30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Misongamano mijini kichocheo ongezeko ugonjwa wa kisukari

Na  AVELINE  KITOMARY, DAR ES SALAAM

INAKADIRIWA  kuwa huenda ongezeko la ugonjwa wa kisukari likawa kubwa zaidi barani Afrika kutokana na kuongezeka kwa misongamano katika miji ya Bara ya hilo.

Hayo yalibainishwa jana na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Homoni katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dk Wolfagang Bernard ikiwa ni kuelekea siku ya kisukari Duniani Novemba 14 kila mwaka.

Dk Bernard ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, alisema  takribani miaka 30 iliyopita Dunia ilikuwa na wagonjwa wa kisukari milioni 30 lakini mpaka kufikia sasa, idadi ya wagonjwa inakadiriwa kuwa milioni 463, ambalo ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na ongezeko la watu  Duniani, ambapo awali walikuwa bilioni 4.5 na sasa ni bilioni 8.

“Sasa utaona ongezeko la watu Duniani ni mara mbili, lakini ongezeko la ugonjwa wa kisukari ni zaidi ya mara 150 huu ugonjwa wa kisukari unaongezeka kwa kasi sana na kasi hii ikiendelea makadirio yajayo ni kwamba mwaka 2030 yaani miaka 10 ijayo idadi ya ya watu wenye kisukari duniani itakuwa ni Milioni 600 na  miaka 25 ijayo  mwaka 2045 idadi ya wagonjwa itakuwa milioni 700.

“Kwa Afrika inakadiriwa ongezeko litakuwa kubwa zaidi na sababu kubwa ni  mabadiliko ya maisha ya watu kwamba watu wanahamia Miji ambapo utaona katika miji ya Afrika mikusanyiko  inakuwa kwa kasi sana.

“Sasa mtu  anapohamia mjini kuna baadhi ya shughuli za mwili zinapungua ukubwa kwa Afrika sasa hivi ni milioni 19 huku Tanzania ikiwa na wagojwa milioni 1.5, lakini sasa hawa ni wale wanajulikana kwani wagonjwa wa kisukari hawaoneshi dalili sana,” alibainisha Dk Bernard.

Alisema hata hivyo huenda idadi ya wagonjwa wa kisukari ikawa kubwa zaidi kutokana na wagonjwa wengi kutokugundulika mapema.

“Watu wanaishi na ugonjwa wa kisukari muda mrefu bila kujijua, hawa milioni 1.5 ni wale wanajulikana lakini huenda wasiojulikana wakawa wengi zaidi.

“Kwa hali hii kama hatutapeana taarifa  na hatutachukua tahadhari ongezeko la kisukari Tanzania  na Duniani kwa ujumla linatisha,” alisisitiza.

Dk Bernaed alisema ugonjwa huo usipodhibitiwa unaleta  madhara na inakuwa vigumu kutibika.

“Kwa kadiri sukari inavyoendelea inachoma viungo vya mwili, inapofusha macho, inaua figo, mishipa ya fahamu, mishipa ya damu, ganzi, vidonda na moyo kushindwa kufanya kazi na hayo madhara ni makubwa sana hayawezi kurekebishwa.

Alisema endapo mtu antawahi anaweza kupatiwa matibabu ambayo yatadhibiti madhara hayo kwa kuweka kiwango sawa cha sukari mwilini.

“Ugonjwa huo dawa zake zimepatikana  muda mrefu uliopita kwa wale ambapo kongosho imeharibika wanahitaji insulin hii ni sinadano ambayo anatakiwa mtu kuchomwa mara mbili au tatu kwa siku ili insulin imsaidie kupungza sukari kwenye damu,” alisema.

Daktari huyo alishauri njia ya kuzuia ugonjwa huo kuwa ni mtindo bora wa maisha ikiwemo ulaji wa vyakula vinavyofaa na kufanya mazoezi.

“Njia ya kuzuia ni rahisi kufanya mabadiliko ya mtindo wa maisha kama kupunguza uzito, kufanya mazoezi, kuepuka kula vyakula vyenye sukari kwa wingi,kuepuka kunywa pombe, uvutaji wa sigara.

“Utumiaji wa sukari kwa wingi kama kuongeza sukari kwenye chai,kunywa juisi yenye sukari na mengine unachosha kongosho na itashindwa kukusaidia.

“Tunashauriwa hasa katika wakati huu wa mabadiliko ya maisha ni muhimu  kufanya mazoezi walau dakika 30 kwa siku,” alishauri Dk Bernard.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles