24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Pochettino majanga, Mourinho kicheko

MTZ30ABDUCADO EMMANUEL NA MITANDAO

DIMBA la White Hart Lane linatarajia kuwaka moto kesho saa 9.00 alasiri kwa mchezo wa watani wa jadi wa jiji la London ‘London Derby’, wakati wenyeji Tottenham Hotspur watakapoikaribisha Chelsea katika Ligi Kuu England.

Kuelekea mchezo huo, Kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino, ameanza kuuona mgumu kufuatia timu yake kutopata muda mwingi wa kujiandaa ukilinganisha na Chelsea.

“Tunakabiliana na timu ngumu, katika hali hii Chelsea ambayo inazo siku tatu zaidi za kujiandaa kuliko sisi ambao tunayo moja. Hii inawapa faida wapinzani wetu. Tunatakiwa kukubali kanuni za mchezo, lakini tunahitaji kusema nini ni kweli kuhusu sisi,” alisema Pochettino.

Hiyo inatokana na timu zote hizo kucheza katikati ya wiki hii, Spurs ikicheza juzi dhidi ya Qarabag na kuifunga bao 1-0 kwenye Kombe la Ligi ya Europa na Chelsea ikakipiga na Maccabi Tel Aviv Jumanne iliyopita na kuichapa mabao 4-0 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho, yeye kwa upande wake ameendelea kupatwa na kicheko kufuatia mwenendo mzuri wa timu yake hivi sasa.

“Ni jambo la muhimu na tunafurahia kushinda mechi zetu mbili zilizopita (Norwich City na Maccabi Tel Aviv). Naamini itatuongezea hali ya kujiamini. Ni jambo la muhimu kwa sababu tulicheza mechi nyingi bila ushindi mfululizo. Kufanya hivyo ni jambo zuri.”

Hata hivyo, Chelsea inaweza kuwa kwenye wakati mgumu dhidi ya Spurs kutokana na rekodi bora waliyonayo kwa sasa wakiwa hawajapoteza mechi yoyote ya ligi, toka walipofungwa na Manchester United katika mchezo wa ufunguzi (1-0).

Vile vile Spurs imeimarika hivi sasa baada ya straika wake tegemeo, Harry Kane, kuanza kuonyesha makeke yake ya msimu uliopita kufuatia kuanza vibaya msimu huu mpaka sasa amefunga mabao tisa ndani ya mechi sita zilizopita.

Kane, 22, ana rekodi nzuri dhidi ya Chelsea ikiwa ni baada ya kufunga mabao mawili wakati Spurs ikiwalaza matajiri hao mabao 5-3 msimu uliopita kwenye siku ya Mwaka Mpya.

Kwa upande mwingine, Chelsea imeanza msimu huu vibaya baada ya kufungwa michezo saba kati ya 13 waliyocheza mpaka sasa, matokeo ambayo yamemweka kwenye presha kubwa Mourinho ya kutimuliwa ndani ya kikosi hicho.

Msimu uliopita kwenye mechi zao mbili baina yao zilitengeneza jumla ya mabao 11, hiyo inaonyesha kuwa safu ya ulinzi ilikuwa katika wakati mgumu sana na kutokana na vipaji vya washambuliaji wa pande zote mbili, mabao yanatabiriwa kufungwa leo.

Winga wa Chelsea, Eden Hazard, amefunga mabao kwenye mechi tatu za mwisho dhidi ya Spurs, huku Kane naye akifunga mawili katika mchezo wa mwisho waliokutana.

Uwepo wa wakali Kane, Christian Eriksen, Mousa Dembele na Mkorea Son Heung-min kwenye eneo la ushambuliaji la Spurs, unatarajia kuwaweka kwenye wakati mgumu mabeki wa Chelsea hasa rekodi yao ikionyesha kuwa wameruhusu mabao 23 ndani ya mechi 13 za ligi msimu huu.

TAARIFA ZA KLABU

Spurs itamkosa kiungo wake Dele Alli, ambaye atakuwa akitumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja baada ya kukusanya kadi tano za njano huku pia ikitarajia kuwakosa Erik Lamela, Nabil Bentaleb, Nacer Chadli na Alex Pritchard walio majeruhi.

Chelsea itamkosa nahodha wake, John Terry, aliyeumia kwenye mchezo uliopita dhidi Maccabi Tel Aviv ya Israel.

REKODI ZAO

Chelsea imefungwa mechi tano na kushinda mmoja kwenye michezo saba iliyopita ya ligi waliyocheza ugenini, pia imeshinda mmoja tu kati ya tisa iliyopita katika Uwanja wa White Hart Lane.

Mshambuliaji wa Spurs, Kane, amefunga mabao saba katika mechi nne zilizopita za ligi, pia imepiga mashuti mengi yaliyolenga lango msimu huu kuliko timu nyingine yoyote ya ligi hiyo.

Spurs imepoteza mechi mbili tu kati ya 20 zilizopita walizocheza kwenye uwanja wa nyumbani. Huku Chelsea ikifunga mabao matatu tu katika mechi zake nne zilizopita za ligi.

Kiungo wa Chelsea, Cesc Fabregas, ametengeneza mabao 11 dhidi ya Spurs, matano zaidi ya timu nyingine yoyote kwenye ligi hiyo.

Mechi nyingine kali kesho, Liverpool iliyokuwa kwenye makali tokea ianze kunolewa na Mjerumani, Jurgen Klopp, itawaalika Swansea ndani ya Uwanja wa Anfield huku Arsenal ikisafiri kuwafuata Norwich, zote zikichezwa saa 1.15 usiku.

 

LEICESTER V MAN UNITED

Wakati shughuli hiyo ikiwa pevu kesho, leo saa 2.00 usiku kutakuwa na mtanange mwingine mkali kwa vinara wa ligi, Leicester City kuwakaribisha Manchester United walio nafasi ya pili kwenye Uwanja wa King Power.

Kocha wa Leicester City, Muitaliano Claudio Ranieri, atakuwa akiangalia tena namna wachezaji wake watakavyopambana na vigogo hao, akichagizwa na kasi nzuri ya nyota wake, Jamie Vardy na Riyad Mahrez.

Vardy ambaye ni mshambuliaji anaamini ya kuwa leo atavunja rekodi ya nyota wa zamani wa Man United, Ruud van Nistelrooy, kwa kufunga bao la 11 mfululizo baada ya kuifikia rekodi ya Mholanzi huyo ya kufunga mabao 10.

Akiwa na mabao 13 mpaka sasa kileleni kwenye ufungaji bora ndani ya mechi 13, Mwingereza huyo amekuwa na msimu mzuri sana akiisaidia Leicester kuongoza ligi kwa pointi 28 huku United wakiwa nazo 27.

MAN CITY V SOUTHAMPTON

Shughuli nyingine pevu itakuwa kwenye Uwanja wa Etihad kwa Manchester City kuwakaribisha Southampton, zote zikitoka kupoteza mechi zao zilizopita, Saints ikifungwa na Stoke City bao 1-0 huku Man City ikipigwa na Liverpool mabao 4-1.

 

Saints chini ya kocha Ronald Koeman, ina rekodi nzuri msimu huu, ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja ugenini ikishinda miwili na sare nne, ikiwemo ule walioichapa Sunderland kwenye mchezo wake wa mwisho wa ugenini.

 

City yenyewe ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 26 sawa na Arsenal, imeshinda mchezo mmoja kati ya minne iliyopita ya ligi, pia imepoteza mechi iliyopita ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kufungwa na Juventus bao 1-0 jijini Turin, Italia.

 

Msimu uliopita, Saints ilifungwa na City mabao 3-0 nyumbani, lakini vijana wa Manuel Pellegrini wakapoteza mchezo Etihad kwa kupigwa na Southampton 2-0.

 

Nyota wa Saints, Jay Rodriguez, ataukosa mchezo huo baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu wake mwanzoni mwa wiki hii, itamkosa pia staa wake, Graziano Pelle, anayetumikia adhabu, huku Fraser Forster na Florin Gardos nao wakiendelea kukosekana.

 

City itamkosa kipa wake tegemeo Joe Hart, nahodha Vincent Kompany, walio majeruhi huku mabeki Pablo Zabaleta na Eliaquim Mangala wakiwa kwenye hati hati ya kucheza, lakini itawapokea kiungo wake nyota David Silva na mshambuliaji Wilfried Bony, watakaorejea dimbani.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles