24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Raia wa Nigeria 51 wameuawa katika maandamano ya amani

LAGOS, NIGERIA

RAIA wa Nigeria wapatao 51 wameuawa katika vurugu zilizozuka nchini humo kufuatia siku kadhaa za maandamano ya amani ya kupinga ukatili wa polisi. 

Aidha askari 11 pia wameuawa na raia wa kawaida 37 wamejeruhiwa katika maandamano hayo. 

Rais Muhammadu Buhari amewalaumu wale aliowaita wahuni kwa machafuko hayo, huku akisisitiza kwamba vikosi vya usalama navyo vilijizuwia kwa kiwango cha juu sana. 

Buhari ameongeza kwamba maandamano hayo yaliyokuwa na nia njema, yametekwa na majambazi walioyaingilia kati. Matamshi hayo ya Buhari yanategemewa kuchochea mivutano zaidi. 

Wanigeria  wengi wamekasirishwa na hotuba ya kitaifa ya Buhari aliyoitoa Alhamisi usiku, kwa kukosa kutaja vitendo vya ukatili vya wanajeshi wake vya kuwafyatulia risasi raia. 

Badala yake Buhari aliwaonya waandamanji dhidi ya kuhujumu usalama wa kitaifa, sheria na utulivu.

Buhari ameonya, serikali yake haitoruhusu mtu au kundi lolote kuvuruga amani ya taifa hilo, na kuwataka waandamanaji kupinga majaribu ya kutumiwa na waasi kuvuruga demokrasia changa ya taifa hilo.

Akizungumza kupitia njia ya televisheni Bukhari amesema kuwa serikali yake haitomvumilia mtu yeyote aliye na lengo la kudhoofisha usalama wa taifa na utulivu pamoja na kwenda kinyume na sheria.

Kulingana na Shirika la Amnesty Internatinal siku ya Jumanne usiku jeshi la polisi liliwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakiimba wimbo wa taifa na kusababisha vifo vya watu 12.

Marekani imelaani machafuko hayo na kile ilichokiita utumiaji wa nguvu kupita kiasi wa jeshi la Nigeria kwa kuwafyatulia risasi waandamanaji wasio na silaha.

Buhari aidha amejibu ukosoaji ambao amepokea kutoka kwa wakuu wa nchi za Kiafrika na viongozi wengine wa ulimwengu na ametaka watafute ukweli wote unaopatikana kabla ya kuchukua msimamo, au kukimbilia kumuhukumu na kutoa matamko ya kumkejeli.

Wakati rais Buhari anaendelea na hotuba yake Wanigeria walio na hasira walifurika katika mitandao ya kijamii kumshutumu.

Usman Okai Austin mmoja wa watumiaji ameandika “Rais Buhari wakati wa hotuba yake amekataa kutambua waliokufa kutokana na mashambulizi ya kijeshi kwa waandamanaji wa Lekki #EndSARS, “

“Kwa hotuba hii, inathibitishwa tuko peke yetu. Roho za kaka na dada zetu waliokufa katika # LekkiMassacre2020 na maeneo mengine kwenye maandamano ya #EndSARS pumzikeni  kwa amani. Inasikitisha, “aliandika Henry Okechukwu.

Machafuko ya ghasia yalizuka siku ya Jumatano huko Lagosna kusababisha uharibifu mkubwa na kuchoma vituo vya polisi, mahakama, vituo vya Televisheni na hoteli,  polisi walipambana kwa hasira na umati wa watu kwa kutumia mabomu ya machozi na risasi.

Katika sehemu nyingine za jiji lenye watu milioni 14 la Lagos, barabara na mitaa na maduka yalikuwa yamefungwa, baada ya amri ya kutotoka nje  kutolewa na serikali ili kuzuia machafuko. 

Huku hayo yakijiri moshi ulionekana ukitoka katika kituo cha kurekebisha tabia cha Ikoyi na milio ya risasi kusikika, Tunde Oguntola.

Mkaazi wa karibu na gereza hilo amesema alisikia milio ya risasi kama askari na maofisa wa polisi walikabiliana na kile kilichoonekana kuwa jaribio la wafungwa kutoroka gerezani.

Msemaji wa polisi Olamuyiwa Adejobi aliliambia Associated Press kwamba gereza lipo chini ya udhibiti, polisi wameingia kusaidia maofisa wa gereza.  

“Maofisa wa polisi kwa sasa wanashika doria katika sehemu kuu za jiji kuhakikisha usalama wa wakaazi.Tafadhali kaeni ndani,” amesema kamanda wa polisi jimbo la Lagos 

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ametaka uchunguzi kuanzishwa mara moja kuhusu vurugu na vikosi vya usalama, ambayo pia imesababisha Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Afrika, Jumuiya ya Ulaya kulaani matukio hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles