
Lilongwe: Malawi
RAIS Peter Mutharika wa Malawi amelitaka jeshi la polisi nchini humo kumkamata Eric Aniva kwa kujihusisha na tambiko la kusafirisha wasichana wadogo na kufanya nao ngono.
Alitoa agizo hilo kutokanana taarifa zilizotolewa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na kuenea dunia mzima.
Rais Mutharika alisema amechukizwa na yaliofichuliwa katika habari hiyo na ameapa kukabiliana na utamaduni wa aina hiyo.
“Nimeambiwa kuwa ukiukwaji na unyanyasaji huu unafanyika kwa kivuli cha utamaduni ambao mimi nimeona haikubaliki,” alisema Mutharika katika taarifa yake.
Rais pia anataka polisi kuchunguza tukio hilo na kumshitaki mtuhumiwa kwa uovu huo ambao yeye tayari amekiri na watu wote waliohusika katika ukiukwaji wa haki za watoto wawaajibishwe.
Aniva ambaye pia ni muathiriki wa Ukimwi anatoka kusini mwa nchi hiyo.
Mtuhumiwa huyo aliyepewa jina la utani la ‘fisi’ kwa uovu huo atashtakiwa kwa kukiuka haki za watoto.
Aniva (40), analipwa kwa kufanya ngono na wasichana wadogo na kuwatoa ubikira kama tambiko la kuwasafisha.
Mtuhumiwa huyo aliripotiwa kufanya mapenzi na zaidi ya wasichana 100 na kulipwa dola za Marekani 3.9 hadi 6.6 kwa kila binti kwa kufanya nao mapenzi kwa siku tatu kila mmoja.