongamano wa makontena katika Bandari ya Malindi, vitendo vya rushwa na kukosa uwajibikaji kwa baadhi ya watumishi wa bandarini.

Alielezadhamira ya Serikali ya kuimarisha bandari za Wete na Shumba Mjini na kuendelea na matayarisho ya ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi huko Mangapwani na kuiimarisha bandari ya Mkoani ili iweze kuhudumia meli kubwa kutoka nje moja kwa moja kwa lengo la kunyanyua uchumi na biashara kwa kisiwa cha Pemba.

Alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane  itaongeza nguvu katika upanuzi wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki.

“Tutahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tutaziba mianya ya upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa kuwahudumia wananchi”,alisema Rais Mwinyi.

Aidha, alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane, itaweka mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara ili sekta hizo ziwe na mchango mkubwa zaidi katika kukuza ajira na katika Pato la Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles