26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

PROF. MUHONGO AGOMA KUSAINI LESENI

NA VERONICA SIMBA – DODOMA


WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amekataa kusaini ombi la uhamishaji wa leseni ya uchimbaji wa kati wa madini ya shaba Na. ML 571/2017 kutoka kwa Mtanzania David Stanley Kayongoya kwenda Kampuni ya Mechanized Minerals Supreme Mining Ltd inayomilikiwa na raia kutoka China.

Profesa Muhongo alikataa kusaini leseni hiyo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 0.43 katika eneo la Fufu wilayani Chamwino mkoani Dodoma, baada ya kubaini kuwa Mtanzania anayetaka kuhamishia leseni hiyo kwa raia wa China, hatanufaika kwa kiwango kinachoridhisha.

Akizungumza na wawekezaji mbalimbali wa sekta husika, waliofika Makao Makuu ya wizara mjini Dodoma kusainiwa leseni zao za uwekezaji jana, Profesa Muhongo alisisitiza kuwa ni lazima wawekezaji katika sekta husika wazingatie suala la masilahi ya wananchi na taifa kwa ujumla, wakati wanapotekeleza kazi zao za uwekezaji.

Waziri Muhongo alimwagiza mwekezaji huyo raia wa China kujadiliana kwa mara nyingine na Mtanzania mwenye eneo husika, ili kuhakikisha ananufaika ipasavyo na uwekezaji huo.

“Ili niweze kusaini leseni hii, rudini mezani, mzungumze na kukubaliana ili David aweze kunufaika. Hatuwezi kukubali kuona Watanzania wakidhulumiwa namna hii,” alisema Prof. Muhongo.

Awali, ilielezwa kuwa mkataba wa mauziano ya leseni husika unaonesha kuwa David amepokea kiasi cha Sh milioni 30, ambapo Waziri Muhongo alipotaka kujua endapo kuna manufaa mengine ambayo atapata, alielezwa kuwa ataajiriwa katika kampuni hiyo kama kibarua.

Ili kuhakikisha suala hilo linatekelezwa ipasavyo, Profesa Muhongo alimwagiza Kamishna wa Madini, Benjamin Mchwampaka, kujiridhisha kwa kupokea ahadi za maandishi kutoka kwa mwekezaji yeyote anayeomba leseni, namna ambavyo atazingatia masilahi ya nchi, kabla ya kumpatia leseni anayoomba.

Kwa upande wake, Kamishna Mchwampaka aliahidi kutekeleza agizo hilo la waziri kwa kuwataka wawekezaji hao kuzingatia kanuni na miongozo mbalimbali ya uwekezaji kama inavyobainishwa katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010.

Wawekezaji wengine waliokidhi vigezo na kusainiwa ni pamoja na Salim Mohamed Salum ambaye leseni yake inahusisha uhamishaji wa leseni tatu za uchimbaji wa kati wa madini ya marble Na. ML 566/2016 iliyoko Mumbwi Wilaya ya Handeni, ML 567/2016 iliyoko Ulanga, Morogoro na ML 568/2016 iliyoko Kwenkambala – Handeni mkoani Tanga kwenda Kampuni ya S & T Marble and Mining Ltd.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles